Mbowe aibomoa CUF


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version
Kumbeba Lwakatare kwa mbwembwe
Mwenyekiti wa CHADEMA,  Freeman Mbowe

WILFRED Lwakatare, anahamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), keshokutwa, Ijumaa.

Kwenye uwanja wa Uhuru mjini Bukoba, Lwakatare atapokea kadi ya Chadema kutoka kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Taarifa za ndani zinasema mkutano mkubwa wa hadhara umeandaliwa rasmi ili kusindikiza hatua hii ya mwanasiasa maarufu na muhimu kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kuhamia Chadema.

Wtakaoshuhudia hatua hii ya Chadema kupora hadharani kiongozi muhimu na mshuhuri mjini Bukoba ambako amewahi kuwa mbunge, ni pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.

Wengine ni wabunge Philemon Ndesamburo, Grace Kiweru, Zitto Kabwe; mjumbe wa Kamati Kuu Profesa Mwesiga Baregu na Balozi Christopher Ngaiza, mgombea ubunge wa chama hicho Muleba Kaskazini mwaka 2005.

Habari za ndani zinasema Lwakatare atahama na wanachama wengine wa CUF wakiwemo viongozi wa mashina, Kata na wilaya, pamoja na ndugu, marafiki na mashabiki wake.

Hii itakuwa mara ya kwanza CUF kukombwa wanachama na mmoja wa viongozi wake wa zamani ambaye walianza kutofautiana tangu Aprili mwaka huu.

Kwa hatua hii, CUF itakuwa imepoteza ngome yake ya Bukoba mjini ambako mashabiki wa siasa walimsimika Lwakatare katika ubunge kwa kipindi cha 2000 hadi 2005 alipong’olewa na Hamis Kagasheki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kuhama kwa Lwakatare kunaiweka pabaya CUF iliyokuwa na matumaini, angalau ya kiti kimoja Bara kutoka kwenye ngome yake kuu – Bukoba Mjini.

Si wanachama na wapiga kura wa Bukoba peke yao, bali hata Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wengine wa chama hicho, wamekuwa wakiamini kuwa hata mwaka 2005 Lwakatare alikuwa ameshinda lakini kura zake ziliibwa.

Hata hivyo, imefahamika kuwa baba yake Lwakatare, Mzee Muganyizi Lwakatare, anataka mwanae “aachane na siasa.”

Lakini taarifa zimeeleza kuwa baadhi ya wapenzi na wafuasi wake, wakiwamo ndugu zake wa karibu, wanamtaka ajiunge na Chadema ambayo katika miaka miwili ya karibuni imeibuka kuwa mshindani mkuu wa CCM.

Naye Lwakatare amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa tayari kuna kila dalili ya chuki ndani ya CUF ambako yameibuka makundi kati ya wanachama na viongozi kadhaa wa Bara na Visiwani.

Alisema juzi Jumatatu, kwa njia ya simu kutoka Bukoba, kwamba amesikitishwa na kauli za kibaguzi zinazotolewa sasa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

“Nimedhalilishwa na Mwenyekiti wangu, Profesa Lipumba. Pia amedhalilisha Watanzania Bara. Nadhani kauli yake kwa vyombo vya habari iliyochapishwa leo (Jumatatu) kwamba imekuwa ni kawaida kwa Wa-bara kujitoa kwenye chama cha siasa kwa sababu za cheo imetudhalilisha,” alisema Lwakatare.

Vyombo vya habari vilimkariri Lipumba akisema viongozi wa Bara wana tabia ya kuhama vyama pindi wanapokosa uongozi au kubadilishwa nafasi zao.

Lwakatare anasema Lipumba anafahamu fika sababu zake za kujivua uongozi, lakini  anakimbia hoja za msingi.

“Ninachokiona mimi kwenye chama hicho ni kwamba, sihitajiki tena. Hivyo hatima yangu ni ama nitaendelea kuwa mwanachama, kuhama au kuacha kabisa siasa; itajulikana kesho (jana) saa tatu usiku,” alieleza.

Baada ya kuwasilisha barua yake ya kujivua uongozi katika kikao cha Baraza Kuu la CUF, wajumbe waliagiza Lwakatare atafuwe na kujadili naye kwa kina masuala yake.

“Ajabu ni kwamba badala ya Profesa Lipumba kunitafuta, nasikia anajibu kwamba eti sipatikani kwenye simu; mbona ninyi watu wa vyombo vya habari mnanipata?” alihoji.

Amesema angekuwa hapatikani, basi asingejitokeza mbele ya televisheni au asingeitwa na chombo cha habari.

“Ningeitwa ningeitikia wito. Lakini sijaitwa, matokeo yake Katibu Mkuu (Seif Shariff Hamad), ananiandikia barua akisema: ‘Nakutakia kila la kheri kwenye chama unachokwenda,’ ” ameeleza.

Kauli hiyo ya Hamad ilichukuliwa kuwa na maana kwamba sasa Lwakatare hahitajiki tena CUF, na labda kuachia kwake vyeo kumewasuza roho wale “aliowanyima raha kwa muda mrefu.”

Wakati Lwakatare anazungumza na mwandishi wa habari hizo, alikuwa njiani kwenda Ibwera, kilometa 30 kutoka Bukoba mjini ambako pamoja na mambo mengine, anakwenda kuzungumza na wazee marafiki wa baba yake.

Wazee hao wameitana ili kujadili msimamo wa Mzee Muganyizi Lwakatare, baba yake Wilfred kwamba mtoto huyo ajiondoe kwenye siasa.

Kuna taarifa kwamba baba yake amemtaka mwanae aachane na siasa akiamini kwamba kijana wake ana umri na elimu ya kutosha kufanya shughuli nyingine.

Walio karibu na baba yake wameeleza kuwa mzee huyo anahofia mtoto wake kuuawa kutokana na mikikimikiki ya siasa.

Kumekuwa na hali ya mvutano kati ya  CUF na Lwakatare tangu mwishoni mwa mkutano mkuu wa uchaguzi ambako alifaulu kuingia Baraza Kuu lakini hakuteuliwa kuendelea na nafasi yake ya  Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara.

Badala yake, Lwakatare aliteuliwa na Mwenyekiti Profesa Lipumba, kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya chama chake.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: