Mbowe sasa amefungua njia


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Freeman Mbowe akiwa mahakamani Arusha

SITAKI kurudia historia ya matukio yaliyotokea jijini Arusha ambapo watu kadhaa waliuawa na kusababisha kukamatwa na hatimaye kufunguliwa kesi kwa viongozi kadhaa wa juu wa Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA), akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, pamoja na wanachama wengine wa chama hicho.

Nazungumzia amri ilitolewa na mahakama ya kumkamata Mbowe kwa kushindwa kufika mahakamani. Ni lazima tutambue kuwa huwezi kuwa na “utawala wa sheria” kwa kuchagua ni wakati gani utawala huo unautumia.

Hoja ya wanaotetea kukamatwa kwa Mbowe wanasema kama kiongozi huyo ameshindwa kufika mahakamani pasipo kutoa maelezo ya kutosha na mahakama ikalazimika kutoa “warranti”  kumkamata ili kumlazimisha kufika mahakamani, ni sawa.

Amri ya mahakama inapotolewa inatakiwa itekelezwe. Hatuwezi kuwa na mahakama ambayo inatoa maagizo halafu hayasimamiwi.

Watetezi hawa, baadhi yetu tunawashangaa. Wanataka tuamini kweli serikali ya Tanzania inazingatia utawala wa sheria? Kuna ushahidi mkubwa unaonyesha pasipo shaka kuwa utawala wa sheria ni dhana ambayo inatumika tu pale watawala wanapotaka. Na bila shaka tukikubali hivi, tutakuwa tunajiandalia madhara makubwa huko mbele.

Eneo mojawapo kubwa la wazi ambalo serikali imeshindwa kuheshimu utawala wa sheria, ni katika kesi ya madai iliyofunguliwa na mfanyabiashara Valambia.

Hii ni moja ya kesi ambazo tunaweza kuuliza watawala kiko wapi hicho kinachoitwa, “hakuna aliye juu ya sheria” na dhana ya “utawala wa sheria” Kesi hii ilihusisha mkataba wa ununuzi wa magari na zana za kijeshi.

Kwa karibu miaka 14 Valambhia bado anahangaika mahakamani kudai haki yake. Katika nchi inayofuata utawala wa sheria, serikali ingeshalipa Sh. 56 bilioni inazodaiwa hasa baada ya kubwagwa zaidi ya mara 10 mahakamani.

Kwenye nchi inayodai kuwa inafuata utawala wa sheria, mara baada ya kushindwa mahakamani, serikali ilitakiwa kulipa Varambia. Lakini wapi!

Badala ya kutekeleza hukumu, serikali ikasuasua jambo ambalo lilifanya Jaji Salum Masati kutoa amri ya kumfikisha mahakamani Dk. Daud Ballali aliyekuwa gavana wa benki kuu ya Tanzania kwa kugoma kumlipa mdai Valambia.

Wala Ballali hakwenda mahakamani. Polisi hawakwenda kumkamata. Ati wanafuata utawala wa sheria. Utawala wa sheria ulisema wamlipe, hawajafanya! Walimu wa sheria wanaweza kueleza vizuri kisa hiki kinachokwenda kinyume na utawala wa haki na sheria katika historia ya taifa hili.

Hata katika ununuzi wa rada ya kijeshi, pamoja na kelele tulizopiga baadhi yetu, kwamba ununuzi ule ulijaa ufisadi na wizi; taasisi ya uchunguzi ya makosa makubwa ya utapeli (SFO) walifanya uchunguzi na kugundua kuwa bei ya rada iliongezwa kwa karibu Sh. 21 bilioni, hatujawaona wanaodai “hakuna aliyejuu ya sheria wakishinikiza wahusika wafikishwe mahakamani.”

Nakumbuka niliandika barua kwa Bunge la Uingreza kueleza dhuluma hiyo. Barua hiyo ilisomwa bungeni na Norman Lamb. Nilielezea kile ambacho waziri wa Maendeleo wa Uingereza, Bi. Claire Short na wengine walikiona kuwa ni unyonyaji uliopita mipaka.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania, Jakaya Kikwete aling’ang’ania kuwa lazima rada ininunuliwe na akasema suala hilo linawahusu Watanzania wenyewe.

Waliokula njama za kununua rada wanajulikana. Walioidhinisha ununuzi wanafahamika. Waliokula fedha wanajulikana kwa majina na mahali wanapoishi. La kushangaza ni kuwa hatujawasikia watetezi wa utawala wa sheria kusimama na kudai watu hao wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Lakini katika suala la Mbowe wanaibuka na kusema, “hakuna aliye juu ya sheria.”

Hata wizi wa fedha za umma uliofanywa na kampuni ya Kagoda hakuna anayesema kuwa hakuna aliyepo juu ya sheria. Tulipoanza kupiga kelele wakati ule, tunakumbuka kwa masikitiko kauli za viongozi – “tukiwakamata Kagoda nchi italipuka,” huku wengine wakisema, “Kagoda hawakamatiki.”

Je, suala la kutokuwa juu ya sheria ni CHADEMA tu? Hawa Kagoda ambao wanajulikana vizuri kwanini hawajakamatwa? Nikitoa pendekezo kuwa hawa wako juu ya sheria,  mtu anaweza kuniambia kuwa nazusha?

Suala la “utawala wa sheria” au dhana ya “hakuna aliyejuu ya sheria” haihusiani na suala la wapinzani tu wanapochelewa kumaliza mkutano, au wanaposhindwa kutokea mahakamani hasa kama wana sababu ya msingi.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), inatuonesha jinsi sheria mbalimbali zilizotungwa zilivurugwa kwa maslahi ya watu binasi. Mfano hai, ni Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) na Sheria za Fedha Haramu.

Lakini hatujasikia kampeni ya “kamata kamata” ya watendaji ambao wamepoteza mabilioni ya shilingi. Hata hatujasikia mtu akisema kwa maneno na vitendo, kwamba “sheria zifuatwe.”

Lakini leo tunaambiwa ati kuna “utawala wa sheria” na kuwa hakuna aliye juu ya sheria.

Haki haitakiwi kuwa na macho. Ndiyo maana utaona yule mama Haki - sanamu ya mwanamke aliyeshika upanga upande mmoja na upande mwingine kashika mizani – inamwonesha akiwa amefungwa kitambaa machoni kwa lengo kuwa haki haina macho.

Kwa hiyo, hata kama yule mama ataletewa mtoto wake aliyehukumiwa kukatwa kwa upanga, basi upanga utamshukia kwani mama hajui upanga wa haki utamshukia nani.

Hapa nchini sanamu ya mama huyo haiwezi kuwa imefungwa kitambaa, bali inabidi jicho moja liwe nje! Kwani utawala wa sheria nchini unahusu kikundi cha watu wachache.

Ingawa ukiangalia kwa jicho la kengeza utaona kuwa kukamatwa kwa Mbowe na wenzake kunaweza kuwa sawa, katika mizani ya haki makosa wanayodaiwa kuyafanya hayawezi kulinganishwa na makosa ya watu kama Benjamin Mkapa, Robert Mboma, Andrew Chenge, Rostam Aziz, Daud Ballali na wengine.

Makosa ambayo kama kweli haki ingefuata mkondo wake, watu hawa na wengine tayari wangekuwa wako katika vyombo vya sheria muda huu.

Lakini safari hii wameamua kuwatisha wanasiasa wa upinzani kuwa watawakamata kwa kisingizio cha kufuata sheria. Hata hivyo, wamefanya kosa kubwa; kosa la majuto.

Kwani sasa wapinzani watasema sawa tumekubali mnafuata haki, basi tunataka mmkamate Kagoda. Hatuondoki hadi tuone Kagoda yuko ndani, wezi wa rada wako mahakamani, wezi wa EPA – wanaodaiwa kurudisha fedha na wasiorudisha – wako ndani, wakwapuaji wa mali ya umma kupitia mradi wa meremeta, Deep Green, wote wamepigwa pingu.

Watataka viongozi wa polisi walioagiza mauaji ya wananchi mkoani Arusha na Tarime nao watiwe pingu. Hayo yasipofanyika watakuwa na haki ya kutaka watawala waondoke madarakani kwa kushindwa kuheshimu utawala wa sheria. Wakifika hapo wasitokee wanaojiita, “utawala wa sheria uheshimiwe.”

Ole wenu ninyi mnaochagua nani apewe haki na nani asipewe. Ole wenu ambao mmeamua kuchukua upande wa wakandamizaji. Kukamatwa kwa Mbowe kunafungua ukurasa mwingine.

<p> mwanakijiji@mwanakijiji.com</p>
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: