Mbunge CHADEMA ateta na wajasiriamali


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
SUZAN  Lyimo

SUZAN Lyimo, mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ana ujumbe mzito kwa akina mama.

Akiwa amesimama mbele ya wanawake wapatao 100 na wanaume 19, kutoka vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA) jijini Dar es Salaam, Lyimo alitamka kwa ujasiri, “Wanawake msisubiri kununuliwa chupi na waume zenu.”

Papohapo alisikika mmoja wa akina mama hao akidakia, “Message delivered” – ujumbe umewasilishwa, kama isemwavyo kwenye simu za mkononi.

Lyimo alikuwa akimwakilisha Halima Mdee, mbunge wa Kawe aliyealikwa kuzindua “Tuamke Vicoba Group,” katika jengo la Nyamachabesi, Tegeta Nyaishozi, nje kidogo ya Dar es Salaam, yapata mita 600 kutoka barabara kuu iendayo Bagamoyo.

Mgeni rasmi alitumia mfano wa nguo muhimu kwenye eneo nyeti la mwili kwa shabaha ya kueleza nia na shauku ya kujiwezesha miongoni mwa wanawake.

Kauli ya Lyimo iliwafanya akina mama kugeukiana, kuangaliana kwa muda na kuanza kupiga makofi na kushangilia. Lakini kabla hawajamaliza kushangilia, Lyimo alikuja na nyongeza katika kuwaamsha akina mama kuondokana na fikra tegemezi.

Alianza kwa kukumbusha kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitaja, wakati nchi inapata uhuru, kuwa kulikuwa na maadui watatu wa taifa jipya. Akawataja kuwa ujinga, umasikini na maradhi.

Huku akipongeza kikundi kwa juhudi zake za kuweka akiba na kuendesha miradi, Lyimo alisema anaamini kuwa miongoni mwa maadui watatu aliowataja Nyerere, ujinga ndiyo adui mkubwa na mkuu.

Akiongea mara baada ya katibu wa Tuamke, Patricia Obadia kusoma risala ya kikundi chake, Lyimo alisema wanawake wasisubiri kuwezeshwa, kwani wana uwezo wa kujiwezesha.

Akioanisha adui ujinga na mazingira ya sasa, Lyimo alisema ni adui ujinga ambaye amefanya akina mama wengi kutojitambua kuwa wana uwezo mkubwa wa kujiwezesha.

Lyimo alisema akina mama wanapaswa kutafuta, kutafiti na kugundua kwanini wako jinsi walivyo katika jamii; kitu gani kimewafikisha hapo; nani anawasukuma huko; na hali na mazingira yapi yananawirisha mkondo huo wa kuwafanya wajione kuwa hawawezi mpaka wawezeshwe.

Alisema wakijielimisha hivyo, basi wataweza kama akina mama wa kikundi alichokuwa amekwenda kuzindua rasmi – Tuamke.

Kwa miaka 10 au zaidi sasa, kumekuwa na kauli za wanasiasa zinazolenga kuwavutia wanawake. Hizi zimepeperushwa mikutanoni, kwenye semina na makongamano.

Moja ya kauli hizo ni “Wanawake wakiwezeshwa wanaweza.” Nao akina mama wamekuwa wakikariri kuwa, “Tukiwezeshwa, tunaweza.”

Kauli ya kwanza imekuwa ikitolewa mara nyingi na viongozi wa kisiasa – wanaume na wanawake walioingia kwenye duara la mfumo dume na hawafikirii tena, kwa uzito unaostahili, mapambano ya wanawake ya kujikomboa kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiimani.

Nao wanawake, ambao wamekuwa wakiambiwa kuwa wakisaidiwa wanaweza kusaidika, wamefikia hatua ya kubuni chao: “Tukiwezeshwa tunaweza.”

Wengi wameshindwa kujiuliza: Je, tusipowezeshwa itakuwaje? Hii ndiyo hoja aliyojenga Suzan Lyimo, mmoja wa wanawake wasomi katika CHADEMA.

Kawaida uzinduzi wa Vicoba huandamana na michango ya papohapo kutoka kwa wanachama wenyewe, vicoba vingine vilivyoalikwa, wageni waalikwa na hasa mgeni rasmi.

Katika risala yao, akina mama walikuwa wamesema, “Tunapenda kukuomba wewe mgeni wetu rasmi na wageni wote kwa pamoja, kufumbua macho yenu na kuona na kutambua juhudi zetu katika kipindi kifupi cha ujenzi wa Tuamke Vicoba Group. Tumejitahidi.”

Hivyo kauli ya mgeni rasmi ilikuwa ikikubaliana na hoja ya wanachama wa Tuamke, kuwa msaada wowote kwao, hautakwenda kama mbegu; bali sehemu tu ya mbolea kwa mche uliochipuka na wenye uhakika wa kukua.

Kwani Tuamke, katika mwaka mmoja na nusu hadi kikundi kinazinduliwa rasmi Jumamosi iliyopita, tayari wametoa mikopo ya zaidi ya Sh. 16 milioni kwa wanachama wake. Wana akiba ya Sh. 6,800,000 /= katika mfuko wa hisa na Sh. 2,200,000/= katika Mfuko wa Jamii.

Kila mwanachama ana biashara yake ndogo. Mkopo unarejeshwa kwa riba ya asilimia 10. Hadi sasa wamekusanya Sh. 1,490,000/= kutokana na riba kwenye mfuko wa akiba; na Sh. 512,000/= kutokana na “adhabu” ndogondogo wanazotoza wanachama kwa kukiuka taratibu au kanuni zilizowekwa na kikundi.

Tuamke ambayo ina akaunti katika Benki ya Twiga Bancorp, Dar es Salaam ina mipango ya kuwa na jengo kubwa litakalokuwa na kumbi za mikutano kwa shughuli mbalimbali; huku ikiendesha kiwanda kidogo cha kutengeza sabuni.

Kwenye sherehe ya uzinduzi, Tuamke ilichangiwa zaidi ya Sh. 1,700,000 zikiwa ahadi na taslimu. Waliochanga ni pamoja na vikundi vya vicoba vilivyoalikwa; wanachama wa Tuamke, mbunge Suzan Lyimo, Benki ya Twiga Bancorp, ahadi ya Halima Mdee na wageni wengine waalikwa.

Kauli ya mbunge imekuwa chachu kwa wanachama wengi wa vikundi vilivyohudhuria. Ilikuwa baada ya sherehe kumalizika na akina mama wakiwa wanajipongeza kwa uzinduzi, wengi walikuwa wakiashiriana kwa kauli ya “Tunaweza.”

Mratibu wa vicoba kutoka asasi ya kijamii ya Umoja Youth AIDS Control and Community Development (UYACODE), yenye makao makuu Ukonga, Dar es Salaam, Bw. Aldo Mfinde; na ambaye amekuwa karibu na kikundi hiki kwa miezi minane sasa anasema, Tuamke ni moja ya vikundi vinavyompa “matumaini ya kukua haraka, kuimarika kiuongozi na kuwa mfano kwa wengine.”

Inafurahisha kusikia salamu za wanachama wa vikoba pale mwenzao au mgeni anapoashiria:

Vikoba: Jiwekee akiba kwa maendeleo ya kweli
Vikoba: Maendeleo ya kweli huduma za jamii na ujasiriamali
Maendeleo ya kweli: Kuwa mmiliki wa mtaji na riba.

Tuamke wana aina mbili za akiba: Mfuko wa Hisa na Mfuko wa Jamii. Hapa maendeleo siyo tena suala la kubishania. Wameanza. Wanaweza. Wataendelea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: