Mbunge: Katiba imevunjwa


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

HOJA ya Rais Jakaya Kikwete kusaini Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011-2016) kabla bunge kuujadili, imeibua shutuma kwa ofisi kuu nchini.

Waziri kivuli wa Mipango, Mchungaji Israel Yohana Natse (CHADEMA) ameliambia bunge kuwa Rais Kikwete alikiuka Katiba pale aliposaini mpango huo kabla bunge kuujadili.

Alisema rais alikiuka ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ibara hiyo inasema, majukumu ya Bunge ni pamoja na “kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo.”

Alisema wakati katiba ikitamka hivyo, mpango huu tayari ulishasainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, siku moja kabla ya kuwasilishwa bungeni.

Mchungaji Natse amesema mpango wenyewe kama ulivyowasilishwa bungeni tarehe 8 Juni, hauonyeshi iwapo ni rasimu.

“Aidha, kwa mujibu wa mpango wenyewe, Rais ameshashukuru wadau kwa maoni yao yaliyowezesha kukamilisha mpango na ameshalishukuru bunge kwa mchango katika kukamilisha mpango husika,” amelalamika mbunge wa CHADEMA.

Mbunge huyo wa Karatu amesema wakati rais anashukuru bunge, “Kambi ya Upinzani haijawahi kushirikishwa wala kushiriki kikao chochote cha Bunge kilichojadili na kupitisha mpango huu.”

“Kwa hiyo, Kambi ya Upinzani inamtaka waziri aeleze ni kikao kipi cha Bunge, na ni mkutano wa ngapi wa Bunge, uliowahi kujadili na kupitisha mpango huu wa maendeleo” na kupelekea rais kushukuru bunge kupitia dibaji ya kitabu cha mpango huo.

Kwa sauti ya kuonyesha uthabiti, Mchungaji Natse alitaka Bunge kufanya kazi zake “kikamilifu na serikali iwe na utamaduni wa kuheshimu hilo.”

“Tunaitaka serikali isiwe na utamaduni wa kuamini kuwa kila jambo litakalowasilishwa hapa, basi Bunge litalipitisha tu. Tunaitaka serikali kuhakikisha kuwa maoni ya wabunge yanazingatiwa na kuingizwa kwenye mpango huu kikamilifu.

Mbunge huyo alilaumu pia uamuzi wa kutumia Kiingereza katika kuandika mpango huo.

Alisema mpango huo unapaswa kusambazwa kwa wananchi kupitia wawakilishi wao kama wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji, madiwani na wabunge ili waweze kupanga mipango yao ya maendeleo kulingana na mpango huu.

Viongozi wengi ambao ni wadau wa mpango huu, hawajui ligha ya Kiingereza. Alitaka baada ya kuujadili, serikali iutafsiri kwa Kiswahili kwa matumizi mapana ya wananchi na viongozi wao.

Kuhusu mikakati na malengo katika vipaumbele mahsusi, amesema mpango huu hauna shabaha za “kutuwezesha kujipima kama taifa kuhusu mafanikio tunayotegemea kuyafikia…”

Alipendekeza baadhi ya shabaha kuu za mpango zuwe:

  • Kupunguza umasikini vijijini kutoka asilimia 37 ya sasa na kufikia asilimia 20.
  • Kumaliza kabisa tatizo la umeme na kuzalisha umeme wa ziada kwa asilimia 20.
  • Kuwa Taifa linalozalisha gesi kwa wingi barani Afrika.
  • Kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanapata maji safi na salama.
  • Kuhakikisha kuwa barabara za vijijini zinapitika kwa wakati wote wa mwaka.
  • Kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Kuhusu utawala bora, mchungaji Natse amesema upembuzi wa kina uliofanywa na Kambi ya Upinzani, umebaini kuwepo kwa mapungufu mengi yanayoathiri utekelezaji wake.

Amesema wakati wananchi wakishinikiza kuanza mapema kwa mchakato shirikishi wa kuandikwa kwa katiba mpya ili, pamoja na mambo mengine, wapate haki ya kuweka mifumo thabiti ya kusimamia uwajibikaji wa utawala kwa umma; kilio chao hicho hakionekani kuzingatiwa kwa uzito unaostahili.

“Kambi ya Upinzani tumeshangazwa na mpango huu kutolipa kipaumbele hata kidogo hitaji la katiba mpya; wala kutenga fedha maalum kwa ajili ya mchakato huo nyeti, katika kuamua hatma mpya ya mwelekeo wa taifa letu,” ameeleza.

Amesema nguzo kuu ya utekelezaji wa mipango na malengo yote mazuri ni kuwepo kwa utawala bora na wenye kuwajibika kikamilifu na kwamba mchakato wa katiba mpya ulipaswa kupewa uzito mkubwa kwa kuwa ni nguzo kuu ya maboresho yote ya ndani.

Hata kama serikali itasema kuwa kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya tume ya kurekebisha sheria, amawasilisha Mchungaji Natse, bado kambi ya upinzani inataka kuona fedha za mchakato wa katiba mpya zikitengwa.

Kuhusu chanzo cha fedha za kurekebisha sheria, Mchungaji amesema kambi ya upinzani inaona ni aibu kubwa kwa taifa kufikia hatua ya kuomba fedha nje kwa ajili ya kurekebisha sheria za ndani.

Wziri kivuli amesema mpango huu umeshindwa kuweka bayana jinsi utakavyoinua uchumi wa vijijini (rural economic growth), ambao kimsingi ndio utakaoweza kupunguza moja kwa moja umaskini wa wananchi wengi.

Amesema mpango umejikita katika kushughulikia vipaumbele vilivyoainishwa kwa ujumla wake kwa kuanzia juu kwenda chini, bila kuzifanyia uwekezaji wa moja ya fursa nyingi za kiuchumi zilizopo katika ngazi za chini za utawala, kama wilayani na vijijini, ambako ndiko wengi wanaweza kukombolewa.

Mchungaji Natse amehoji ni kwa kiasi gani wananchi wameshirikishwa kwenye kuandaa mpango huu akisema “…au tunataka washiriki kwenye utekelezaji tu?”

Amesema mipango mingi inakwama kwa sababu wananchi wanaachwa kwenye hatua za utayarishaji na hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji.

“Mheshimiwa Spika, ukisoma mpango huu utaona kuwa hakuna ufafanuzi wa Wadau wa Maendeleo ambao serikali imewaainisha kuwa watachangia katika kutekeleza mpango huu. Hili litaleta shida ikiwa wadau wengi watashindwa kutekeleza ahadi zao au kutekeleza wakiwa wamechelewa,” amewasilisha.

Ametaka serikali kuweka bayana orodha ya wadau ambao wameonyesha nia ya kuuchangia mpango huu ili wajulikane na kiasi cha ahadi walizoahidi.

Amesema Kambi ya Upinzani inaona haja ya mpango huu kutekelezwa kuanzia ngazi ya halmashauri huku jukumu la serikali kuu likibakia kuwa ni la kuratibu utekelezaji.

“Kwa kufanya hivyo, utekelezaji wa mpango huu utaweza kugusa wananchi moja kwa moja kuliko kuweka mamlaka ya utekelezaji kwenye ngazi ya serikali kuu pekee. Utekelezaji wa ushauri wetu huu utaufanya ile dhana nzima ya serikali ya ugatuaji wa madaraka itekelezeke,” amesema.

Mchungaji Natse ametaka serikali kueleza kwa kina ni mikakati gani ya kukabiliana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya nchi ili kuhakikisha kuwa mpango huu unatekelezwa kikamilifu ndani ya miaka mitano kwa makadirio ya fedha yaliyowekwa sasa.

“Vinginevyo, mpango huu utakuwa hautekelezeki, na tutajikuta tukilazimika kuufanyia mapitio (review) ili kuweza kukabiliana na kushuka kwa thamani ya shilingi,” ameeleza.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: