Mchungaji Msigwa: Tuna viongozi legelege


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 July 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Mchungaji Peter  Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini

HANA makeke. Ni mpole, lakini mwenye msimamo thabiti wa kutetea anachokiamini. Si mwingine, bali Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Bunge la Muungano katika jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, pamoja na mambo mengine, Mchungaji Msigwa anasema kuna tofauti kubwa kati ya wabunge wa CHADEMA na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anasema: “Wabunge wa CHADEMA wanalazimika kufanya kazi mara kumi zaidi ya ile inayofanywa na wabunge wa CCM, kwa sababu, wabunge wa CCM wamekuwa na utamaduni mchafu wa kutanguliza mbele maslahi ya chama chao kuliko maslahi ya taifa. Unapokuwa mbunge wa CHADEMA unakuwa pia mbunge wa wananchi wote wa Tanzania.

“Unapofikiri uwafanyie nini wapiga kura wa jimbo lako, papo hapo unatakiwa kufikiri uifanyie nini nchi yako. Unatakiwa ufikiri utawasaidiaje Watanzania wengine kutatua matatizo yao. Ni kwa sababu wabunge wa CCM wamekuwa wakiutumia wingi wao vibaya kupitisha mambo ambayo kila mwenye kulitakia mema taifa hili anaona si sahihi.

“Hata wale wachache miongoni mwao wanaotaka kujitutumua kutetea maslahi ya taifa, wanabanwa na chama chao kukubaliana na kila linaloletwa na serikali hata kama halina maslahi na taifa.”

Mchungaji Msingwa anasema, pamoja na changamoto hiyo kubwa inayowakabili wabunge wa chama chake, bado wanajivunia wajibu huo mkubwa waliojitwisha kuwakilisha Watanzania.

Alizungumzia kilichomsukuma kujitumbukiza katika ulingo wa kisiasa, tena kupitia vyama vya mageuzi, wakati yeye ni kiongozi wa kidini, Mchungaji Msigwa anasema: “Nimeingia kwenye siasa ili wasio na sauti waweze kusikika.

“Katika maandiko matakatifu walikuwapo watumishi wa Mungu waliosimamia haki na kuonya watawala walioenda kinyume cha maagizo ya Mungu. Mfumo tulionao unakandamiza wanyonge. Kwa hiyo, mimi kama Mchungaji napaswa kufanya kila niwezalo kuhakikisha haki za wanyonge zinasikilizwa na kuheshimiwa.”

Mchungaji Msigwa ni miongoni mwa wabunge 48 wa chama hicho wanaochangamsha Bunge kwa hoja nzito.

Akiwa ameingia Bungeni kwa mara ya kwanza, Mchungaji Msigwa anatambua changamoto tatu zinazomkabili. Anasema:
“Kwanza, changamoto kubwa ninayokumbana nayo ni jinsi ya kuwawakilisha wananchi wa Iringa Mjini na Watanzania kwa wakati mmoja.

“Ni changamoto ya kupambana na kasi ya muda, ili kuutumia vizuri katika kushughulikia masuala yote ya kijimbo na ya kitaifa.

“Nikiwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, nina majukumu mengine zaidi ya kuhakikisha utajiri wa utalii na maliasili ya nchi hii vinatumika vizuri kuwanufaisha Watanzania, na kuishitaki serikali kwa wananchi pale inapoendeleza ufisadi na sera mbovu zisizowanufaisha wananchi.

“Pamoja na changamoto hiyo kubwa inayotukabili wabunge wa CHADEMA, bado tunajivunia wajibu huo mkubwa tuliojitwisha wa kuwakilisha Watanzania.

“Ndiyo maana Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipotumia magari zaidi ya 50 ya kifahari na ndege mbili katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa, nilisimama kupinga hatua hiyo. Niliona huu ni ubadhirifu unaochangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwa sababu, fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo zinatumika kwa safari za anasa. Hili nililifanya bila kuujali Pinda ametembelea mkoa wa Iringa.

“Pili, kuna changamoto ya kubadilisha mtazamo wa wananchi (mind set) kuhusu majukumu ya mbunge. Baadhi ya wananchi wanamtazama mbunge kama mfadhili badala ya kumtazama kama mwakilishi na mtetezi wao.

“Baadhi wanafikiri kazi ya mbunge ni kutumia fedha zake binafsi kujenga barabara, shule au kugharamia shughuli nyingine za kimaendeleo. Hiyo si kazi ya mbunge, na hata ingekuwa ndiyo kazi ya mbunge basi isingewezekana kwa mshahara wa mbunge kufanya shughuli kubwa za kimaendeleo kwa ajili ya wananchi.

“Mbunge kama mtu namba moja anayeguswa na kero na matatizo ya watu wa jimbo lake, anaweza tu kuchangia baadhi ya shughuli za kimaendeleo kama watu wengine, lakini majukumu ya msingi ya mbunge, mbali na kuwasilisha kero na matatizo bungeni, ni kuhakikisha kodi inayolipwa na wananchi wote pamoja na mapato yatokanayo na raslimali za nchi, vinatumika kuwaletea maendeleo. Kwa hiyo, wakati nashughulikia kero na matatizo ya wananchi, nachukua pia wajibu wa kuwabadili mtazamo.

“Tatu, changamoto nyingine ni mbunge aliyenitangulia (wa CCM) ambaye alikuwa anapenda kuwapa baadhi ya wananchi vitu vidovidogo kama mchele, maharage, na kuwafanya baadhi yao waamini kuwa hayo ndiyo maendeleo, na hiyo ndiyo kazi pekee na ya msingi ya Mbunge, kumbe sivyo.

“Mimi sitawarubuni wananchi wa jimbo langu kwa kuwapa vitu vidogo vidogo. Badala yake, nitahakikisha napigania mgawo mzuri wa fedha zao kutoka kwenye bajeti kuu ya serikali na ile ya halmashauri, ili wapate maendeleo ya kweli na endelevu kwa manufaa ya vizazi vya leo na kesho, kama nilivyowaahidi katika kampeni zangu. Kazi hiyo nimeshaanza.”

Ingawa amekaa Bungeni kwa miezi saba tu, Mchungaji Msigwa anasema amejifunza mambo kadhaa, na ana matarajio kadhaa.

“Mwanzoni tulidhaniwa kuwa hatujui kitu kwa sababu ya ugeni wetu, lakini kama nilivyojibu swali lako la kwanza, ni kujifunza mfumo huu uliopo, na wakati unaendelea kujifunza unapaswa kuwawakilisha wananchi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla.

Matarajio yangu ni kuwa na bunge linalojadili mambo ya msingi yanayolihusu taifa bila kuoneana aibu. Bunge la sasa halinifurahishi kabisa kwa sababu wenzetu kutoka CCM wanaweka ushabiki wa kichama ndani ya Bunge hata kwenye mambo ya msingi,” anasema.

Hata hivyo, Mchungaji Msigwa anasema anatumaini wabunge hawa watabadilika.

Anakiri kwamba licha ya uchanga wake Bungeni, yu miongoni mwa wabunge wachache wanaoheshimika kwa wananchi kutokana na kuichachafya serikali. MwanaHalisi lilitaka kujua siri ya mafanikio yake.

“Siri ya mafanikio yangu ni huduma ya kichungaji. Mtu moja aliwahi ‘kama kuna jambo muhimu linaendelea kukaa kimya ni kuenzi uwongo; na kama utaamua kukaa kimya maana yake nawe ni mwongo.’

“Kwa kuwa namheshimu Mungu siwezi kukaa kimya ninapoona mambo hayaendi inavyopaswa kwenda, utakuwa ni uwongoa nami pia nitakuwa mwongo.

“Taifa hili tuko katika kipindi ambacho maadili ya uongozi yametoweka, viongozi wanasema wasiyoyaamini. Naomba ieleweke sipo bungeni kuichachafya serikali, nipo bungeni kusimamia na kuishauri serikali bila kumuonea mtu. Viongozi tuna sehemu muhimu sana katika jamii.

“Ukiwa na baba dhaifu utakuwa na familia dhaifu. Vilevile ukiwa na kiongozi dhaifu tarajia taifa dhaifu. Kwa bahati mbaya viongozi wetu hawataki mabadiliko ambayo yatatupelekea kupevuka.”

Anazungumzia pia matarajio ya wana Iringa mjini katika miaka mitano ya ubunge wake.

“Kwanza, watarajie mabadiliko makubwa ya kimtazamo na kifikra. Bunge ni kioo cha taifa. Ni maombi yangu kuwa uwakilishi na fursa hii niliyoipata iwe ni baraka kwa kila Mtanzania. Mchango wowote nitakaoutoa uwe na faida kwa Watanzania na mustakabali wa taifa letu.

“Pili, watarajie kuwa sitaweza kukaa kimya pale ambapo Bunge litatumika kama mhuri wa kupitishia mambo ya serikali.”

Kwa mujibu wa Mchungaji Msigwa, CHADEMA ndilo tumaini pekee la Watanzania, kwa maana ndicho chama chenye mwelekeo.

Anawataka wananchi kwa wakiunge mkono kwa hali na mali, maana yeye na wenzake tayari wameshajitoa kikamilifu kukitumikia chama na taifa. Ameoa na ana watoto.

0
Your rating: None Average: 4.6 (5 votes)
Soma zaidi kuhusu: