Membe: Wizi ulipangwa Hazina


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
WAZIRI wa Mambo ya Nje, Bernard  Membe

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema njama za kuiba mabilioni ya shilingi ya safari za Rais Jakaya Kikwete, zilifanikishwa na maofisa wa Hazina.

Amesema maofisa wa Hazina walikiuka taratibu za kutoa fedha kwa wizara yake.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam juzi, Membe amesema anatuhumu watendaji wa Hazina kwa kuhusika na njama hizo “…hawa wanajua taratibu za kutoa fedha kwa wizara yetu.”

Waziri Membe amesema kwa mujibu wa taratibu, mwenye mamlaka ya kuomba fedha Hazina ni waziri husika, naibu waziri, katibu mkuu, na naibu katibu mkuu.

Amesema hata baada ya viongozi hao kuomba fedha, lazima maofisa wa Hazina waende kwa mhasibu mkuu wa wizara husika ambaye atathibitisha iwapo kiasi cha fedha ambacho waziri anaomba, kipo na katika akaunti ipi.

“Sasa kilichofanyika hapa, ni kwamba waliokuwa wanakaimu nafasi walifanikiwa kutoa fedha hizo benki. Jambo tunalojiuliza ni nani aliidhinisha fedha hizo kutolewa Hazina?” alihoji Membe.

Membe amehoji, “Waziri wanamfahamu, naibu waziri, katibu mkuu na naibu katibu mkuu wote wanawafahamu. Wao ndio wataalamu wa fedha, wanafahamu taratibu za utoaji fedha; ilikuwaje wakatoa fedha kiasi kikubwa kama hicho bila idhini ya wale wanaowafahamu kuwa ndio wenye mamlaka?”

Amesema wakati fedha hizo zinachotwa, hakuwapo. Naibu Waziri, Mahadhi Juma Maalim hakuwapo; pia Katibu Mkuu John Haule na hata naibu wake, Balozi Rajabu Gamaha, hakuwapo.

“Ilikuwaje basi Hazina watoe fedha zote hizo kwa viongozi wanaokaimu nafasi zetu? Hilo ndilo linalochunguzwa,” anasema waziri Membe.

Membe alikuwa anatoa ufafanuzi wa habari kwamba maofisa watano wa wizara yake wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuiba fedha zilizotengwa “kwa ajili ya safari za rais.”

MwanaHALISI lilikariri taarifa za wizara na ikulu katika toleo lililopita zikisema kwamba maofisa hao, akiwemo Mkuu wa Itifaki, walifanikiwa kuchota Sh. 3.5 bilioni “kutoka benki moja nchini.”

Ilielezwa kuwa fedha hizo zilikuwa sehemu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi katika safari za rais kwa ziara za Geneva, Uswisi; Rio de Janeiro, Brazil; Addis Ababa, Ethiopia na safari ya ndani ya nchi – kwenda Arusha.

Maofisa waliosimamishwa ni pamoja na Mkuu wa Itifaki aliyetajwa kuwa ni Anthony Itatiro. Wengine ni ofisa katika Idara ya Itifaki, Shamim Khalfan; Kaimu Mhasibu Mkuu, Kasim Laizer; Mhasibu aitwaye Deltha Mafie na karani wa fedha Shabani Kesi.

Membe alisema, “…wizi huu umefanywa kwa ujanja wa hali ya juu na kuna mtandao mkubwa ambao Tume iliyoundwa itauweka wazi. Matokeo ya uchunguzi hayatakuwa siri.”

Waziri Membe amefafanua kuwa mtandao huo ulifanikiwa kuchukua kiasi hicho cha fedha, 8 Machi 2012 kutoka Benki ya NMB, tawi la Bank House lililoko Barabara ya Samora, katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Amesema pamoja na kufanikiwa kuchota fedha hizo, hawakuweza kugawana kwa sababu walinaswa na fedha taslimu walipokuwa wanataka kugawana. Maofisa usalama wa wizara ndio waliowafuma na kuwakamata.

“Kwa hiyo, hata senti moja haikupotea, fedha zote zilirudishwa,” amesema.

Katika suala hilo, Membe amesema, “…sisi tumeshika mkia na sasa tunatafuta kichwa. Kinachotafutwa hapa ni kichwa. Na hicho kichwa kitapatikana.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: