Mfumo dume wa uchaguzi unadumaza demokrasia


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Celina Kombani

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani anatamba: "Uchaguzi umefanikiwa kwa asilimia 98."

Kombani, mbunge wa Ulanga Mashariki, mkoani Morogoro, katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) yaliyofanyika asubuhi Jumatatu, alitaja kasoro moja tu aliyoita “kubwa.”

Kasoro hiyo katika uchaguzi uliofanyika nchi nzima Jumapili, 25 Oktoba, ilitokea mkoani Lindi ambako vifaa vya uchaguzi havikufikishwa.

Ni kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Kutofika kwa vifaa hadi saa 7 mchana, kulisababisha uchaguzi kuahirishwa na waziri akasema uchaguzi utafanyika baada ya siku saba.

Ingawa alisema kwingineko kulitokea kasoro ndogondogo “za kawaida,” alikiri maeneo ya Wilaya ya Kilindi, na Tanga kulikuwa na matatizo pia.

Akasema inaonekana kuna chama kimoja chenye watu wakorofi kilihusika na hayo. Hakukitaja, lakini aliendelea, “Inashangaza siku zote chama hicho huwa kinaleta ukorofi.”

Waziri Kombani ambaye ni mwanachama na kiongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) anatuhumu chama fulani kwamba kina watu wakorofi na akaelekeza wananchi “waelewe hivyo.”

Nilitarajia yatabainishwa matatizo mawili au matatu tu na hayo yatumike kigezo cha ufanisi wa serikali katika jukumu la kusimamia uchaguzi huu.

Nilijua tu kwa kuwa ni utamaduni viongozi wa serikali kutoa visingizio vya tatizo sugu la usimamizi wa uchaguzi, itatumika mifano michache kulaghai wananchi.

Hapa ukweli haujasemwa. Matatizo mengi yanayotokea kwenye uchaguzi, ukiwemo ule mkuu wa madiwani, wabunge, wawakilishi na marais, chimbuko lake ni mambo mawili makuu.

Kwanza, kutokuwa tayari kwa chama tawala, CCM, kustawisha demokrasia ya kweli. Kustawisha demokrasia ya kweli kunatakiwa kuwe kwa matendo siyo matamko peke yake ya viongozi.

La pili serikali ya CCM kuendekeza mfumo mbaya wa usimamizi wa uchaguzi. Hili linatokana na hilo la kwanza.

Nataka ieleweke kuwa tatizo la mfumo-dume katika uchaguzi. Kama ulivyo ule wa kimaamuzi kuweka kando wanawake katika ushiriki wa mipango na maamuzi ya mambo ya maslahi na nchi, ndivyo ulivyo mfumo wa uchaguzi Tanzania.

Ukichunguza, utabaini wakati wa uchaguzi, maeneo ambayo CCM haina hofu ya kushindwa, hakutokei matatizo ya kuchelewesha uchaguzi kufanyika. Husikii tatizo la vifaa wala chochote. Kila kitu huenda vizuri; tofauti na yale ambayo chama hiki wanajua wamekabwa koo.

Mkoani Lindi, Tanga, maeneo mengi ya visiwani Zanzibar na Dar es Salaam yanajulikana kwa kupata matatizo ya kuvuruga uchaguzi kila unapofanyika uchaguzi.

Maeneo ambamo vyama vya upinzani vimejijenga, hata matokeo ya uchaguzi hucheleweshwa na mwingine yakitangazwa lazima pawe na ulinzi mkali, maana mengine yamechezewa kunufaisha CCM.

Katika maeneo haya, hata hivyo, si kutwa kusikia watu wasiojulikana wamepora masanduku ya kura. Mfano mzuri ni Karatu na Tanga. Hayo ni matokeo ya mfumo dume kufanya kazi.

Wasimamizi wa uchaguzi mkuu, wakurugenzi wa halmashauri, na wale wanaosimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao ni maafisa watendaji, wote wanateuliwa na mfumo dume unaolindwa na CCM.

Kanuni za uchaguzi hufuatwa zaidi mle ambamo vyama vya upinzani havina nguvu. Maeneo ambamo CCM inakabiliwa na ushindani, kanuni zinavunjwa na wanaofuatilia kusakamwa.

Maeneo kama hayo, polisi hawalindi wananchi, bali maslahi ya CCM na wanatishia watu wenye msimamo wa kukataa udikteta. Ikitokea mpiga kura anaulizwa kitambulisho, akibisha tu, anatishiwa hata bunduki.

Haya yametokea maeneo mengi ya Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Dodoma, Arusha, Manyara ambako CCM ilitaka ushindi kwa nguvu.

Ni katika maeneo kama haya, askari huwa hawasikilizi mtu isipokuwa viongozi wa serikali na makada wa CCM. Hapo si rahisi haki za wagombea wa upinzani kuzingatiwa. Na wakiwa “ngangari” kufuatilia mwenendo wa uchaguzi, si kutwa wakaishia kudhalilishwa.

Sikiliza kadhia iliyotokea kijiji cha Kibilashi, wilayani Kilindi, Tanga: Huku hakuna uchaguzi, ni vurugu tupu, wagombea wetu wametishiwa usalama wao wasipojitoa. Kweli walijitoa siku ya uchaguzi. CCM walipobaini tumeshinda wakaibuka makomandoo wao na kupora masanduku ya kura na kwenda kuyachoma moto.”

Usiku wa mkesha wa uchaguzi, zilienea taarifa kutoka Kilindi kuwa mbunge mmoja alifuatana na vijana wa CCM hadi kijiji cha Gezaulole na kupitia wagombea wanaopinga wale wa CCM, na kuwahonga kila mmoja Sh. 50,000.

Katika eneo hilo, wagombea wengi wa Chadema wamejitoa dakika za mwisho. Wale waliokataa kujitoa, walikwenda mafichoni.

Kituo cha uchaguzi cha Mwananyamala Kisiwani, Dar es Salaam palizuka zogo. Inajulikana eneo hilo CUF ina nguvu, lakini CCM ikitaka kutoka mshindi. Polisi wapatao 40 walipelekwa mapema asubuhi na kuzusha mtafaruku usio lazima.

Hali ilikuwa mashaka matupu wilayani Karatu ambako kunajulikana kulivyo ngome imara ya CHADEMA, chama kinachoshikilia halmashauri ya wilaya. Kwa kuwa CCM imekuwa na mikakati ya kudhoofisha nguvu za Chadema, dola ilishusha askari wengi na kusababisha mivutano mingi.

Katika jimbo la Kawe, wakati wananchi walikuwa wanashangilia ushindi waliopata CUF katika baadhi ya mitaa, wasimamizi wa uchaguzi walitumia muda mrefu kujivuta hata walipotangaza matokeo.

Hali kama hiyo ilikuwapo Msewe, kitongoji maarufu pembeni mwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Orodha za wapiga kura zilikuwa hazionekani kirahisi, jina la mgombea wa CCM lilikosewa kusudi kutoa nafasi ya jingine kuandikwa kwa kalamu. Bado hadi saa 7 mchana Jumatatu, msimamizi wa uchaguzi, Paul Ngunga alikuwa hajatangaza matokeo.

Wananchi ambao sehemu kubwa walikuwa wamejizatiti kubadilisha uongozi, walilalamika kutotangaziwa matokeo kwa wakati ingawa upigaji kura ulimalizika ilipofika saa 10 alasiri.

Ngunga alipoulizwa, alisema alitangaza matokeo usiku wa Jumapili baada ya taratibu kukamilika. “Nilitangaza matokeo tangu jana usiku na nipo ofisi za Kata kusaini hati muhimu ili nipeleke matokeo kunakohusika,” alisema.

Lakini mgombea uenyekiti wa mtaa kupitia CHADEMA, Chesko Daniel Lupumbwe, alipinga na kueleza matokeo hayakutangazwa hadi mchana isipokuwa yalibandikwa saa 7 mchana nje ya ofisi ya serikali ya mtaa. Kwa muda mrefu alisema wakimtafuta mtendaji ofisini hakupatikana.

Ngunga alisema Jafari Juma Nyaigesha wa CCM alishinda uenyekiti kwa tofauti ya kura 26 dhidi ya Chesko aliyepata kura 491. Jafari alipita na wagombea wake wote wa nafasi za ujumbe na viti maalum katika uchaguzi ambao idadi ya kura zilizotangazwa, zilizidi zilizopigwa. Chesko aliahidi kupinga matokeo hayo mahakamani.

Askari wengi walipelekwa Msewe ambako kama ilivyokuwa kwa maeneo mengi ya Dar es Salaam kulikokuwa na upinzani, majina ya wapiga kura yalibandikwa katika karatasi zisizoonekana vizuri na kusababisha watu kadhaa kuamua kuondoka bila ya kupiga kura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: