Mgodi wa Lusu karaha tupu

KILE kinachoitwa uhusiano mwema hakionekani kati ya Resolute (Tanzania) Limited (RTL), kampuni inayoendesha mgodi wa dhahabu wa Lusu uliopo Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, na wananchi wanaoishi maeneo yanayouzunguka.
Hivyo kauli ya RTL kwamba inatambua umuhimu wa kuishi vizuri na majirani kwa kuwa wana mchango mkubwa katika kuzifanya shughuli za mgodi kwenda vizuri, ni sawa na “danganya toto.”
Kila niliyekutana naye katika ziara ya kutembelea vijiji vya karibu na mgodi huu, anatoa simulizi zinazothibitisha uhusiano mbaya uliopo kati ya wawekezaji na jamii.
Katika siku ya tatu ya ziara ya kusikiliza maoni ya wananchi wanaotazamana na mgodi wa Lusu, ambao kulingana na taarifa za kiserikali una akiba ya dhahabu ya kiasi cha tani 76.82 wakati wa utafiti, nilikataliwa kusogelea geti la kuingilia mgodini upande wa kitongoji cha Mkwajuni kinachopakana na mgodi.
Walinzi walinisimamisha kabla ya kukaribia geti pale mmoja wao aliposema, “Unatakiwa kusita ulipo. Unafuata nini huku. Hatuna kibali cha kuruhusu mgeni hapa. Tafadhali geuka nyuma uendelee na zako.”
Hapo ndipo niliomba namba ya Ofisa Uhusiano lakini walinzi waliniangalia kwa muda mfupi na kunipa mgongo. Hapa nilipata picha kuwa kuendelea kuwadadisi ni kutafuta mgogoro nao. Nimehangaika kutafuta namba ya simu ya Ofisa Uhusiano bila mafanikio.
Naye mmoja wa viongozi watendaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Omary Mohamed Nganya, anasema uhusiano wa halmashauri na wawekezaji wa Lusu, unaishia kwenye malipo ya ruzuku.
Kila mwaka, Halmashauri ya Wilaya inapata ruzuku ya Sh. 200 milioni kutoka mgodi huo, malipo yanayolenga kusaidia mipango ya halmashauri, ameeleza Nganya ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya.
Anasema kama wananchi wanalalamika kusumbuliwa na walinzi wa mgodi, hali ya mambo iko hivyohivyo kwa watu wengine; hata kwao viongozi wa halmashauri.
Anasema hakuna kiongozi kati yao anayeota kuwasiliana na viongozi wa kampuni inayochimba dhahabu kwenye mgodi huo kwa jambo lolote lile.
Juu ya matumizi ya fedha zinazotolewa na mgodi kila mwaka, Nganya anasema yanapangwa kwa kujumuisha mahitaji ya kibajeti ya halmashauri nzima.
Miongoni mwa matatizo niliyoelezwa kijiji cha Mwaluzwilo, makao makuu ya Kata ya Lusu, ni kinachoitwa unyanyasaji unaofanywa na polisi kwa kuwakamata na kudai kuwa wananunua na kuuza mafuta ya kuendeshea mitambo yanayosadikiwa kuibwa mgodini.
“Hata mtu ukihangaika kupata chakula chako unasingiziwa unang’ara kwa sababu ya biashara ya mafuta yanayoibwa mgodini. Hata ukikutwa na madumu umebeba kwenye baiskeli yako, hata kama hayana kitu, unaambiwa unapanga kununua mafuta ya mgodi. Unakamatwa,” anaeleza Mgalula.
Baadhi ya watu wanakiri mafuta mengi yanaibwa mgodini na wapo waliojenga nyumba kutokana na biashara hiyo. Wanauliza kama walioko mgodini wanatoa mafuta, kwa nini wao wasiyachangamkie.
Shukurani kidogo kwa RTL ni kusaidia mradi wa ng’ombe wa kisasa ambao kinyesi chao kinatumika kuzalisha nishati ingawa haujawa endelevu. Gharama zake ni kubwa na hakuna msaada huku uongozi wa shule ukiwa na kigugumizi kuuendeleza.
Hakuna zahanati karibu. Wajawazito na wagonjwa wengine wanabebwa kwa baiskeli kupelekwa zahanati za mbali na watoto wanasoma kwa shida.
Bi Angelina Ngasa wa kitongoji cha Mkwajuni ni mfano mzuri. Mtoto wake, Amos Fabian, alishindwa kujiunga na sekondari ya Mwaluzwilo, iliyoko kiasi cha kilomita 15 kutoka hapo, kwa sababu ya kukosa ada na mahitaji mengine.
Ilikuwa baada ya mahangaiko ya muda mrefu, Angelina alipata fedha kidogo akanunua sare na madaftari machache na kumpeleka Amosi shule Aprili mwaka huu badala ya mapema Januari.
Hata hivyo, ilimchukua Amosi wiki tatu tu kabla ya kurudishwa na uongozi wa shule kwa madai eti jina lake halikuwa katika orodha ya waliotakiwa kujiunga.
Madai hayo yametolewa kama vile si uongozi huohuo uliompelekea Amosi fomu ya kujiunga na shule kwa barua ya 23 Desemba 2009 iliyosainiwa na Kaimu Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Mwaluzwilo, S. Majegule.
Katika barua hiyo ambayo niliiona, Mwalimu Majegule anampongeza Amosi kwa kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza, anamkaribisha kujiunga na anamtakia masomo mema.
Barua ilikuwa inaeleza mahitaji anayotakiwa kwenda nayo shuleni. Baadhi ni Sh. 5,000 za tahadhari, Sh. 5,000 (kitambulisho), Sh. 4,000 (fulana na nembo ya shule), Sh. 10,000 (sweta), Sh. 2,000 (nembo katika shati), Sh. 3,000 (picha), Sh. 4,500 (fulana ya njano na nembo nne).
Mama Amosi anasema yeye ni mwathirika wa ukimwi anayetumia dawa anazopata kutoka Hospitali ya wilaya Nzega na kwamba amekimbiwa na mumewe. Anasema katika hali hiyo, ni vigumu kumhudumia Amosi.
“Ninajibanabana kupata angalau chakula lakini mengine siwezi. Nahofia Amosi atakosa shule maana mimi ni masikini sasa. Unajua hawa wawekezaji wametufilisi kimaisha,” anasema kwa huzuni.
Kama walivyo watoto wengi wa Mkwajuni, Amosi naye hulazimika kufanya kazi ya kuchekecha mawe yanayopatikana kwenye mgodi ambayo wenyeji wanapata kwa kuvizia kwa ajili ya kutafuta dhahabu.
Nimebaini hisia za woga miongoni mwa viongozi wa ngazi ya vitongoji na vijiji kuzunguka mgodi. Wengi wanaogopa kusema wanachokijua.
Mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe aliniambia kuwa usalama wao uko hatarini kutokana na shughuli za mgodi - milipuko ya miamba na mavumbi yatokanayo na kazi hiyo vinaathiri afya zao.
“Unajua ni kama tumekufa hapa. Akija mtaalamu kuchunguza afya zetu, labda sote hatupo salama. Kila siku tunaumwa vifua na kukohoa ovyo. Tunaishi kwa hewa chafu hapa Mkwajuni na vitongoji vya wenzetu karibu na mgodi. Lakini nani anajali, sisi ni mafukara mwanangu,” anasema kiongozi mmoja.
Iwapo Mwaluzwilo wanalalamika, Isanga wanalalia shida; Mkwajuni wanahofia afya zao na ndio majirani wa mgodi wa Lusu unaozalisha dhahabu mbele ya macho ya wenyeji.