Mgogoro wazinyemelea Zambia, Malawi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 12 October 2011

Printer-friendly version

MGOGORO wa kidiplomasia umeanza kuzinyemelea nchi jirani za Zambia na Malawi na huenda ukazivuruga hata nchi wanachama wa Comesa na Sadc.

Mgogoro huu ambao chimbuko lake ni hatua ya Malawi kumatia kwenye msukosuko mkubwa Michael Sata mwaka 2007, umepata mashiko baada ya kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF) kushinda urais wa Zambia mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kwa hiyo ushindi mnono aliopata Sata na kuapishwa kuwa rais wa Zambia unaweza kuwa umepokewa kwa shangwe na wananchi wengi wa Malawi, lakini ni mchungu kwa Rais Bingu wa Mutharika.

Rais Sata amekataa mwaliko aliopewa na Rais Bingu Wa Mutharika kwenda kuhudhuria mkutano wa mwaka wa Comesa uliopangwa kufanyika Malawi wiki hii.

Rasi Sata ameeleza bayana kuwa hataweza kuhudhuria mkutano huo wiki hii kwa sababu alitangazwa kuwa ni mtu asiyehitajika Malawi (persona non grata – PNG – au prohibited immigrant – PI) baada ya kukamatwa na kufukuzwa na serikali mwaka 2007.

Akizungumza baada ya kukutana na ujumbe uliotumwa na Rais Bingu Wa Mutharika kumwalika kwa ajili ya mkutano huo, Rais Sata alisema atakwenda Malawi ikiwa suala hilo litakuwa limetatuliwa. Kwa wakati huu, alisema bado anahofia kwa vile serikali ya nchi hiyo bado inamtambua kama mtu asiyeruhusiwa kuingia Malawi.

Katika mazungumzo na ujumbe huo kwenye ikulu ya Zambia, Rais Sata alisema alidhani kiongozi wa ujumbe huo alikuwa amewasilisha barua ya kuondoa marufuku aliyowekewa kuingia Malawi.

“Nadhani unafahamu mtanziko nilionao kwa serikali yako,” Rais Sata alimwambia Balozi wa Malawi nchini Zambia, David Bandawe baada ya kuwasilisha barua ya mwaliko kuhudhuria mkutano wa mwaka wa Comesa.

“Nilikwenda Malawi kukutana na kiongozi wa upinzani lakini serikali yako ilinikamata ikanitia kwenye (Toyota) Land Cruiser na ikanitangazia marufuku ya kutoingia tena Malawi. Serikali yako haijaonesha ujasiri wowote wa kuomba radhi na kwa kweli najisikia vigumu kuingia Malawi.”

Badala yake, Rais Sata amemteua Makamu wa Rais, Guy Scott kuongoza ujumbe wa Zambia kwenye mkutano huo wa Comesa.

Sata alikamatwa katika Uwanja wa kimataifa wa Chileka jijini Blantyre 15 Machi 2007, alipokwenda Malawi kufanya mazungumzo na Rais wa zamani wa Malawi, Bakili Muluzi.

“Hakuna sababu zozote zilizotolewa kwa kukamatwa kwake kwa saa kadhaa kwenye kituo cha polisi ya Blantyre ambako alipigwa marufuku kuingia Malawi,” alisema mwanasheria Ralph Kasambara.

Kisha alipakiwa kwenye gari akatolewa chini ya ulinzi hadi kwenye kituo cha mpaka wa Malawi na Zambia cha Mwami umbali wa kilomita 500 kutoka Blantyre.

Mwanasiasa huyo machachari ambaye nchini Zambia anafahamika kama ‘King Cobra’ aliishtaki serikali ya Malawi kwa kumdhalilisha na kuchafua hadhi yake.

“Alifungua kesi ya udhalilishaji na kumweka ndani kimakosa,” alisema Kasambara ambaye alikuwa wakili wa Sata. Akaongeza, “Kesi imemalizika ila tunasubiri hukumu isomwe bna Jaji Healey Potani.”

Kwa mujibu wa sheria, Rais Sata bado haruhusiwi kabisa kuingia Malawi mpaka pale Ofisa mkuu wa Idara ya Uhamiaji Elvis Thodi atakapofuta marufuku hiyo.

Bingu wa Mutharika mwenyewe ameonja uchungu wa hali isiyoeleweka ya uhusiano kati ya nchi mbili hizo.

Pamoja na kutoa pongezi kwa Sata kuwa rais mpya wa Zambia na hata kuwataka Wamalawi washirikiane na wenzao wa Zambia kufurahia ushindi huo, Rais Bingu wa Mutharika alionja ‘joto ya jiwe’ alipokwenda haraka kwenye sherehe za kuapishwa Rais Sata.

Alipanda ndege kwenda Zambia kwenda Lusaka, lakini hakuonekana kwenye sherehe. Haijulikani kama alipewa mwaliko na maofisa walio chini ya Sata kwa vile safari hiyo ilipangwa hata kabla ya King Cobra kutangazwa mshindi. Jambo la dhahiri ni kuwa Bingu wa Mutharika hakuonekana kwenye meza kuu ya wageni waalikwa.

Serikali ya Malawi kwa upande wake imesema haioni sababu za kuomba radhi kwa Rais Sata kutokana na kadhia iliyotokea mwaka 2007.

Msemaji wa serikali ya Malawi, Patricia Kaliati alisema Sata akiwa Rais wa Zambia "anakaribishwa sana nchini Malawi" hivyo hakuna sababu kwa serikali ya Malawi kuomba radhi.

Bi Kaliati alisisitiza kwamba chochote kilichomtokea Sata mwaka 2007 kilimtokea yeye binafsi na siyo kama Rais wa Zambia. "Hatujabadili msimamo wetu. Sata yuko huru kuja Malawi," alisema Kaliati.

Lakini msemaji wa Rais Mutharika, Hetherwick Ntaba alidai kwamba suala hilo lilikuwa halijamfikia Rais wa Malawi kwa hiyo hakukuwa na kauli yoyote kutoka kwa Rais huyo mwenye umri wa miaka 77 kwa sasa.

Tofauti na hao wote, Balozi wa zamani wa Malawi nchini Japan, Dk. John Chikago alimlaumu Rais Mutharika namna anavyoshughulikia mgogoro dhidi ya Rais Sata, akisema Rais wa Malawi anapaswa kutuma ujumbe kwenda kufafanua hadhi ya Rais mwenzake.

"Ni ukweli usiopingika kwamba Rais Sata hakutendewa vizuri mwaka 2007 na Malawi lazima itume ujumbe kwenda Zambia kujieleza kwa Rais Sata.

"Malawi ilipaswa kutuma taarifa kwa Balozi wa Malawi nchini Zambia kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje,” alisema Dk. Chikago.

"Hili ni suala ambalo linaweza kutatuliwa kwa urahisi kabisa. Rais Sata ana haki ya kuomba ufafanuzi. Anataka kujua nini kitatokea ikiwa hatakuwa Rais wa Zambia."
Tayari Wazambia walioanza kuona kukua kwa mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo jirani wametoa wito kwa Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika – Sadc – kuingilia haraka kusuluhisha.

"Tutaomba Sadc kuteua mtu asiyeegemea upande wowote kama (rais mstaafu wa Zambia, Kenneth) Kaunda kuwakutanisha viongozi wawili hao wakuu wa nchi ili mgogoro huo usikue na kuwa kikwazo,” alisema Lee Habasonda, mkuu wa asasi inajihusisha na utatuzi wa migogoro kusini mwa Afrika iitwayo Southern African Centre for Constructive Resolution of Disputes (SACCORD).

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)