Miaka 13 ya mchezo mchafu wa Blatter


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 27 July 2011

Printer-friendly version
Sepp Blatter

MOHAMED bin Hammam ameanguka! Je, ni kweli alitoa rushwa ili Qatar ichaguliwe kuandaa fainali za Kombe la Dunia 2022 au kwa kuwa alipambana na Sepp Blatter katika uchaguzi mkuu?

Ili kujua kilichomponza bin Hammam, nimechanganua matukio kadhaa ya ubabe wa Blatter tangu mwaka 1998.

Mwaka huo ulifanyika uchaguzi mkuu wa Rais wa FIFA, Blatter akachuana na aliyekuwa Rais wa UEFA, Lennart Johansson.

Mwaka 1999, mwandishi wa habari za uchambuzi, David Yallop alitoa kitabu kiitwacho How They Stole The Game kilichofichua uozo ndani ya FIFA.

Yallop alipoanza kusambaza kitabu hicho katika nchi za Ulaya, Blatter alikimbilia mahakama ya Ujerumani na kuomba itoe amri ya kuzuia usambazaji katika nchi za Ujerumani na Uswisi.

Baada ya kufungua kesi hiyo ya kumziba mdomo Yallop, Blatter alieleza ndani ya FIFA.com, “Haikuwa nia yangu kuziba mdomo wala kuzuia uhuru wa habari.”

Mwaka 2000, Rais wa Shirikisho la Oceania (OFC), Charlie Dempsey, katika mazingira ya kutatanisha alijitoa kupiga kura katika raundi ya tatu na ya mwisho kuteua nchi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2006.

Alipohojiwa na gazeti la The Weekend Herald, Dempsey alisema, “Niliwekewa barua chini ya mlango wangu iliyoniambia nitapewa zawadi ikiwa nisingeipigia kura nchi fulani.” Kinyang’anyiro kilikuwa kati ya Ujerumani iliyoshinda Afrika Kusini.

Mwenyekiti wa kamati ya Afrika Kusini, Irvin Khoza kwa masikitiko makubwa alisema, “Sielewi inakuwaje mtu anaweza kupiga kura raundi mbili lakini ya tatu ambayo ni muhimu anatoroka. FIFA ichunguze hili.” Kwa tafsiri ya kauli ya Khoza, Dempsey alihongwa, lakini FIFA haikuchunguza.

Mwandishi wa habari za uchunguzi Andrew Jennings, anasema, “Hakuna shaka yoyote kwamba (Dempsey) alitoka nje, kwa sababu kwa mtazamo wangu alilipwa fedha na Ujerumani kwa vile alikuwa mpigakura muhimu.” Ujerumani ilishinda kura.

Mwaka 2002, Makamu wa Rais wa CAF, Farah Addo alimtuhumu Sepp Blatter kutumia vibaya fedha aweze kushinda uchaguzi mwaka huo.

Addo aliliambia gazeti la Daily Mail, kwamba alipewa dola za Kimarekani 100,000 ili ampigie kura Blatter mwaka 1998 na kwamba anafahamu wajumbe 18 wa CAF walihongwa pia wampigie kura Blatter.

Kilichotokea ni Blatter kwenda kumshitaki Addo katika mahakama ya wilaya ya Meilen kwao Uswisi na akataka alipwe fidia Faranga za Uswisi 14,948 kwa kumchafulia jina.

Mwaka huo, aliyekuwa katibu mkuu wa FIFA, Michel Zen-Ruffinen alitoa waraka ukimtuhusumu Blatter kwa matumizi mabaya ya fedha.

Madai ya Zen-Ruffinen yaliyosisimua sana ni kwamba Blatter alitoa takrima kwa Rais wa CONCACAF, Jack Warner. Wajumbe 11 wa Kamati Tendaji ya FIFA pia walimshtaki Blatter.

Baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu akalipiza kisasi kwa kumtaka Michel Zen-Ruffinen kujiuzulu. Baada ya kuona hivyo, pia wale wajumbe 11 wakafuta kesi yao kortini, wakamalizana nje ya mahakama.

Mwaka 2010, gazeti la Sunday Times lilifumua uozo mwingine kwamba mjumbe wa FIFA, Amos Adamu wa Nigeria aliuza kura yake kwa pauni za Uingereza 500,000. FIFA ikamfungia Adamu kujishughulisha na soka miaka mitatu na kulipa Faranga za Uswisi 10,000.

Gazeti hilo likambamba Rais wa OFC, Reynald Temarii akiuza kura yake kwa pauni 1.5 milioni. Temarii alifungiwa mwaka mmoja na kulipa faranga 5,000.

Vilevile mwaka huo, Mwenyekiti wa zamani wa FA, Lord Triesman akawatuhumu kwa hongo Jack Warner, pamoja na Rais wa CAF, Issa Hayatou na wajumbe wa FIFA, Jacques Anouma, Nicolas Leoz, Ricardo Teixeira na Worawi Makudi. Warner amejiuzulu.

Baada ya kushinikiza Farah Addo aondoke FIFA kwa ‘kumzushia’ bosi wake, Blatter akampandisha Chuck Blazer kuwa mjumbe wa Kamati Tendaji ya FIFA na akawaingiza Warner na Hammam kwenye kamati ya maadili.

Blazer ndiye amedai bin Hammam na Warner walilipa dola 40,000 kwa wajumbe wa CONCACAF.

Warner hakutaka kufa peke yake, akamtuhumu katibu mkuu wa FIFA, Jérôme Valcke kwamba alikutana pia na kamati ya maombi ya Qatar. Valcke hakuadhibiwa.

Katika mahojiano na shirika la Sky Sports News Jumatatu iliyopita, bin Hammam alikiri kwamba utoaji wa zawadi ni jambo la kawaida katika FIFA.

“Hii ni kawaida, kawaida, jambo la kawaida,” alisema bin Hammam, huku akionyesha saa yake ya mkononi. “Saa hii ni zawadi niliyopewa kutoka kwa mtu fulani. Ni ishara ya upendo. Nilipopokea sikutoa chochote.”

Mlolongo huo wote unaonyesha matatizo makubwa ya rushwa yalianza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1998 uliofanyika Ufaransa. Watu wote waliokiri au kufichua habari za kuhongwa na mawakala wa Blatter walitupiwa virago.

Matukio hayo yote yanawafanya washindani wake na hata watazamaji wamwone Blatter kuwa analiongoza shirikisho hilo kwa mkono wa chuma. Blatter ni dikteta.

Bin Hammam amefungiwa kwa madai ya kutoa rushwa ili kuhakikisha nchi yake ya Qatar inateuliwa kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022.

Vizuri. Wako wapi waliohongwa? Kwanini kosa liwe kutoa rushwa lakini waliopokea na wakachagua kwa shinikizo la rushwa hawachukuliwi adhabu?

Hii ndiyo sababu Shirika la Transparency International limeitaka FIFA kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tuhuma hizo pamoja na wajumbe watatu wa FIFA waliokuwepo Trinidad ambako bin Hammam inadaiwa alijaribu kuwahonga wajumbe kutoka Caribbean.

Wajumbe wa FIFA, Worawi Makudi, Vernon Manilal Fernando na Hany Abou Rida waliongozana na bin Hammam nchini Trinidad. FIFA iko kimya.

0789 383 979
0
No votes yet