Miaka 4 ya utawala: Lipi la kujivunia?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 December 2009

Printer-friendly version
Gumzo
Rais Jakaya Mrisho Kikwete

UTAWALA wa awamu ya nne umetimiza miaka minne madarakani; ambayo ni sawa na asilimia 80 ya muda wa miaka mitano ya kipindi cha kwanza cha utawala wa Jakaya Mrisho Kikwete.

Hiki ni kipindi cha kutosha kwa yeyote kupima utendaji wa serikali na wanaoiongoza. Mengi yamefanyika na mengi pia hayajafanyika.

Kabla na baada ya kuingia madarakani, Rais Kikwete aliwajaza wananchi matumaini makubwa kutokana na ahadi zake.

Aliahidi serikali yake itaimarisha na kusimamia utawala bora, na itatenda kazi zake bila ubaguzi. Aliahidi kujenga misingi imara ya uchumi; na kusisitiza kuwa atasitisha uuzaji wa mashirika ya umma na kuimarisha machache yaliyosalia.

Ahadi nyingine ya rais ilihusu urudishaji wa nyumba za umma mikononi mwa serikali. Kwa kauli yake alisema, “Nyumba zilizouzwa kinyume cha utaratibu zitarudi serikalini.”

Aliahidi kupambana na rushwa na ufisadi. Katika hilo, Rais Kikwete alisema hatamuonea aibu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo.

Ahadi za rais zilikoleza imani ya wananchi pale aliposema atapambana na umasiki; atawezesha wanawake na wajasiriamali wengine kujitegemea; ataanzisha benki ya wanawake itakayokuwa inatoa mikopo na kwamba ruzuku kwa wakulima halitakuwa tatizo tena.

Ahadi zilikuwa nyingi. Alihitimisha kwa ahadi babukubwa ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania.”

Lakini ukilinganisha, utabaini kuwa kilichofanyika ni sehemu ndogo sana ya kile ambacho rais aliahidi wananchi.

Je, sasa hali ikoje? Ni kweli kwamba Rais Kikwete alianza mwaka wanne vema, pale alipogomea viongozi wa chama chake kugawa pikipiki 19 mkoani Arusha, ambazo upatikanaji wake ulitiliwa shaka na wengi.

Tatizo ni kwamba pikipiki zilitiliwa mashaka lakini hakuna hatua zozote za kiutawala wala kisheria ambazo zilifuatia ili kuondoa mashaka hayo. Angalau hakuna taarifa juu ya hilo.

Lakini hadi sasa, Kikwete ameshindwa kurudisha nyumba zilizouzwa. Hata yeye mwenyewe, aliyenunua nyumba ya serikali, ameendelea kujenga upya nyumba yake na hivyo kuzika kabisa matumaini ya wananchi katika jambo hilo.

Ni matokeo ya uuzaji huo wa nyumba za umma kwa watu binafsi, ulioingiza serikali hasara kubwa baada ya wateule wapya kuishi mahotelini na nyumba za kufikia wageni kwa gharama kubwa na za serikali.

Kwa upande wa mashirika ya umma, mafanikio yaliyoahidiwa na kutarajiwa, hakika hayajaonekana katika kipindi cha miaka minne.

Tuchukue mfano wa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL). Hivi sasa liko hoi. Kabla ya serikali kuligawa kwa shirika la ndege la Afrika Kusini, ATC lilikuwa linaanza kuimarika.

ATC ilisheheni marubani wa ujuzi na wazoefu; wenye nidhamu na ari ya kutenda kazi. Lakini mara baada ya kukabidhiwa kwa mwekezaji wa Afrika Kusini, likaanza kuporomoka hatua kwa hatua.

Mpango wa kusomesha marubani wapya, au kuendeleza wale waliokuwapo, ukazikwa na mwekezaji. Matokeo yake, marubani wengi, ama waliachishwa kazi au waliacha wenyewe.

Hata karakana ya ATCL ilifungwa na ndege zake zikawa zinafanyiwa matengenezo Afrika Kusini.

Miaka minne imepita hakuna hatua nyingine madhubuti iliyochukuliwa kuokoa shirika hili. Hata Sh. 5.4 bilioni ambazo serikali ilizitoa kwa ATCL katika bajeti mbili zilizopita, zinadaiwa kuishia kununulia magari ya kifahari.

Hakuna fununu zozote juu ya hatua alizochukuliwa yule aliyeidhinisha fedha hizo. Minong’ono inasema sababu ni “swahiba wa rais.”

Lakini kuna hili pia. Serikali inaendelea kubeba wawekezaji wa kitapeli, wale walioshindwa kuendesha mashirika waliyookabidhiwa.

Mfano hai, ni Kampuni ya Reli ya India (RITES) ambayo imeingia mkataba wa kuendesha Shirika la Reli la Taifa (TRC) na kampuni ya kupakua na kupakia mizigo bandarini (TICS).

Hadi sasa miaka miwili baada ya TRC kukabidhiwa mwekezaji wa kigeni, serikali bado inaendelea kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa niaba ya mwekezaji.

Wakati hayo yakitendeka, kuna taarifa kwamba mameneja wa RITE kutoka nje ya nchi, wanalipana Sh. 30 milioni kwa mwezi kila mmoja. Inadaiwa kiongozi wao mkuu analipwa Sh. 50 milioni kwa mwezi.

Wakati haya yote yanajulikana, serikali inaendelea kushikwa na kigugumizi na kushindwa kuchukulia hatua mwekezaji aliyeshindwa wajibu wake.

Matokeo yake, wananchi wanajuliza: Uko wapi uimara na uadilifu wa serikali tuliyoelezwa kabla ya Kikwete kuingia madarakani?

Wanafikia maoni kwamba huu ni udhaifu wa Kikwete katika kutenda na kuchukua maamuzi magumu yenye maslahi kwa taifa.

Rais anajua kuwa mwekezaji huyu ameshindwa kuendesha shirika. Anajua kuwa anayejiita mwekezaji hana mtaji, hana uwezo wala hana sifa za kuongoza shirika alilokabidhiwa.

Kama wananchi wanajua hivyo, bila shaka rais anajua zaidi. Anajua kuwa RITES hawakuja nchini kuwekeza, bali kuchuma kile wasichopanda.

Anajua kuwa “mwekezaji” huyu anabebwa na baadhi ya watendaji wake serikalini kwa maslahi binafsi. Rais anajua matokeo ya kukumbatia wawekezaji wa aina hii.

Kwamba uchumi unaporomoka. Maendeleo yanadidimia. Huduma za jamii zinakwenda mrama na nchi na wananchi wanazidi kuwa masikini na ombaomba.

Rais anayajua haya kwa kuwa ana vyombo vya kumulika, kuona na kumueleza. Lakini, pamoja na kuwapo kwa vyombo vyenye macho, masikio na mikono mirefu yenye uwezo wa kunasa yeyote yule na popote alipo, miaka minne imekatika bila hatua kuchukuliwa.

Ahadi nyingine ya serikali ya Rais Kikwete ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, nayo imeshindwa kutekelezwa kwa vitendo katika miaka minne ya utawala wake.

Wananchi sasa wanasema kwamba “Msamiati wa Maisha bora kwa Watanzania” umegeuka kuwa “Maisha bora kwa kila kiongozi” wa ngazi ya juu. Gharama za maisha zimepanda kwa kiwango ambacho hakiwezi kuelezeka.

Ukitaka kupima hili angalia hali za sasa za wananchi na linganisha na miaka mitano iliyopita. Wakati huo, bei ya kilo moja ya sukari ilikuwa kati ya Sh. 400 na 500. Hivi sasa, bei ya kilo moja ya sukari ni kati ya Sh. 1,200 na 1,500.

Kwa upande wa unga wa mahindi (sembe), bei ilikuwa kati ya Sh. 200 na 250. Sasa ni kati ya Sh. 800 na 1000.

Nyama ya ng’ombe nayo imepaa kama ilivyo kwa bidhaa nyingine. Kwa sasa, bei ya kilo moja ya nyama ni kati ya Sh. 4,500 na 6,000.

Miaka mitano iliyopita ilikuwa kati ya Sh. 1,500 na 2,000. Hali ni hiyohiyo kwa bidhaa nyingine kama mchele, chumvi, mafuta ya taa na yale ya kupikia.

Tayari mitaani na katika mabaraza wananchi wameanza kuuliza, yako wapi “Maisha bora kwa kila Mtanzania?” Wanauliza inachukua muda gani maisha kuwa bora? Je, mwaka mmoja uliosalia utatosha?

Ahadi nyingine ya serikali ya Rais Kikwete ni kutekeleza maagizo ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kifisadi kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (RDC).

Bunge liliagiza serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria, baadhi ya watendaji wa serikali walioshiriki kupitisha mkataba huo.

Lakini badala ya kutekeleza maazimio ya Bunge, Kikwete ameunda kamati ya rais mstaafu Alli Hassani Mwinyi kutafuta chanzo cha wabunge kuparurana na kuisakama serikali.

Kikwete anajua kwamba kiini cha yote hayo ni misimamo ya wabunge, hawa wakitetea na hawa wakihinya mkataba wa Richmond na waliohusika nao.

Anajua kuwa ripoti ya Bunge ndiyo iliiibua udhaifu wa serikali na kufichua uzembe wa watendaji serikalini katika kusimamia mikataba.

Ripoti ya Kamati Teule ndiyo iliyoonyesha sura halisi za maswahiba wawili wa Rais Kikwete – Edward Lowassa na Rostam Aziz.

Kwamba Lowassa alikuwa akitoa amri, maelekezo na wakati mwingine kuvunja sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 alimradi umepatikana mkataba kati ya serikali na Richmond.

Haikutarajiwa kwa rais kutekeleza maazimio ya Bunge kwa njia ya kuvizia. Haikutarajiwa pia rais kutenda kama yuko mafichoni.

Ilitarajiwa kuwa rais angetekeleza maagizo ya Bunge kikamilifu, hasa kutokana na ukweli kwamba ripoti ya Kamati Teule ilikuwa na baraka zake kabla ya kuwasilishwa bungeni.

Ni hatua hiyo ya kuendelea kususua, iliyowafanya wenzake katika chama na serikali, kuanza kutilia mashaka uwezo wake wa kupambana na mambo mazito.

Ndiyo chanzo cha malalamiko, tuhuma na shutuma kwamba Kikwete amewekwa mfukoni na mafisadi.

Na hili linapata nguvu zaidi kutokana na kauli ya mteule wake, Yusuph Makamba pale alipokaripia wanasiasa, wasomi, wanaharakati, viongozi wa dini, viongozi waandamizi wa serikali na CCM, pamoja na viongozi wastaafu wa vyombo vya ulinzi na usalama, hadi kuwaita “wehu.”

Viongozi hao walitaka Kikwete afanye maamuzi magumu na atende kwa manufaa ya nchi. Kwamba akishindwa asipitishwe kugombea tena urais 2010.

Kauli za viongozi wa sasa na wastaafu zilisikika wakati wa kongamano la Kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam

Walisema Rais Kikwete ameshindwa kuchukua hatua ngumu kukabiliana na watuhumiwa wa ufisadi, jambo ambalo linahatarisha amani na utulivu; kinyume na alivyoahidi kabla ya kuingia madarakani.

Kingine ambacho serikali ya Kikwete imefumbia macho ni ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi serikalini unaodaiwa kufanywa na makampuni mbalimbali yakiwemo Meremeta, Tangold, Deep Green na Kagoda Agriculture Limited.

Bado serikali haijawa wazi kuhusu miliki ya mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira na ule wa chuma wa Mchuchuma mkoani Mbeya.

Serikali haikusema ukweli pale ilipodai kuwa mmiliki wa mgodi huo si rais mstaafu Benjamin Mkapa, kwa kile Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alichoita, “Kampuni ya ANBEN” iliuza hisa zake na hivyo ilijiondoa katika umiliki.

Ukweli ni kwamba kampuni ya ANBEN bado ni miongoni mwa wamiliki wa mgodi wa Kiwira.

Katika miaka minne ya Kikwete, serikali imeshindwa kuchunguza madai ya rushwa na ufisadi katika ununuzi wa rada na ndege ya rais. Imeshindwa kuonyesha uwazi katika mambo mengi.

Ukichukua yote hayo haraka utabaini kuwa wananchi wamepoteza, kwa kiasi kikubwa, imani yao kwa CCM, serikali na hata kwa Kikwete mwenyewe.

Kikubwa ambacho wananchi wamepoteza imani nacho ni tabia hii ya kubeza ukweli, kuporomosha matusi, kusakama na kutukana wanaozungumzia mambo ya msingi ya kitaifa.

Hata tabia ya wateule wa Kikwete kukaripia wanaosemea wanyonge na kukejeli fikra za Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kumezidisha ufa kati ya serikali na viongozi wao.

Sasa Kikwete afanye nini ili kujiokoa? Jibu liko wazi. Atende kama alivyoahidi. Achukue hatua kama alivyosema miaka mitano iliyopita.

Kikwete akubali ukweli, kwamba kuna matatizo makubwa ndani ya serikali yake; wananchi wengi hawaridhishwi na utendaji kazi wake na ule wa baadhi ya viongozi katika serikali yake.

Katika yote haya, Rais Kikwete anastahili kujiuliza, “Nitakumbukwa kwa kufanya nini?”

Kama kipo apaze sauti. Kama hakipo ajirekebishe na kuanza upya; kwa kasi kubwa au akae pembeni wengine watengeneze historia machoni mwake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: