Miaka 50: Tumekwama wapi?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 December 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

HIVI sasa taifa liko kwenye sherehe za miaka 50 ya uhuru. Ni miaka mingi mno. Ni kipindi cha kuangalia nyuma na kutafakari kwa makini wapi tulifanikiwa, wapi tuliteleza na wapi tulianguka.

Kujiuliza huko lazima kusaidie kuelewa vyanzo vya mafanikio, kushindwa kwake, hatua gani tunachukua kulinda mafanikio hayo kama kweli yapo na kupambana kwa akili na ujasiri na matatizo yatakayojitokeza.

Ni ukweli usipoingika kuwa, taifa hili ni moja. Lakini lenye mchanganyiko wa watu wa makabila, dini na rangi mbalimbali. Lenye lugha moja ya taifa, lakini lenyewe limeathiriwa na imani za dini mbalimbali, kulitokana na kuchangamana na mataifa ya ulaya, bara hindi na nchi za Falme za Kiarabu.

Taifa linalohubiri kutokuwa na dini, lakini lenye watu wenye uhuru wa kuabudu watakavyo.

Wakati linapata uhuru, lilikuwa na watu wengi wasio na elimu wala kujua kusoma na kuandika. Lilikuwa halina hata chuo kikuu kimoja na kwamba lilikuwa na wahandisi wanne tu.

Ni taifa ambalo liliamua kupambana na maadui watatu – ujinga, umasikini na maradhi. Lilitunga falsafa ya maendeleo ya nchi kuwa ni siasa ya ujamaa na kujitegemea na kuweka nguzo kuu za uchumi mikononi mwake.

Kwa kiasi kikubwa sera ya ujamaa ilifanikiwa kuleta maendeleo ya kijamii katika nyanja za afya, elimu ya umma, na miundo mbinu ya umeme, barabara na reli. Ilfanikiwa hata katika kuunda vijiji vya ujamaa.

Hata hivyo, makosa yalifanyika kwa kudhoofisha vyama vya wafanyakazi, kuvunja vyama vya ushirika na serikali za mitaa; makovu ya makosa hayo yako mpaka leo.

Taifa hili lililojivunia mchango uliotukuka wa kuwa kinara wa ukombozi katika bara la Afrika. Baada ya vita hiyo, uchumi wake uliyumba sana na lilinyimwa misaada ya kufufua uchumi na mashirika ya wabadilisha fedha ya kibwanyenye ya Benki ya Dunia (WB) na shirika la fedha ulimwenguni (IMF).

Ni taifa liliohimili njama za kutaka kuangushwa serikali yake na lililokuwa likilengwa na mataifa ya kibwanyenye.

Mvumo wa mabadiliko ya kisiasa ya Ulaya Mashariki ya mwaka 1989-91 ulichangia kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini na mwaka 1992 kwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

Mabadiliko hayo yalikuwa ni ya shingo upande na matokeo yake ni kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilijirimbikizia madaraka ya namna na kuyaendesha. Ndio maana tokea uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi hakujawa na uchaguzi huru na haki wa uraisi na wabunge.

Tumekuwa na genge la watu wachache wanaoamini kuwa jimbo lao ni kuchakachua uchaguzi na hata kufikia kubadilisha katiba ili wale wanaongoza tume ya uchaguzi wawe ni watu ambao wako tayari kuchakachua uchaguzi bila aibu.

Uchaguzi wa mwaka 2010 ni uchaguzi uliochakachuliwa bila aibu na serikali viongozi wake wanajua hilo vema. Pale uhalali wa kuongoza unapokuwa wa mashaka, wahusika hutumia nguvu. Ndivyo ilivyo kwa taifa hili – miaka 50 baada ya uhuru.

Kuanzia mwaka 1994 taifa letu likageuzwa dodoki kwa kufuata sera ya kugawa rasilimali zake kwa wanyonyaji na wachukuaji wa nje. Madini yakaanza kubinafusishwa kwa kupewa makampuni ya kutoka nje kama Canada, ambayo mwaka 1995 mara baada ya uchaguzi mkuu wakadai kuwa mtu wao (Benjamin Mkapa) ameingia ikulu.

Muda si mrefu, watu laki nne (400,00) wakatimuliwa kwenye mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, mkoani Shinyanga, huku zaidi ya  watu 52 wakifukiwa ndani ya migodi. Mpaka leo serikali imekataa kufanyika uchunguzi huru wa suala hilo.

Tokea hapo nchi yetu haina inachopata kutokana na madini hayo. Makampuni ya madini kutoka nje hayalipi kodi yoyote ya maana licha ya maneno ya kejeli ya viongozi wa serikali kuanzia rais na mawaziri wanaamini ni lazima “tuliwe ndio tule,” kana kwamba tuna madini yasiyokwisha.

Taifa limekuwa na donda la kutisha la rushwa. Miaka 50 baada ya uhuru hakuna hatua za makusudi na za dhati za kupambana na rushwa na ufisadi mkubwa kama ule wa Deeep Green, Kagoda, Meremeta na majengo pacha ya Benki Kuu ya Taifa (BoT).

Kuzima jitihada za vyama vya upinzani na taasisi za kiraia dhidi ya ufisadi, wanufaikaji wa ufisadi wakaanzisha kampeni za kutugawa kwa misingi ya udini, ukanda, rangi na ukabila. Bila aibu watu wao sasa wanatumia misikiti, makanisa na mitandao ya kijamii kueneza chuki katika nchi.

Kingine katika miaka 50 ya uhuru ni kushamiri kwa jitihada za kuvunja Muungano, ikiwa ni pamoja za Zanzibar kudai kuwa inaonewa katika Muungano na kuwa serikali yake lazima iwe na madaraka kamili ikiwa hata katika mambo ya Muungano.

Mabadiliko ya hivi karibuni ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yako wazi na kwayo Muungano wetu uko katika chumba cha uangalizi maalumu hospitalini (ICU).

Kama taifa tuna jukumu kubwa la kuchagua na ni lazima tupambane na matatizo yanayolikumba taifa letu ikiwa ni rushwa, utengano wa kidini na ukabila, ufisadi na kuporwa kwa rasimali za umma.

Ni lazima kizazi cha sasa kikatae kuendelea kuwa taifa masikini, wakati kuna rasilimali za kutosha. Ni lazima tupambane kwa ujasiri mkubwa na ufisadi na kuwajibisha wote wanaoshiriki katika vitendo hivyo vichafu.

Ni lazima tujenge taifa la demokrasia ya kweli, lenye katiba inayotoa mgawanyo sahihi wa madaraka wa mihimili ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali. Ni lazima vyombo hivi viwajibike kwa umma. Lazima tuwe mfumo wa uchaguzi huru na wa haki na katu tusikubali kuwa na uchaguzi wa kuchakachuliwa.

Taifa lijenge mfumo madhubuti wa uchumi ikiwa ni pamoja na kujenga misingi inayounganisha mikoa, wilaya, tarafa na kata zitakazochagiza kukua kwa shughuli za maendeleo.

Misingi mbinu hiyo lazima iunganishe na nchi jirani. Ni lazima tuwe na reli nyingi na barabara kubwa na nzuri. Tuache utamaduni wa kujenga barabara za njia mbili. Barabara zote kuu lazima ziwe za njia nne, sita na kuendelea.

Miaka 50 ijayo tuanze leo kuwekeza katika kutafuta elimu bora. Elimu inayomuwezesha mtoto wa Kitanzania kuelewa mazingira yake, nchi yake na namna ya kuweza kujiendeleza na kutumia vipaji vyake kwa maendeleo yake na taifa. Ni lazima ijenge uzalendo na upendo kwa taifa letu.

Tunatakiwa kuwa na huduma bora za afya kila kona ya nchi. Hospitali zetu lazima ziwe na vifaa vya kutosha na vya kisasa. Tuwe na madaktari mabingwa na mahiri kila kona ya Jamhuri na lazima tuwekeze kwa nguvu zote katika kuwasomesha watoto wetu.

Ili kuyafanya hayo ni lazima tuwe na uchumi unaokua na serikali inayokusanya kodi na kuadhibu bila huruma ukwepaji wa kukusanya kodi. Kila raia anayefanya kazi katika sekta ya umma na binafsi, lazima alipe kodi. Kulipa kodi kusionewe aibu.

Hata rais lazima alipe kodi. Msamaha wa rais kutolipa kodi ni dhana potofu inayomuona rais kama mfalme. Zawadi ambayo Rais Jakaya Kikwete anayoweza kuwapa Watanzania leo, ni kubadilisha Sheria ya Kodi ya Mwaka 2004 ili naye alipe kodi.

Tuna mengi ya kufanya na tunapoanza safari ya kuelekea miaka 75 ya uhuru ni lazima tuweke ahadi ya dhati ya kupambana na maadui wanne wa nchi yetu ujinga, maradhi, umasikini na ufisadi.  Inawezekana timiza wajibu wako.

0
No votes yet