Miaka 50 walimu wengi hawana viwango


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 21 December 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MATOKEO ya ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa kati ya Julai na Septemba mwaka huu ili kupima utendaji kazi wa shule za msingi na uwezo wa walimu katika Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, yameonesha walimu wengi hawana viwango.

Shule za Huruma na Kipika, ndizo ambazo walimu wake wote waliokaguliwa wamepata wastani juu ya 50. Shule nyingine zenye walimu bora ni Kiwanjani, lakini imeshushwa katika wastani kutokana na walimu wanne kuwa chini ya 50 na watatu chini ya 10.

Vilevile, shule nyingine za Nazareth, Mbinga, Nyerere, Kiyaha na Masumini zina walimu wengi bora japokuwa miongoni mwao wamepata chini ya asilimia 50.

Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga italazimika kufanya kazi ya ziada kwa shule za msingi za Mabuni, Nakatoke, Litumbandyosi, Kilosa, Kilindi, Mnazi Mmoja, Kiyaka, Mikolola, Mbangamao, Lihutu, Kagugu, Luhikitiki zenye walimu ambao uwezo wao unatia shaka.

Walimu wote walipimwa katika vigezo vitatu: kuandaa somo, kutoa mazoezi na utendaji kazi.

Wale walioshindwa maana yake wanafundisha kwa mazoea na ubabaishaji.

Ukaguzi huo uliojumuisha pia walimu wakuu wa shule, unaonesha walimu 151 ndio walipata wastani juu ya 50 wakati 213 wamepata wastani chini ya 50. Walimu wengi wamefeli kigezo cha maandalio na utendaji kazi.

Aliyeshika nafasi ya mwisho anatoka shule ya msingi ya Mabuni na alipata asilimia zero katika maandalio, asilimia 23 katika mazoezi na asilimia zero katika utendaji kazi.

Katika ukaguzi huo, Mwalimu Analis Mapunda anayefundisha shule ya msingi Kipika iliyoko kata ya Mbinga Mjini, amejitokeza kuwa mwalimu bora baada ya kupata wastani wa asilimia 144 katika maandalizi ya masomo, asilimia 113 katika mazoezi na asilimia 129 utendaji kazi.

Aliyeshika nafasi ya pili ni Florensia Mlekwa wa shule ya msingi ya Huruma iliyoko kata ya Mbinga Mjini akifuatiwa na Simon Ndunguru wa shule hiyohiyo ya Huruma.

Wengine walioko kwenye orodha ya 20 bora na majina ya shule zao kwenye mabano ni George Kapinga (Kiyaha), Bibiana Ngongi (Huruma), Elizabeth Komba (Mateka), Deo Hyera (Huruma), Agatha Francis (Kipika), Norberta Mapunda (Kiwanjani), Sr. Lukresia Nombo (Huruma).

Wengine ni Venancia Hyera (Nazareth), Eva Kapinga (Huruma), Alena Ndunguru (Mbambi), Yordan Ndunguru (Masumuni), Hilda Maendaenda (Masumuni), Oresta Komba (Kipika), Ritha Kumburu (Halale),  Helmina Nindi (Mnazi Mmoja), Violet Malugu (Mbinga) na Ndigwako Gwakisa (Nyerere).

Lengo la Wilaya ya Mbinga ni kutekeleza kaulimbiu isemayo “kila mwanafunzi anahitaji mwalimu bora.” Kwa hiyo, moja ya vigezo vya kupima maendeleo ya elimu, hasa shule za msingi ili kujua stadi za mwanafunzi za kusoma, kuandika na kuhesabu, uwezo wa mwalimu ni muhimu kuzingatiwa.

Japokuwa mwalimu bora ametoka Kipika, wastani kwa shule nzima, Huruma ndiyo imekuwa kinara ikifuatiwa na Kipika. Huruma imepata wastani wa 70 (maandalio), asilimia 96 (mazoezi) na asilimia 83 (utendaji kazi), na Kipika ina asilimia 84 (maandalio), 70 (mazoezi), 77 (utendaji kazi).

Shule zinazofuata kwa ubora ni Mateka, Mbinga, Maganagana, Nyerere, Nazareth, Masumuni, Halale, Tugutu, Lazi, Kigonsera, Kiyaha, Lupilisi, Kiwanjani na Mbambi.

Shule 10 zilizoshika mkia ni Mabuni iliyoshika nanga kwa maandalio 2, mazoezi 8 na utendaji kazi 5, Litumbandyosi (1-13-7), Ukimo (1-19-10), Lipilipili (3-15-12), Nakatoke (4-22-13), Kingoli (0.3-24-13), Maliba (2-25-14), Kwambe (7-22-15), Mahumbato (12-19-16 na Luhikiti (6-29-17).

Ukaguzi wa aina hii unaweza uwe utaratibu mgeni kwa Mbinga na Tanzania kwa ujumla lakini si mpya duniani.

Mathalani, Novemba 2008, Kamishna wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa jimbo la Kwara nchini Nigeria, alipata shaka juu ya uwezo wa walimu wa shule za msingi na sekondari. Akaamua kupima uwezo wao.

Alichukua mtihani wa Kiingereza na Hisabati ambao uliandaliwa kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne akawapa walimu hao. Jasho liliwatoka. Matokeo yalipotangazwa, walimu 259 kati ya 19,125 waliofanya mtihani huo walifeli.

Tangu uamuzi huo ulipofanyika, gavana wa jimbo hilo anakabiliwa na swali la kwa nini waliamua kuwaingiza tena walimu kwenye chumba cha mtihani?

Jibu analotoa ni “kuondoa uozo.” Ndiyo, uamuzi mwingine mbaya ukafuata; waliokuwa kwenye orodha ya walimu walioteuliwa kusahihisha mitihani walifutwa na wakatakiwa kufanya upya mitihani mwaka uliofuata kuboresha uwezo wao vinginevyo wangefutwa kazi.

Kwa wilaya ya Mbinga shule 54 zilizokaguliwa sawa na asilimia 16 ya 321 zilizopo na walimu 364 waliofanyiwa tathmini sawa na asilimia 18 tu ya walimu 2021 ni sampuli tu. Hata hivyo, dawa ya walimu waliofeli iko jikoni.

“Tumebaini kwamba walimu hawaandai maazimio ya kazi, hawaandai somo na pia hawatoi mazoezi kwa wanafunzi hivyo kufanya hali kwa sasa shuleni kuwa mbaya,” anaeleza Afisa Elimu Wilaya ya Mbinga, David Mathias Mkali.

Katika mikakati ya kuinua elimu, Mkali anasema walimu wakuu zaidi ya 50 watashushwa vyeo au kuhamishwa.

Uzembe kiutendaji ndio umesababisha shule ya msingi Ndingine iliyoko kata ya Liwundi wanafunzi kusomea chini ya mbuyu kwa miaka mingi, jengo mojawapo katika shule ya msingi Mkili kugeuzwa mahabusu au walimu wa shule za msingi kata ya Liwundi kuishi kwenye nyumba za nyasi.

Ukaguzi huu utasaidia kujua walimu wenye mapenzi na kazi. Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Lumecha, Agustino Kinyengo Mapunda anakiri kuwa katika shule yake, ufaulu umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka kutokana na baadhi ya walimu kutowajibika ipasavyo kufundisha vipindi vyao.

Mwaka 2010 wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 24 lakini ni wanafunzi tisa tu ndio waliofaulu. Wanafunzi walihohitimu mwaka huu ni 40 ambapo kati yao wanafunzi watano wamemaliza wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Mratibu elimu kata ya Kingerikiti, Martha Christian Lipa anasema tatizo kubwa linalochangia wanafunzi hasa wa kata yake kumaliza elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma na kuandika ni walimu kukosa upendo kutokana na kutojitoa na kuwa na moyo wa kujituma kuwafundisha.

“Walimu wengi wanaifanya kazi ya ualimu kwa sababu ya kupata mshahara na si kumkwamua mwanafunzi na hiyo ni roho mbaya na walimu wa namna hii hawatakiwi,” anasema Lipa.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet