Miaka 50 ya Uhuru, hatuna kubwa la kujivunia


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version

DESEMBA 9, 1961 timu ya soka ya taifa ya Tanganyika iliwapa burudani maelfu ya mashabiki wa soka kwenye Uwanja wa Taifa (sasa uwanja wa Uhuru) ilipoitandika Malawi (zamani Nyasaland) mabao 1-0 katika mchezo wa kirafiki.

Mchezo huo ulioandaliwa siku ya Tanganyika kupata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza, mpaka leo umebaki kwenye kumbukumbu kwani haujapatikana tena si dhidi ya Malawi tena wala timu nyingine yoyote katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Kabla ya uhuru, michezo na utamaduni vilitumika kuwaunganisha Watanganyika katika harakati za kudai haki yao na uhuru wa kujitawala na baada ya uhuru ilitoa burudani, ajira na kuimarisha umoja na mshikamano.

Mchezo wa bao, ngoma za kienyeji, mpira wa miguu, riadha na ngumi ni miongoni mwa michezo iliyotumika kuleta umoja wakati huo. Waziri mkuu na baadaye Rais wa kwanza wa Tanganyika huru, Mwalimu Julius Nyerere naye alishiriki kikamilifu kama mwamuzi na mcheza bao na aliunda wizara iliyoshughulikia michezo na utamaduni.

Baada ya kupata uhuru Tanganyika ilijitahidi kushiriki kikamilifu katika michezo yote na hadi miaka ya 1980 ilitamba zaidi katika riadha na ngumi za ridhaa duniani. Mashirika ya umma yalisaidia michezo na ulionufaika zaidi ulikuwa mchezo wa netiboli. Katika soka klabu za Simba na Yanga zilitamba.

Kuanzia 1961 hadi 1964, Tanganyika haikufanya vizuri katika michezo nje ya nchi japokuwa shule zilitumika kuzalisha wanamichezo mbalimbali hadi nchi hiyo ilipoungana na Zanzibar 26 Aprili, 1964 na kuzaa Tanzania.

Mwaka 1969, klabu ya soka ya Yanga iliyoanzishwa 1935 iliweza kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika. Yawezekana hayo ndiyo mafanikio makubwa ya soka iliyopata Tanzania kwenye ukanda wa Afrika katika miaka ya 1960 kwa ngazi ya klabu.

Tanzania iling’ara zaidi katika michezo hasa riadha miaka ya 1970, baada ya Filbert Bayi kutwaa medali ya dhahabu mwaka 1973 katika mbio za mita 1500 za michezo ya Afrika ‘All Africa Games’ huko Lagos, Nigeria na 1978 huko Algiers, Algeria. Bayi pia aliitoa kimasomaso Tanzania mwaka 1974 baada ya kutwaa medali ya dhahabu kwenye michezo ya Jumuia ya Madola katika mbio hizo za mita 1500.

Baadaye 1980 Bayi  alitwaa medali ya fedha katika michezo ya Olimpiki kwenye mbio za mita 3000 huko Moscow, Urusi.  Baada ya Bayi kuanza kufanya hivyo, mwanariadha mwingine Suleiman Nyambui naye alitwaa medali ya shaba katika michezo ya Afrika mwaka 1978 kwenye mbio za mita 5000.

Nyambui pia alitwaa medali ya fedha katika Olimpiki huko Moscow kwenye mbio za mita 5000. Wanariadha wa kike waliowahi kutamba ni Mwinga Mwanjala.

Baadaye 1982, Juma Ikangaa naye akatwaa medali ya fedha katika mbio za marathoni kwenye Jumuia ya Madola huko Brisbane, Australia.

Katika soka, Tanzania ilifikia mafanikio makubwa zaidi mwaka 1980 baada ya kufanikiwa kucheza Kombe la Mataifa Huru ya Afrika 1980 (wakati huo), huko jijini Lagos, Nigeria na kuishia raundi ya kwanza.

Kidogo Simba ilifanikiwa kufika fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993 na kukosa ubingwa dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast mbele ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

Kabla na baada ya hapo, klabu za Tanzania zimekuwa zikiishia hatu ya robo fainali ya michuano mbalimbali inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Leo hii Tanzania inafanya vizuri angalau katika michuano inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuanzia ngazi ya klabu na taifa.

Timu za jeshi za Ngome na magereza Kiwira zilitamba katika mchezo wa mikono Afrika Mashariki na Afrika. Medali ya mwisho ya dhahabu katika ngumi alirudi nayo Michael Yombayomba katika michezo ya Jumuiya ya Madola, Kuala Lumpur, Malaysia.

Halafu michezo ikapata pigo. Waziri wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai akapiga marufuku mashindano shuleni ya Umishumta na Umiseta ambayo ilikuwa ikisaidia kuzalisha nyota mbalimbali wa soka, riadha, netiboli na michezo mingine. Ilirejeshwa tena mwaka 2006 japo haina mvuto wala nguvu kama ilivyokuwa zamani.

Mwaka jana timu ya taifa ya netiboli ilifanikiwa kucheza Kombe la Dunia na safari hii imeshika nafasi ya tatu katika Michezo ya Mataifa ya Afrika, Maputo, Msumbiji.

Mbali ya mafanikio hayo machache niliyotaja hapo juu, ndani ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika au Tanzania Bara haina jambo lingine kubwa la kujivunia kupitia michezo zaidi ya Uwanja wa Taifa (mpya) wenye uwezo wa kuchukua watazamaji zaidi ya 60,000.

Uwepo wa uwanja huo, ulichochea kwa kiasi kikubwa ujio wa timu za taifa za News Zealand, Ivory Coast na Brazil iliyocheza mechi ya kirafiki na Taifa Stars 7 Juni mwaka jana.

Bado serikali na wadau wengine wa michezo nchini, tuna kazi kubwa ya kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika kukuza maendeleo ya michezo na kuifanya nchi hii iwe tishio kote duniani.

0713801699
0
No votes yet