Mjadala wa uraia wa Kabila washika kasi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Rais Joseph Kabila

MwanaHALISI Toleo Na. 247 (Juni 22- 28, 2011) katika ukurasa wa Gumzo la Wiki, kuna makala inayozungumzia Joseph Kabila: Mnyarwanda anayetawala Kongo?

Inawezekana kabisa kuwa kuna ukweli kuhusu Unyarwanda wa Rais Kabila.  Lakini inatia shaka kuona maudhui hasi ya makala ikiwa na nia ya kupandikiza chuki dhidi ya jamii ya Kitusi katika ukanda wa maziwa makuu.

Makala inapotosha ukweli halisi wa masuala yaliyojadiliwa kwa makusudi na kwa malengo mahsusi. Nayajadili mambo yaliyopotoshwa.

Kwanza, dunia nzima inayatambua majina ya rais wa sasa wa Kongo kama Joseph Kabila Kabange.  Mwandishi maalum wa makala anaeleza kuwa ubini wa baba wa kibiologia wa Rais Kabila ni Kanambe. Mbona mwandishi asisumbuke kueleza jina Kanambe lilitokea wapi?

Pili, makala inaeleza kinagaubaga jinsi marehemu Rais Laurent Kabila alivyoasili  (adopt) watoto  wa Kanambe (akiwamo Joseph na dada yake) na kujitwalia mama yao kama mke baada ya mumewe, Kanambe kuuliwa.

Hivi Mwandishi Maalumu hajui kuwa 'adoptees' wanapata haki sawa na watoto wa kibiologia wa 'adoptor’ ikiwemo haki ya uraia?

Katika swala hili la uraia wa Joseph Kabila; ulitokana na adoption ya hiari ya Laurent Kabila. Kumbambakiza Rais Kagame wa Rwanda ni uonevu wenye lengo ovu (demonisation).

Tatu, historia imeandikwa wazi kuwa watu wa  jamii ya Wanyamulenge waliishi eneo la Mashariki mwa Kongo kabla ya ujio wa mipaka iliyokatwa na wakoloni (Partitioning of Africa) baada ya mkutano wa Berlin  (Berlin Conference) mwaka 1884. 

Siyo kweli na ni upotoshaji wa historia kudai kuwa Wanyamlenge ni wakimbizi wa kisiasa wa Rwanda wa mwaka1958.

Nne, mwandishi amedai kuwa Chama cha UNAR kiliundwa huko Kongo na wakimbizi wa Kitusi.  Ukweli ni kuwa chama hiki, Rwanda National Union kiliundwa huko Rwanda, kikiwa chama cha kwanza cha kizalendo kilichoongoza mapambano ya kudai uhuru.

Uchaguzi mkuu wa uhuru ulighushiwa na wakoloni wa Kibeljiji kukipendelea chama cha PARMEHUTU cha (Gregoire) Kayibanda.

Tano, mwandishi amedai kuwa Yoweri Mseveni na Paul Kagame walikuwa na mkataba wa kijeshi sawa na ule wa CNL na UNAR.

Kweli ni kuwa akina Paul Kagame na kundi kubwa la wakimbizi wanzake walinyimwa haki ya uraia wa nchi yao ya asilia.

Ilikuwa haki yao ya msingi kupigania kurejesha haki hiyo bila kujali mazingira mengine yoyote.  Na mtetezi wa haki yeyote, popote alikuwa na uhalali wa kuunga mkono mapambano hayo.

Katika ukanda wetu wa Maziwa Makuu, yamekuwa yakiibuka madai ya kuhoji uraia wa viongozi wakuu wa nchi zetu. Mifano ni mingi.

Mwalimu Nyerere aliitwa Mrundi na Watanzania wenye itikadi ya kikaburu. Rais Mkapa aliitwa Mmakonde wa Msumbiji. Rais Kaunda aliitwa Mmalawi; mrithi wake Chiluba aliitwa Mzaire.  Rais Museveni aliitwa Mnyarwanda; Rais Abeid Karume, Mmalawi n.k.

Hata kama madai haya yana ukweli ndani yake, historia ya Waafrika kabla ya ujio wa wakoloni imesheheni majibu maridhawa.  Vilevile utumishi wa kizalendo wa kiongozi kwa nchi yake ndio kipimo halisi cha uraia wake.

Naamini kuwa mwishoni wa ngwe ya uongozi wa Rais Kabila, atapimwa kwa mchango alioutoa kwa Kongo akilinganishwa na wazawa kina Mobutu na ndipo Unyarwanda au Ukongomani wake utadhihiri.

Mwisho, ni muono wangu kuwa maudhui ya makala haya haikuwa hasa uraia wa Rais Joseph Kabila, bali kile kijulikanacho kama 'HIMA EMPIRE' pacha wake "HUTU EXTREMISM AND GENOCIDE IDIOLOGY"

Nzichoko Gerald
S.L.P 1368 TABORA.

 

Nilikuwa na Joseph JKT

Gazeti lako Toleo Na. 247, uk. 10, 11 unazungumzia Joseph Kabila. Joseph Kabange na dada yake, Janet Kabange, nilikuwa nao JKT MAKUTUPORA mwaka 1992/1993 katika operesheni “Vyama Vingi.” Mimi na joseph tulikuwa kombania A. Dada yake Janet alikuwa kombania E, ikiongozwa na Ofisa Isisha. Wakati huo mkuu wa kambi ya makutupota alikuwa Lt. Kanali Rajab. Kasoma Ilambo Sekondari na kituo chake cha mitihani kilikuwa Sangu.

0753 428689

 

Alisomea Mbeya, si Uganda

Makala yenu kkuhusu “Utata wa uraia wa Joseph Kabila” ina utata hasa kwetu tuishio Mbeya au waliowahi kuishi Mbeya. Tunajua elimu ya sekondari kasoma Mbeya na si Uganda.

Joji
0754 762459

 

JKT kwa wasio raia?
Nimewahi kusikia Joseph kabila alikuwa JKT katika moja ya kambi hapa nchini. Je, alikuwa huko kama nani? Alikuwa anaandaliwa kwa vita nchini mwao au alikuwa amepata uraia wa Tanzania? (Tafadhali usionyeshe simu yangu).

0
No votes yet