Mkukuta unaufanya umaskini uwe sugu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version

DUNIANI kote umaskini unaongezeka kwa kasi sana licha kuongozeka utajiri na matajiri. Umoja wa Mataifa (UN) unakadiria kuwa watu zaidi ya bilioni 1.5 ni maskini, hohehahe wasio na uwezo wa kumudu mahitaji yao muhimu ya kila siku. Katika nchi zinazoendelea kati ya asilimia 30 na 60 ya watu wake ni fukara.

Sababu kubwa ya kuongezeka umaskini ni kuendelea kuliangalia tatizo la umaskini kwa kutumia mtazamo wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wa nini kifanyike katika vita dhidi ya umaskini.

Zipo dhana aina tatu na zote zinatoka katika Benki ya Dunia, IMF na mataifa ya Magharibi. Dhana zote hizi zinaongelea ‘kupunguza’ umaskini na si kuondoa umaskini.

Maneno Kiingereza yanayotumika katika mikakati ya kuondoa umaskini ambayo yamesambazwa katika nchi zote maskini duniani kuanzia Bangladeshi, Tanzania hadi Haiti ni ‘reduction’ na ‘alleviation’ yote yana maana sawa ya kupunguza.

Kila nchi katika Afrika na kwingineko inao “Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini” ambao unafanana neno kwa neno isipokuwa tu jina la nchi. Na kosa kubwa katika vita dhidi ya umaskini linaanzia hapo.

Unapunguza umaskini kwa kiwango gani na katika nini na kwa nani?  Viashiria na vyanzo vipi vya umaskini unavyovipunguza na viashiria vipi na vyanzo vipi unaviacha?

Na unavyoviacha unavidhibiti vipi ili visiongezeke na kuongeza umaskini zaidi? Tatizo la umaskini si la kupunguza bali ni la kuondoa ‘eradicate’.

Unakwenda hospitali kutibiwa ili kuondoa malaria na si kuipunguza. Unapopunguza malaria inakuwa sugu na unawaambukiza wengine. Madhara ya kupunguza ni makubwa kwani kama ulikuwa unatumia krolokwini basi itabidi utumie fansida na ukiendelea kupunguza tu fansida nayo inakuwa haifai tena hapo utahitaji kwinini ya drip na ulazwe hospitali ili upone kabisa vinginevyo ni kifo. Gharama ya matibabu ya kupunguza ni kubwa kuliko kuondoa ugonjwa.

La kusikitisha kupunguza ndiyo lugha rasmi na silaha dhidi umaskini katika Mkukuta. Tunapima kupungua umaskini kwa kuangalia pato la taifa (GDP). Mwalimu Julius Nyerere kila mara alikuwa akisema “kupima utajiri wa nchi na maendeleo yake kwa kutumia tu kigezo cha pato la taifa ni sawa na kupima tu vitu bila kuzingatia maisha ya wananchi yameboreshwa kiasi gani na bila kuzingatia kuridhika kwao.”

Takwimu za serikali za mwaka 2007 zinaonyesha umaskini ulikuwa unaongezeka nchini na kwamba asilimia 50 ya Watanzania waliishi katika umaskini. Kwa uhalisia, hali ni mbaya sana katika Tanzania ya leo.

Historia inaonyeshwa wazi kabisa kwamba Benki ya Dunia na IMF hazikuanzishwa kuondoa umasikini. Hili si lengo lake. Na hata wanaoendesha taasisi hizi hawaujui umaskini ni nini.

Pamoja na mema machache sana yanayofanywa na taasisi hizi, kimsingi taasisi hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa umaskini duniani ikiwemo Tanzania kwa sera za zake zisizo na utu.

Wanaoendesha taasisi hizi wako Wall Street Washington na ulimwengu wote unajua fika kwa mchezo mchafu na ulaji riba kama kinavyosema kitabu ‘The Globalisation of Poverty: A New World Order (2nd Ed)’ cha Michael Chossudovsky.

Taasisi hizi ndizo zinatupangia namna ya kupunguza umaskini. Dhana ya kwanza wanayoitumia ni kwamba umaskini unatokana na kutokuwa na raslimali kama ardhi, shule, hospitali, ukosefu wa ajira na pia kutokuwa na wataalamu katika fani mbalimbali.

Benki ya Dunia inatoa suluhisho kwamba umaskini unaweza kupunguzwa iwapo shule nyingi zitajengwa na kutoa elimu; hospitali nyingi zitajengwa na kutoa huduma ya afya na wasio na ardhi wakapewa fursa ya kupata ardhi.

Lakini katika suluhisho, kinachotafutiwa ufumbuzi si kiini cha tatizo la umaskini bali ni viashiria vya umaskini. Tunatibu dalili tu baadala ya ugonjwa. Ni sawa na kumpa mtu panado kupunguza homa bila kumpa kwinini kutibu malaria inayomsumbua.

Hivyo basi tunapaswa kujiuliza kwa nini hakuna ajira, kwa nini ubora wa elimu umeshuka sana, kwa nini huduma ni za ovyo katika hospitali na ni namna gani mifumo yetu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inarekebishwa katika nchi.

Hiki ndicho kiini ambacho hakiguswi na dawa kutoka Benki ya Dunia. Ni ukweli usiofichika kwamba kama serikali inatawaliwa na mafisadi hata zikiletwa pesa kiasi gani kutoka kwa wafadhili zitaishia kwenye akaunti za watawala.

Aidha, hata zikijengwa shule na hospitali kila kijiji lakini kama majengo yake pamoja na huduma inayotolewa haina viwango bora huwezi kutoa wanafunzi bora au kutoa tiba bora. Na juu ya hayo mfadhili anapokata pesa basi hospitali nayo inazikwa.

Unaweza kutengeneza ajira nyingi tu za wachuuzi na machinga kwa kuwapa mikopo ambayo ina riba kubwa. Matokeo yake wanaishia kufanyia tumbo tu na benki. Hakuna faida. Hawawezi kujiwekea akiba kwa kuuza vitana na leso. Hivyo basi huwezi kujenga taifa au kufanya mapinduzi ya kiuchumi kwa uchuuzi.

Vijana hawa wanahitaji ajira katika sekta ya uzalishaji viwandani zenye mafao ya uzeeni na si uchuuzi. Kwa hiyo utaona kwamba umaskini hauondolewi kwa pesa au teknolojia bali unaondolewa na siasa safi, uongozi bora na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi. Hili ndiyo suluhiso sahihi lililokuwa ndani ya Azimio la Arusha.

Mtazamo wa pili ni ule wa nchi tajiri za magharibi kuziwezesha nchi maskini katika nyanja za menejimenti na usimamizi wa biashara, kilimo, uchimbaji madini, uvuvi, ufugaji kupitia uwekezaji ili kuongeza uzalishaji.

Pia kutoa msaada wa kitaalamu wa kuwasaidia watu katika nchi maskini kuongeza uzalishaji katika kilimo na mifugo na namna ya kupata mikopo kwa wanaojiajiri katika sekta isiyo rasmi, na kuwapa mafunzo ya kuboresha uzalishaji wao.

Lakini katika uhalisia wa mambo wawekezaji hawalipi kodi. Wanachuma na kupeleka kwao na ni kiwango kidogo sana cha pesa kinabaki katika nchi.

Pia nchi zetu hazina mifumo na taasisi imara za kuwasidia wakulima. Ushirika umekufa. Kilimo hakina tija. Wakulima wakichukua mkopo, riba inawavunja mgongo. Na suluhisho linarudi pale pale kuwa ni siasa safi, uongozi bora na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.

Mtazamo wa tatu ni umaskini unasababishwa na kutokuwepo/ kutokuheshimu haki za binadamu. Kwamba wale wenye nguvu katika kudhibiti uzalishaji na uuzaji katika soko huria basi ndio wataendelea kutajirika na wasioweza watakuwa mafukara.

Tanzania imelikumbatia sana soko huria. Hapa suluhisho ni wasio na nguvu katika soko basi wapewe haki ya kulifikia soko na kuuza. Tumewasikia watawala wakisema soko la Ulaya na Marekani liko wazi pelekeni bidhaa zenu. Ni nani mwenye nguvu ya kushindana katika soko hili ingawa tayari anayo haki?

+447404486150
0
No votes yet