Mkuu wa Wilaya ya Tarime kuwadi wa Barrick


Nyaronyo Mwita Kicheere's picture

Na Nyaronyo Mwita ... - Imechapwa 26 October 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, John Henjewele

KWA Mheshimiwa sana, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, John Henjewele; Salaam.

Baada ya salamu hizi, napenda kukujulisha kwamba mimi na familia yangu hatujambo huku kwetu Tungi – Kigamboni jijini Dar es Salaam; hofu na mashaka ni juu yako wewe uliye mbali na sisi huko kwetu Tarime mkoani Mara.

Madhumuni ya waraka huu mfupi kwako ni kukujulisha kwamba mimi na wenzangu wapenda amani na maendeleo tumekuchoshwa na vitimbi vyako ambavyo vimezidi kipimo na sasa unaelekea kubaya.

Mambo uliyowafanyia wakazi wa Nyamongo, hasa wenyeviti wa vijiji vya Kewanja, Nyangoto na Matongo hayavumiliki na sasa mimi najitokeza hadharani  kupasua jipu.

Utakumbuka kwamba hii si mara ya kwanza mimi na wewe kupishana katika mambo ya msingi kuhusu wenyeviti wa Kewanja, Tanzania Omtima (CHADEMA), Elisha Marwa Nyamhanga wa Nyangoto (CCM) na Daudi Itembe Nyamhanga Itembe wa Matongo (CCM).

Sielewi ni kwa nini unawaandama watoto hawa wadogo tena bila aibu hata unavunja sheria, kanuni na taratibu za utawala bora kushughulikia mambo ya kiserikali ili kuufurahisha uongozi wa mgodi wa North Mara unaomilikiwa na African Barrick Gold.

Nimefuatilia kauli zako, tangu Septemba mwaka jana uliposhirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Fidelis Lumato na mgodi wa North Mara kuandaa semina iliyofanyika Mwanza.

Katika semina ile ya tarehe 28 Septemba 2010, kwa mara ya kwanza, mgodi ulitoa wazo la kufuta mikataba ya awali kati ya vijiji na mgodi. Wazo hilo lilipokataliwa na viongozi wa vijiji saba vinavyouzunguka mgodi wa Nyamongo, wewe na Lumato mlisusa na kuondoka mkutanoni. 

Mlisusa ili iweje? Ninyi viongozi mnaopaswa kusaidia wanavijiji kufikia makubaliano yenye manufaa kwa wananchi mnalazimisha mikataba kwa niaba ya mgodi kwa malipo yepi? Mna hisa ngapi Barrick?

Tarehe 31 Desemba 2010 ulikutana na Halmashauri ya Kijiji cha Nyangoto ambako ulisema hakutakuwa na kulipiwa karo watoto wao kwa sababu mgodi hauhusiki na uzazi wao.

Baadaye siku hiyo hiyo ulipokutana na Halmashauri ya Kijiji cha Kewanja ulianza kufoka lakini kabla hujamaliza kuongea wananchi walitawanyika na kukuacha solemba. Ukatamka, “Hata mkitawanyika ninayotaka nitatekeleza, hata mkisema kasemeni mimi ninaongea na (Rais Jakaya) Kikwete muda wote, sibabaiki.”

DC, hata kama unaongea na Rais Kikwete kila siku, au Waziri Mkuu Mizengo Pinda kila saa au Katibu Mkuu Philemon Luhanjo (ambaye nimeambiwa mnatoka kijiji kimoja) kila dakika, bado wewe unatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Na hili ni jamblo la lazima, si hiari. Kufuata sheria, kanuni na taratibu ni amri inayotokana na matakwa ya katiba na sheria, na wewe Mheshimiwa huko juu ya sheria, unapaswa kuelewa hilo. Mahusiano na mapenzi yako kwa mgodi wa North Mara yasikupofushe ukajisahau.

Siku ile ya 31 Desemba 2010 wewe ulifoka sana kwa sababu eti wenyeviti na Halmashauri zao za vijiji wanagoma kutia sahihi mikataba mipya na mgodi. Mikataba hiyo itafuta mikataba ya zamani kati ya vijiji hivyo na mgodi wa North Mara mikataba ambayo si wewe DC wala Mkurugenzi wala Halmashauri mlioshiriki kuipitisha wala kuisaini mwaka 1994.

Watu wengi pamoja na mimi, tungependa kufahamu kutoka kwako kwamba tangu lini wewe uliajiriwa na mgodi na kupewa majukumu ya Afisa Uhusiano au Mwanasheria wa Barrick wa kusimamia mikataba yake?

Halafu tarehe 1 Mei 2011 ulimwamuru Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime na Rorya kuwaita wenyeviti hawa watatu ofisini kwake na walipofika tarehe 3 Mei 2011 aliwanyang’anya bunduki (bastola) zao licha ya wao kuwa na hati za kumiliki. Kamanda alifanya hivyo kutekeleza amri yako bila hata kuwaambia wenyeviti wale maskini makosa.

Aidha tarehe 17 Mei 2011 uliwaita wenyeviti hao kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuhojiwa huku ukiwatwisha tuhuma kuwa wao ndio wanaoshawishi watu kuvamia mgodi. Ukatishia kuwafunga.

Vilevile tarehe 3 Juni 2011 wewe ukishirikiana na uongozi wa mgodi, mliandaa kikao mjini Tarime mkitaka wenyeviti hao wasaini mikataba yenye vipengele vinavyotaka wapewe dola laki moja na waachane na madai yao yote ya nyuma. Wenyeviti Matongo, Kewanja na Nyangoto kwa kufahamu hilo hawakuhudhuria.

Tarehe 6 Juni 2011 ulimwagiza Lumato kumwondoa Omtima (CHADEMA) naye akamwandikia Mtendaji Kata ya Kemambo aitishe mkutano kwa ajili hiyo bila kufuata utaratibu wa kawaida wa kufuta kazi viongozi wa kuchaguliwa.

Tarehe 12 Septemba 2011 uliitisha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kuagiza tena wenyeviti wa Nyamwaga, Kerende, Nyakunguru na Genkuru, kutia saini mikataba na mgodi na walipokataa kwa sababu haikuwa na mabadiliko ukaikusanya na kuondoka nayo! Matongo, Kewanja na Nyangoto kwa kufahamu hilo hawakuhudhuria tena.

Katika mikataba hiyo kunatolewa pendekezo la vijiji kulipwa dola laki moja ili wafute madai yao yote ya nyuma, nawe ukasisitiza kuwa lazima vijiji visaini mikataba hiyo. Na ulikimbia na nakala zote ukidhani hawatapata nyingine. Kwa taarifa yako, wamepata nakala hiyo kwingineko nami ninayo moja.

Tarehe 20 Septemba 2011 ilikuwa funga mwaka. Katika kikao cha pamoja cha kamati za ulinzi za mkoa wa Mara na wilaya ya Tarime uliwatuhumu wenyeviti wa Matongo, Kewanja na Nyangoto kuwa wameandaa watu kumfanyia vurugu Waziri Mkuu  Pinda kwenye ziara yake Nyamongo.

Mbaya zaidi ukadai watu walioandaliwa kumfanyia vurugu Pinda walikuwa wamekusanyika nyumbani kwa Matiku Nega Mwiturubani. Kutokana na taarifa hizi za uongo polisi wakiwa katika ‘defenda’ nne walivamia nyumbani kwa Nega na kukuta umati wa akina mama wakichota maji kutokana na vyanzo vingi  kuchafuliwa na maswahiba wako Barrick.

Alhamisi ya 20 Oktoba 2011 ukadai mkutanoni Matongo kuwa badala ya kufanya shughuli za maendeleo wenyeviti wa Nyangoto (CCM), Matongo (CCM) na Kewanja (CHADEMA) wanakimbiakimbia kuandika magazetini kitu ambacho hakitawasaidia na kwamba wewe utatekeleza ulichokusudia.

Ushauri wa bure. Mheshimiwa DC, fanya mpango na polisi wawabambikie wenyeviti hawa kesi ya mauaji au waende nyumbani kwao watupe bastola uani halafu waseme ni majambazi wamekutwa na silaha. Rahisi kabisa, watafungwa nawe utabaki kufurahi na maswahiba zako bila bughdha.

DC unahangaikia nini? Tumia polisi wenu hao kuwapiga risasi wenyeviti hawa waishilie mbali. Wangapi wameuawa kwa njia hii na wauaji wakaachiwa huru na hata pale walipofungwa wakasamehewa! Shida ipo wapi? Waungwana mkose fedha za Barrick kisa wenyeviti ambao hata shule hawakwenda?

Mwisho nakushauri kazungumze na mwanasheria wa Halmashauri akuelimishe juu ya sheria ya mikataba. Hakuna mkataba hata mmoja unaoingiwa kwa lazima. Yanatumika maneno matamu yaani majadiliano yafanyike kwa hiari na kwa uhuru – siyo kulazimishwa.

Waktabahu.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)