Moses Machali: Nitapambana kulinda NCCR-Mageuzi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 November 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MBUNGE wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Joseph Machali, ameibuka na kusema ndani ya chama chake hakuna mgogoro wa uongozi.

Amesema kilichopo, ni genge la watu wanaoongozwa na wabunge wawili wanaopandikiza mbegu za kutaka kukivuruga chama hicho kwa maslahi yao binafsi.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI juzi Jumatatu, Machali anawataja David Kafulila, mbunge wa Kigoma Kusini na Felix Mkosamali, mbunge wa Muhambwe, kwamba ndio wanaotumika “kukivuruga chama kwa maslahi binafsi.”

Anasema, “Kafulila anataka kumuondoa mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, James Mbatia ili yeye aweze kushika nafasi hiyo. Nina ushahidi juu ya jambo hili,” anaeleza Machali.

“Nimesema ndani ya vikao vya chama na naweza kulisimamia hili mahali popote; kwamba anayeendesha vikao vyenye lengo la kumuondoa Mbatia ni Kafulila…anayetumiwa kuvuruga upinzani ni Kafulila,” anasema Machali.

Anasema, “Nyuma ya Kafulila kuna mwanasiasa mmoja kijana…ni mtu wa karibu sana na Kafulila. Ana ndoto ya kutaka kugombea urais mwaka 2015; lakini hakubaliwi ndani ya chama chake. Hivyo anaona suluhisho ni kuhamia NCCR-Mageuzi ili aweze kupata fursa hiyo.”

Madai yameenea kuwa mwanasiasa huyo ndiye anayemtumia Kafulila kwa madia kuwa Mbatia akiwa mwenyekiti hatamruhusu agombee nafasi hiyo.

Anasema, “Unajua kuna mambo mengi ndani ya mpango huu, ambayo wananchi hawajaelezwa. Wapo watu wanaotaka kuitumia NCCR kama daraja la kuivuruga CHADEMA,” anaeleza Machali.

Ndani ya mpango huu, anasema yupo mwanasiasa mmoja anayetaka kugombea urais na ambaye anatuhumiwa kuivuruga CHADEMA kwa kutaka kuhamisha wanachama na ufuasi, anasema.

Anasema Kafulila anataka uenyekiti, kama kivuli cha watu wengine walio nje ya chama chetu na kuongeza, “Anataka kutumia NCCR-Mageuzi kuivuruga CHADEMA na kudhoofisha mageuzi. Hivyo, nimeamua kupambana naye kwa kuuarifu umma kuwa chokochoko zote hizi, chimbuko lake ni Kafulila na genge lake.”

Machali alikuwa akijibu maswali ya mwandishi wetu. Ilibidi apigiwe simu tena kufafanua baadhi ya maoni yake.

Swali: Huyo mwanasiasa ni wa chama gani na ana nafasi gani katika chama chake?

Machali: Ni mbunge na anatoka mkoa wa Kigoma.

Swali: Kama ni hivyo, basi atakuwa anatoka ama CCM au CHADEMA, kwani ndio vyama vikubwa na vyenye wabunge Kigoma.

Machali: Ni kweli (hakufafanua).

Swali: Anayejulikana kuwa rafiki wa Kafulila ni Zitto Kabwe, aliyewahi kutamka hadharani kuwa atampigia kampeni awe mbunge pale alipotimuliwa (Kafulila kutoka) CHADEMA. Ni huyo?

Machali: Yote yatakuwa wazi. Hakuna litakalobaki gizani. Nawe tafuta kwa njia yako.

Gazeti hili linaweza kuripoti kuwa mbunge aliyewahi kuonyesha kutaka kugombea urais ni Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini na naibu katibu mkuu wa CHADEMA. Amekuwa akisikika pia kutaka kugombea urais mwaka 2015.

Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umri wa kugombea urais ni miaka 40 ambayo Zitto hajafikisha. Labda yafanyike mabadiliko katika “katiba mpya;” ya kuteremsha umri kufikia miaka 35 ambayo atakuwa amefikisha.

Akieleza hatua kwa hatua ilivyokuwa, Machali anasema, “Kafulila amekuwa akinieleza kuwa kuna wanasiasa wakubwa wanaotaka kujiunga na NCCR-Mageuzi, lakini wanashindwa kwa sababu ya Mbatia.”

“Baadhi ya aliowataja ni viongozi wakubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na wengine kutoka vyama vingine vya upinzani,” ameeleza Machali.

Uvumi ulioenea ni kwamba Kafulila akiwa mwenyekiti NCCR-Mageuzi, vigogo wa CCM wanaotaka kukimbia chama hicho wataingia huko; naye atamwachia uongozi mmoja wao, huku “rafiki yake” (Zitto) atakuwa mgombea urais.

Kuhusu Mkosamali, Machali anasema, “Huyu anaonekana kuburuzwa au kutumiwa na Kafulila katika jambo hili, pengine kutokana na kutofahamu vizuri kilichopo nyuma ya mkakati huu.”

Katika mpango wa kumuondoa Mbatia, Kafulila anadaiwa kumshirikisha au kushirikiana na Hassan Mbwana, kamishana wa chama hicho kutoka mkoa wa Tanga.

Ni Mbwana aliyewasilisha hoja ya maandishi kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kwamba Mbatia hana sifa ya kuwa mwenyekiti wa chama.

Mwana anadai kuwa tangu alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama, Mbatia ameshindwa mara mbili kwenye uchaguzi mkuu katika  jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro mwaka 2000 na uchaguzi wa ubunge kwenye jimbo la Kawe, mwaka 2010.

Hata hivyo, wanaomtetea Mbatia wanasema, kushindwa kwenye uchaguzi si hoja. Wanatoa mfano wa viongozi kadhaa wa kitaifa walioshindwa kwenye uchaguzi.

“Hoja si Mbatia kushindwa kuongoza chama, kama ambavyo Mbwana ameeleza Machali, bali ni kwamba Kafulila anataka uenyekiti wa chama.”

Anasema “kundi hili” ndilo linaeneza uzushi kuwa Mbatia anakula, kila mwezi, ruzuku ya chama ya Sh. 120 milioni; wakati wanajua kabisa ruzuku ya NCCR- Mageuzi ni Sh. 12 milioni kwa mwezi.

Anasema kwa vyovyote itakavyokuwa, NCCR Mageuzi, haiwezi kukabidhiwa kwa watu wasiokuwa na maadili na vibaraka wa waliopo madarakani na wale wanaowashabikia.

Machali anasema hakuna binadamu aliyekamilika. Anasema inawezekana Mbatia akawa na mapungufu, “lakini mapungufu hayo hayatoshi kumuondoa kwenye uenyekiti wa chama na kukikabidhi kwa mtu kama Kafulila na genge lake.”

Alipoulizwa iwapo ni kweli kuwa baadhi ya wajumbe wa NEC walihongwa ili kupitisha azimio la kumuondoa Mbatia kwenye uongozi, Machali alisema, “Nimesikia hilo, na kwamba fedha hizo zimetolewa na jamaa hao wawili.”

Anasema katika jimbo lake kuna tatizo kubwa la ujambazi. Katika kukabiliana nalo ameamua kushirikisha wananchi kuwafichua wale wote wanaotajwa kuwa na tabia za uhalifu.

Kingine ambacho Machali anakitaja kuwa kinamnyima usingizi, ni  migogoro ya wakulima na wafugaji kutokana na uhaba wa maeneo ya kilimo na na malisho ya mifugo.

Moses Joseph Machali alizaliwa 9 Agosti 1981 wilayani Kasulu, mkoani Kigoma. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi, Mwenge, wilayani Kasulu, kati ya mwaka 1990 na 1996. Mwaka 1997 alijiunga na Shule ya Sekondari Kasulu. Alimaliza masomo yake hayo mwaka 2000.

Baada ya kumaliza masomo ya sekondari, Machali alijiunga na Chuo cha Ualimu Kasulu kati ya mwaka 2001 na 2002 alipohitimu na kupata cheti cha daraja A. Ni mhitimu wa chuo kikuu cha St. Augustine, jijini Mwanza mwaka 2007.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: