Moto wawaka UWT


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 24 June 2008

Printer-friendly versionSend to friend
Ni vita vya wanamtandao maslahi, matumaini
Anne Kilango Malecela: Huko mimi simo
Sophia Simba, Waziri wa Maendeleo ya  Jamii, Jinsia na Watoto

VIGOGO wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshika koo, kuwania nafasi ya mwenyekiti wa umoja huo, imeelezwa.

Taarifa za ndani zinasema tayari baadhi ya wanasiasa wanaowania nafasi hiyo, ama wao wenyewe ama kupitia mawakala wao, wameanza kupita mikoani kutafuta kuungwa mkono.

Nafasi ya mwenyekiti wa UWT kwa sasa inashilikiwa na Anna Abdallah ambaye kwa mujibu wa wapambe wake, amesema "hana mpango wa kugombea tena nafasi hiyo."

Miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa kutaka kuwania nafasi hiyo, ni pamoja na Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margreth Sitta na mbunge wa Piramiho, Janet Mhagama.

Wengine ni mbunge wa kuteuliwa, Janet Kahama, mbunge wa Mlandege-Unguja, Fatuma Said Alli na mwanasiasa machachari Shey-Rooze Banji.

Shey-rooze alithibitia mwandishi wa habari hizi majuzi mjini Dodoma kwamba atawania nafasdi hiyo. Alisema tayari amejipima na kutafakari ikiwa pamoja na kupata ushauri kutoka kwa wanasiasa wakongwe.

"Mimi nitajitosa katika kiti. Nagombea na ishaala mungu atasaidia jina langu litarudi na nitashinda," alisema kwa njia ya kusisitiza.

Hata hivyo, taarifa za ndani ya umoja huo zinasema, mwenyekiti anayeondoka tayari analochaguo lake. Anayetajwa ni Janet Kahama.

"Unajua hata vijembe ambavyo mama (Anne Abdallah) alikuwa anavirusha wakati wa kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha, vililenga kiti cha UWT," alisema mjumbe mmoja ambaye hayupo katika kambi ya mwenyekiti.

Alisema, "Huyu mama inasemekana anamgombea wake anayetaka kumuachia kiti. Ndiyo maana alihakikisha anammaliza Kilango (Anne Kilango)."

Akichangia mjadala wa bajeti, Anna Abdallah alisema kwamba hakuna mbunge anayeweza kutishwa na wala bungeni hakuna vitisho, kauli iliyotafsiriwa na wachambuzi wa mambo kwamba ililenga Kilango.

Alahamisi iliyopita, mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango alikuna Watanzania na baadhi ya wabunge pale aliposimama bungeni na kusema, "kama fedha za EPA hazitarudishwa hapatatosha."

Alisema kwa muda mrefu ulinzi wa fedha za Watanzania ulikuwa hauko salama, na kuhakikishia umma kuwa atasiama imara kuhakikisha fedha zilizoibwa zinarudishwa.

"Wewe hujui. Mwenyekiti wakati anachangia, si kwamba alikuwa amenunuliwa na wale wanaotuhumiwa na ufisadi, hapana. Alikuwa katika vita ya kutaka kuacha kiti chake kwa mtu wake," alisema mtoa taarifa.

Alisema, "Huyu mana alimuona Kilango kwamba ni hatari kwake. Nadhani anajua kwamba anataka kiti," alisema mbunge huyo."

Kuna taarifa kuwa Kilango, ni miongoni mwa wanasiasa watakaojitosa kuwania nafasi hiyo.

Hata hivyo, Kilango aliliambia MwanaHALISI wiki hii, kwamba hana mpango wa kuwania nafasi hiyo, kwa kile alichokieleza "tayari ninalojukumu la kutumikia wananchi wangu."

"Unajua moja ya jambo ambalo watu wanataka kiti kile, ni kuwa na uhakika wa kuwa mbunge. Mimi tayari ninalojimbo langu. Na bado ninatamani kuendelea kuwa mbunge wa jimbo. Sasa intake kiti cha UWT kwa kazi gani," alisema Kilango katika mahojiano yaliochapishwa kwa ukamilifu katika uk-7 wa gazeti hili.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kujitoa kwa Kilango kunaweza kukafungua njia kwa mgombea anayetokana na "kundi la mtandao matumaini."

Kundi la mtandao matumaini limetokana na mgawanyiko wa kundi la mtandao na kuzaliwa kwa makundi ya mtandao matumaini na mtandao maslahi. Haya ni makundi yaliotokana na mtandao uliomuigiza Jakaya Kikwete madarakani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: