Mpelelezi aponda uwezo wa Netanyahu


mashinda's picture

Na mashinda - Imechapwa 01 August 2012

Printer-friendly version

MKUU wa zamani wa Idara ya Upelelezi iitwayo Shin Bet, amedai kuwa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi, Ehud Barak hawana uwezo wa kuiongoza Israel katika vita na wanapotosha umma dhidi ya vitisho vya Iran.

“Waziri wa Ulinzi, Ehud Barak na Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu wanawapotosha Waisrael kuhusu kitisho kutoka Iran,” alisema mkuu huyo wa zamani wa Shin Bet, Yuval Diskin.

Bosi huyo wa upelelezi Diskin ameushutumu mzaha wa utawala wa kisiasa kwa kuzungumza sana kuhusu uwezekano wa kufanya shambulio la kijeshi dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran.

Katika maoni yake kwa uwazi yenye lengo la kuzidisha mgogoro dhidi ya Iran, Diskin aliyestaafu ukuu wa idara hiyo mwaka jana alisema “hana imani” na uwezo wa Netanyahu na Barak kuanzisha na kusimamia vita.

Viongozi hao, ambao wako mstari wa mbele kuhusu uchukuaji hatua za kijeshi dhidi ya proramu za nyuklia za Iran hawakuwa na “uwezo wa kusukuma mbele gurudumu la vita,” alisema Diskin Ijumaa iliyopita.

"Tatizo langu kubwa ni kwamba sina imani na uongozi wa sasa ambao unatakiwa kutuongoza katika kipindi cha vita dhidi ya Iran au vita vyovyote eneo hili, ” alisema.

"Simwamini waziri mkuu wala waziri wa ulinzi. Siamini uongozi huu kama unaweza kufanya maamuzi mazito. Niaminini, nimewachunguza kwa karibu sana…Hawa si watu ambao mimi binafsi nawaamini kuiongoza Israel katika matukio kama hayo na wakasimamia sawia.

"Wanaupotosha umma kuhusiana na suala la Iran. Hawa wanasema eti Israel ikishambulia, Iran haiwezi kubakiwa na bomu. Huu ni upotoshaji. Ukweli, wataalamu wengi wa masuala ya kijeshi wanasema kuwa shambulio lolote kutoka Israel litaichochea Iran katika mbio za kutengeneza nyuklia."

Hayakupatikana mara moja majibu kutoka ofisi ya waziri mkuu.

Maoni hayo ya Diskin yalikuja baada ya kuibuka kauli zenye msisimko Jumatano iliyopita na mkuu wa jeshi, Benny Gantz, iliyotofautiana na kauli za mara kwa mara za Netanyahu kuhusu Iran.

Gantz alisema kwamba haamini kama utawala wa Iran umejiandaa “kwenda maili moja zaidi” kumiliki silaha za nyuklia kwa sababu “ina mchanganyiko wa watu waungwana” wanaoelewa madhara yake.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni kukemea msimamo wa waziri mkuu, Gantz aliongeza: "Maamuzi yanaweza na lazima yafanywe kwa uangalifu sana kwa kuzingatia historia bila jazba."

Si Netanyahu wala Barak aliyerekebisha kauli yake. Hivi karibuni waziri mkuu alikaririwa akisema kwamba wale wanaodharau kitisho cha nyuklia kutoka Iran “hawajajifunza lolote kutokana na mauaji ya halaiki". Aliongeza: "Utawala wa Iran unatoa wito wa wazi wa kutuangamiza na wanafanya juhudi usiku na mchana ili hatimaye wafikie kutengeneza silaha za nyuklia."

Alhamisi iliyopita, Barak alisema nafasi za Iran kusitisha programu za nyuklia baada ya kuwekewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa inaonekana kuwa ndogo.

0
No votes yet