Mpendazoe aendelea kutesa

- Achota mamilioni bungeni
- Chiligati apigwa na butwaa
BUNGE la Jamhuri linaendelea kumlipa mshahara mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe, imefahamika.
Taarifa za ndani ya ofisi za Bunge mjini Dar es Salaam zinasema Mpendazoe anaendelea kupokea mamilioni yake ya shilingi ingawa aliishatamka kuwa anaondoka CCM.
Hata madai kuwa Mpendazoe aliandika barua kwa Spika Samwel Sitta akimweleza kuwa amejiuzulu uanachama CCM, yameshindikana kuthibitishwa na ofisi ya bunge.
Bali Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila amelithibitishia MwanaHALISI kuwa kimsingi, bunge linalazimika kumlipa Mpendazoe mshahara wake wa kila mwezi.
Amesema hii ni kutokana na ofisi yake kutopata taarifa rasmi kutoka CCM zinazoeleza ukomo wa uanachama wa Mpendazoe.
“Huwezi kusimamisha mshahara wa mtu kinyemela. Taratibu zetu ziko wazi, kwamba chama kinachohusika kinapaswa kutufahamisha kuwa Mpendazoe si mwanachama wao. Lakini mpaka sasa, hawajafanya hivyo,” ameeleza Dk. Kashilila.
Alipouliza wanamlipa kwa misingi ipi wakati hayupo bungeni, Dk. Kashilila alisema, “Zile fedha za vikao hawezi kupata kwa sababu hajahudhuria. Lakini fedha za mshahara zinatakiwa kuingizwa kwenye akaunti yake na ndivyo bunge linavyofanya.”
Katibu wa Bunge amesema ofisi yake haijapokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM, kwa hiyo bunge bado linaendelea kumtambua Mpendazoe kuwa mbunge halali.
“Hatujakatisha mshara wake. Bado tunaupeleka katika akaunti yake kama taratibu zinavyoagiza. Tutaendelea kufanya hivyo hadi chama chake kituletee taarifa,” amesema Dk. Kashilila.
Amesema nchi hii inaendeshwa kwa misingi ya sheria na kwamba ofisi yake haiwezi kuzuia haki za mbunge au mfanyakazi mwingine bila kufuata taratibu au sheria.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba hakupatikana kutoa maelezo lakini mwezi mmoja na nusu uliopita alinukuliwa akisema si yeye binafsi wala CCM ambaye ana “ugomvi na Mpendazoe.”
Lakini Katibu Mwenezi wa CCM, John Chiligati, akiongea na gazeti hili kwa simu alisema tayari chama kimelifahamisha bunge kuhusu hadhi ya Mpendazoe.
Hata hivyo amesema anakiri na kusikitika kuwa walichelewa kufanya mawasiliano hayo.
Chiligati anasema walichelewa kuandika barua kwa bunge kwa vile walidhani Mpendazoe angewataarifu rasmi badala ya kupitia vyombo vya habari.
Alisema, “Tumekaa naye vizuri. Alipoondoka tulidhani angefanya uungwana. Angesema, ‘Mimi nilikuwa kwenu. Mambo yenu siyawezi bwana. Naondoka.’”
Swali: Sasa mliandikaje barua bila yeye kuwaambia.
Jibu: Tuliandika kuwa bwana huyu, akiwa na akili timamu, ametangaza mwenyewe kwamba ameondoka kwenye chama chetu na sisi ndio tuliompa ubunge wa Kishapu; kwa hiyo tunataarifu ofisi ya spika juu ya jambo hilo.
Naye Mpendazoe alipoulizwa juu ya bunge kuendelea kumpelekea mshahara benki, alijibu kwa sauti ya mshangao, “Eh, bado wanapeleka?”
Ilikuwa saa 2.40 usiku lakini alimwambia mwandishi kuwa anakwenda benki “sasa hivi kuona kama zipo” kwa vile alisema ana akaunti maalum kwa ajili ya mshahara.
Alilieleza gazeti hili kuwa amekutana na katibu wa bunge ambaye alimweleza kuwa bado anatambuliwa kuwa ni mbunge wa Kishapu.
Machi mwaka huu, Mpendazoe ambaye alikuwa mmoja wa wabunge waliojipambanua katika vita dhidi ya ufisadi, alitangaza kuhama CCM na kujiunga na Chama cha Jamii (CCJ) kilichopata usajili wa awali.
Muda wote amekielezea chama chake cha zamani kuwa “kimegeuka gulio la kila mtafuta cheo na utajiri haramu.”
Amesema CCM “imegeuka kimbilio la kila mwenye dhamira ya ulanguzi… imepoteza maadili ya uongozi na imekuwa ngome ya mafisadi wanaotafuna utajiri wa nchi yetu.”
Mpendazoe alijizolea umaarufu kutokana na ujasiri wake wa kuibana serikali kushughulikia “watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.”
Wakati Mpendazoe anatangaza kuhama CCM alisema anakiacha chama hicho baada ya kuishiwa matumaini.
“Nimeishi kwa matumaini, nikitegemea siku moja mambo yatabadilika ndani ya CCM, lakini mpaka leo sioni dalili yoyote. Ni heri niheshimu dhamira yangu,” alisema.
Aliuambia mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, “Watanzania sasa wanahitaji mabadiliko mapya, kizazi kipya, mtazamo mpya, ambao hauwezi kuletwa na CCM.”