Msemakweli ama hajui asemacho au anatumiwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

MTU huyu anatumika kuficha ukweli. Ni Kainerugaba Msemakweli. Anasema mabilioni ya shilingi yaliyokwapuliwa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited (KAL), ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT) hayakutumika kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Anasema wezi wa Kagoda walichota fedha BoT, Februari 2006, na kwamba uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ulimalizika Novemba 2005. Yote haya yanaonyesha jinsi Msemakweli, ama anavyotumika bila kujijua, au anavyotumiwa na watu wenye malengo binafsi.

Kile ambacho wengi hawajakifahamu, ni nani anayemtumia Msemakweli. Je, aweza kuwa anatumiwa na Kagoda au anatumiwa na wapinzani wa Kagoda?

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari (Alhamisi iliyopita jijini Dar es Salaam, Msemakweli amekuja na madai mawili makubwa. Kwanza, fedha za Kagoda hazikutumika kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.  Anasema ushahidi wake ni “nyaraka zinazoonyesha Kagoda iliiba fedha BoT, Februari 2006 na ilizisafirisha nje ya nchi Machi 2006.”

Pili, Msemakweli anatetea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa hakikutumia sehemu ya fedha hizo kuingia madarakani. Hatua hii inaleta maswali mengi kuliko majibu; yakiwa ni pamoja na iwapo Msemakweli anafahamu anachikitenda.

Kwanza, hati ya kiapo ya wakili Bhyidinka Sanze wa kampuni ya mawakili ya Malegesi – Malegesi Law Chambers – ya Dar es Salaam, kwa Kamati ya rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inaeleza fedha za Kagoda ziliibwa ili kufanikisha kampeni za CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Sanze anakiri kuwa ni yeye alishuhudia “…mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.”

Andishi lake linaeleza kuwa Rostan Aziz, Peter Noni na Bered Malegesi walimthibitishia kuwa Rostam alikuwa kwenye kikao ambako rais mstaafu Benjamin Mkapa alitoa maelekezo kwa Gavana wa BoT, Dk. Daudi Ballali kutoa fedha hizo kwa Rostam kwa ajili ya uchaguzi.

Sanze anasema, “Niliitwa na Bw. Malegesi ofisini kwa Bw. Rostam Aziz…Nilipofika…niliwakuta Bw. Rostam Aziz, Peter Noni (Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa benki ya raslimali) na Bw. Malegesi; wakaniambia fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa CCM na rais wake.”

Hili ni andishi ambalo mpaka sasa halijakanwa na serikali, Mkapa, Rostam, Sanze, Meregesi wala Peter Noni.

Je, Msemakweli anayedai amefanya utafiti wa suala hili kwa miaka miwili mfulululizo hajaliona andishi hili? Hakulitafuta? Kama ameliona, kwa nini anataka kuficha ukweli? Kama hakuliona, kwa nini hakuuliza walilonalo?

Kama hakuliona andishi la Sanze, hakulitafuta na hakuuliza walilonalo, anatoa wapi ujasiri wa kusema, “fedha za Kagoda hazikuibwa kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005?” Anamtumikia nani na nani anataka kumuokoa au kumzamisha?

Kampuni ya Kagoda ilikwapua jumla ya dola za Kimarekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya BoT.

Fedha hizi ziliibwa kati ya Septemba 2005 na Novemba 2005. Kagoda ilifanikiwa kuchukua fedha BoT na kuzipitisha katika matawi saba ya benki ya CRDB jijini Dar es Salaam kwa mtindo wa “kuingiza na kutoa papo hapo.”

Aidha, serikali imekuwa ikijikanyaga kuhusu wizi huu. Aliyekuwa waziri wa fedha, Zakia Meghji aliwaandikia maodita wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini akisema, fedha za Kagoda zilitumika kwa “kazi za usalama wa taifa.”

Katika barua yake ya 15 Septemba 2006, Meghji anasema, “Kama unavyofahamu vema, mamlaka ya serikali huwa na siri, vilevile haja ya kugharamia matumizi ya busara.

“Kwa hiyo... malipo ya dola 30,732,658.82 za Marekani yaliyofanywa na BoT kwa Kagoda Agriculture Limited, yaliidhinishwa na serikali kugharamia matumizi yake nyeti na ilikuwa lazima kuchukua hatua hii ya kudumisha usiri huu.”

Msemakweli anajichanganya pia katika eneo jingine ambamo anamtaja mmoja wa wafanyabiashara mashuhuri nchini, kwamba ndiye aliyesafirisha fedha hizo Machi 2006.

Lakini nyaraka ambazo amezitumia kupeleka shauri hilo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), zinaonyesha mfanyabiashara anayemtaja, ameingia mkataba wa kukopeshana fedha na Kagoda 12 Septemba 2005, kipindi ambacho Kagoda yenyewe ilikuwa haijasajiliwa.

Kuna visingizio vingi vimetumika kuhalalisha wizi huu na kutaka kuisafisha CCM. Kwa mfano, mara kadhaa serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamnbana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Waziri wa Fedha, Mustaph Mkullo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na DPP, Eliezer Feleshi wamedai, kwa nyakati tofauti kuwa Kagoda haifahamiki na haijulikani iliko.

Lakini ni Kagoda inayodaiwa kumuondoa nchini aliyekuwa gavana wa BoT, Dk. Daud Ballali. Baadaye serikali ikaeleza, “gavana Ballali ameaga dunia.”

Pili, Msemakweli anasema fedha zisingeibwa mwaka 2006 ili kutumika mwaka 2005. Hata kama tukikubaliana na Msemakweli, kwamba fedha ziliibwa benki mwaka 2006, bado huo hauwezi kuwa utetezi.

Je, haiwezekani wezi wa Kagoda wakaipa CCM fedha mwaka 2005 kwa makubaliano kuwa wajilipe mwaka 2006 kwa kutumia EPA?

Nyaraka zinaonyesha kuwa hata kabla kampuni hiyo kusajiliawa, Kagoda tayari ilishachota sehemu ya fedha ilizokwapua.

Kwa mfano, aliyeitwa Meneja Mkuu wa Kagoda, John Kyomuhendo anaonekana akimwandikia Gavana wa BoT tarehe 12 Septemba 2005. Barua nyingine ya Kagoda, ikikumbushia nia ya kuhamisha fedha kutoka BoT iliandikwa tarehe 7 Oktoba 2005.

Naye gavana anajibu mawasiliano hayo kwa barua Kumb. Na. 6054/1355 ya 13 Oktoba 2005 inayofuatwa na barua ya Kagoda ya 20 Oktoba ikielekeza uhamishaji wa fedha kwenda benki.

Maelekezo ni kwamba fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti Na. 01J021795700 iliyoko benki ya CRDB tawi la Holland jijini Dar es Salaam.

Barua kutoka Kagoda inayoelekeza jinsi ya kuhamisha zaidi ya Sh. 25 bilioni ilipokelewa na benki siku hiyohiyo ya 20 Oktoba 2005, kuwekwa katika faili na kupewa namba (folio) 7.

Wakati mawasiliano yote yakifanyika, ikiwa ni pamoja na kuchota mabilioni ya shilingi, Kagoda ilikuwa haijasajiliwa. Biashara ilikuwa “mali kauli.”

Kagoda ilisajiliwa na Msajili wa Makampuni (sasa wakala wa usajili wa makampuni – BRELA) tarehe 29 Septemba 2005 na kupewa hati Na. 54040, huku wakiwa tayari wamekwapua mabilioni ya shilingi kwa kauli tu.

Pamoja na uhalifu huu wa wazi wa Kagoda, kwa kushirikiana na BoT, ambao ulifahamika kwa wajumbe wa Timu ya Rais na bila shaka kwa rais mwenyewe, Msemakweli anataka kulinda wezi.

Hapa inaonyesha jinsi Msemakweli alivyokuwa tatizo badala ya suluhisho katika sakata la Kagoda. Kisheria, Msemakweli anageuka shahidi tata au shahidi adui, na kwamba vyombo vya – upelelezi (ofisi ya DCI, DPP na TAKUKURU), ni sharti viwe makini naye.

Shahidi anayefunua ukweli na kuufunika hapohapo huwa ana dalili za kutumiwa na wale anaodai kuwa anawashitaki bila yeye kujijua. Msemakweli anajua, kwamba Rais Jakaya Kikwete aliunda Kamati Maalum ya rais ya kufuatilia walioiba benki. Anafahamu Kamati Maalum ya rais ilivyomweleza Rais.

Kwamba baadhi ya wezi waliorudisha fedha na kusamehewa kinyume cha sheria, wanalalamika kutapeliwa kwa kuwa wamelazimika kurudisha hata fedha ambazo walizigawa kwa CCM ili kufanikisha harakati zake za uchaguzi mkuu wa 2005. Miongoni mwao, ni Kagoda Agriculture Limited.

Kama Msemakweli hayafahamu haya, basi hana sababu ya kusema amefanya utatiti. Aseme, “Nimehadithiwa na walionituma.” Ikiwa wezi wenyewe wanakiri kurudisha fedha kwa niaba ya Kagoda, Msemakweli anapata wapi ujasiri wa kuisafisha CCM kuwa haikuchukua fedha hizo?

Vilevile, wanaotuhumiwa kuiba fedha kwa mgongo wa Kagoda, wanalalamikiwa na baadhi ya wana-CCM, kwamba hawakuwakilisha fedha yote waliyoiba benki ndani ya chama. Badala yake, wanadaiwa kutumia fedha hizo kujitajirisha binafsi.

Ni utajiri huo ndio unaotumika kuwanyanyasa wale ambao hawakupata mgawo. Je, madai haya ni ya uongo? Kama ndiyo, mbona ndani ya CCM kumeibuka minyukano isiyoisha, inayotokana na tuhuma za wizi wa fedha hizo, kwamba baadhi ya wanaotuhumiwa kushiriki wanasema zimetumika kuingiza serikali hii madarakani?

Rais Kikwete mwenyewe siyo tu anaamini hivyo, bali mbele ya wananchi anatazamwa kama mtoto wa Kagoda na mjukuu wa EPA.

Hata baadhi ya wananchi wa kawaida, wakiwamo wana-CCM na viongozi wake, wanaamini Kagoda ndiyo iliingiza serikali hii madarakani. Kagoda ndiyo sababisho la minyukano isiyokwisha ndani ya chama.

Aidha, ni kiini cha kuibuka kwa tamthilia mpya ya kujivua gamba na ndiyo sababu ya serikali kuingia katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga, miezi 10 baada ya kumalizika uchaguzi mkuu.

Katika mazingira haya, wananchi wamebaki na jambo moja la kuamini. Kwamba ni kweli kuwa Msemakweli ametumwa na waliomtuma wanafahamika. Ni wale waliokuwa mstari wa mbele kujionyesha wanapambana na ufisadi, lakini papohapo wakikumbatia ufisadi wa kisingizio cha kuitetea CCM.

Ndiyo msingi wa madai yake haya. Kwamba “fedha za Kagoda hazikutumiwa kufanikisha mgombea wa CCM kuingia madarakani.”

Jambo moja ni muhimu. Hatua ya Msemakweli kutetea CCM, kwamba haikutumia fedha za Kagoda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, inazidisha kiu ya wananchi kutaka kufahamu Kagoda ni nani na ana uhusiano gani na Msemakweli anayemtetea?

Jingine ambalo wananchi watataka kufahamu kwa kutumia mizani ya Msemakweli, ni serikali inashughulikia vipi “ukweli” aliousema Msemakweli na kuachana na propaganda zake za kuwasafisha wezi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: