Mshindani wa Museveni atahimili vishindo?

JE Kapteni Mstaafu wa Jeshi, Daudi Ruhinda Maguru atabaki ni mshindani madhubuti wa Rais Yoweri Museveni katika harakati za Chama cha National Resistance Movement (NRM) kutafuta mgombea wake wa urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao?
Hili ni swali kubwa ambalo limeanza kuulizwa na wachambuzi wa siasa za Uganda kwa sasa baada ya Kapteni Ruhinda kutangaza kutaka kushindana na kamanda wake jeshini kugombea urais kupitia chama hicho.
Msingi wa kuulizwa swali hili ni yaliyotokea huko nyuma baada ya Dk. Kizza Besigye kujitokeza mwaka 2000 kumpinga Museveni katika urais kupitia NRM. Kama alivyo Kapteni Ruhinda, Dk. Besigye alikuwa mshirika mkuu wa Museveni wakati NRM kikiwa kikundi cha waasi dhidi ya serikali ya kidikteta ya Idi Amin Dada.
Dk. Besigye aliyeacha jeshi la Uganda akiwa na cheo cha Kanali, alionekana kama kiongozi asiye na nidhamu kwa mkuu wa nchi na msaliti. Alilazimika kukabiliana na vitisho na mikakati ya kummaliza na hivyo kuchukulia mikakati hiyo kama jitihada za kutaka kumuua.
Kapteni Ruhinda, alianza kujitambulisha kama mshindani wa Rais Museveni ndani ya NRM ulipofanyika mkutano mkuu wa chama Juni 25 hadi Julai 2, kwenye ukumbi wa mikutano wa Mandela uliopo Namboole.
Bila ya wajumbe kutarajia, walishtukia bango kubwa lililokuwa na picha ya Kapteni Ruhinda akiwa amevalia sare za jeshi, akitangaza nia ya kuomba chama kiteue kugombea urais utakapofanyika uchaguzi mkuu.
Kapteni Ruhinda amesema mapema kuwa hatua yake hiyo haina maana anamdharau kamanda wake, Rais Museveni. Kinyume chake anasema kama vile walivyofanya viongozi mashuhuri Nelson Mandela wa Afrika Kusini na Daniel arap Moi wa Kenya kuachia makamanda wao kushika madaraka ya nchi huku wao wakongwe wakibaki kutoa ushauri, ndivyo anatarajia Museveni ataichukulia hatua hiyo.
Miezi michache iliyopita, Felix Okot Ogong alitangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya NRM. Kilichofuata ni Meja Jenerali Kahinda Otafire ambaye ni mmoja wa wanaowania nafasi ya katibu mkuu wa NRM, alisema, “Nahusudu ujasiri wake na pia ninashuku busara zake.”
Kauli ya Meja Jenerali Otafire ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Utalii, inajenga taswira kwamba yeyote anayejitokeza kutaka kuchukua madaraka anayoshikilia Museveni anacheza na hatari.
Wengi wa viongozi wa ngazi ya juu wa NRM wanaogopa kama ukoma kufikiria kukabiliana na Rais Museveni katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa chama na rais wa nchi.
Na hiyo ndiyo sababu kubwa ya makada wengi wa NRM wakiwemo wanaoshika uwaziri hubaki kukabiliana wao kwa wao kugombea nafasi nyingine za uongozi ndani ya chama lakini siyo urais wa chama na taifa kwa kuona huo ni wadhifa mkubwa aliohulukiwa tu Rais Museveni.
Hali imekuwa hivyo miaka yote ya uchaguzi kiasi cha kuonekana kwamba nafasi hizo zibaki kushikwa na Museveni hadi pale atakapoamua mwenyewe kuachia ngazi.
Historia ya Kapteni Ruhinda
Historia ya Kapteni Ruhinda inaonyesha alijiunga na Jeshi la Uganda akiwa kijana sana na alipotimia umri wa miaka 17 alikuwa miongoni mwa kikundi cha wanajeshi vijana wa UPDF kabla ya kubadilishwa baadaye na kuitwa NRM.
Wakati Meja Jenerali Mugisha Muntu akiwa mkuu wa jeshi, iliamuliwa kwamba askari wote waliokuwa wanapaswa kusoma, warudi shule ili wapate kujiendeleza kielimu.
Ruhinda na wanajeshi wenzake vijana walitumia fursa hiyo kusoma hadi chuo kikuu. Mpaka alipokuwa anastaafu, alikuwa miongoni mwa maofisa waliopata elimu nzuri wakiwa wanajeshi. Yeye ana shahada ya heshima ya sheria na shahada ya uzamili (Sera za kiuchumi) aliyoipata Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.
Kapteni Ruhinda hadi hivi karibuni alikuwa miongoni mwa wasaidizi binafsi wa mdogo wa Rais Museveni, Jenerali Salim Saleh. Hata hivyo, maofisa wawili waandamizi walio karibu nao, wanasema kudhoofika kwa uhusiano wao kumetokana na suala la matumizi mabaya ya fedha.
Guma Rutahigwa na Amon Bagarukayo wa taasisi ya Pan-African Movement, Kapteni Ruhinda alikuwa katika kikundi kilichopewa Sh. 40 milioni za Uganda na Jenerali Saleh kuchapisha jarida la African lililokuwa mradi wa Umoja wa Vijana wa Afrika (PAYM) lakini mpaka leo, hawakueleza matumizi ya fedha hizo.
Kapteni Ruhinda ni mtu anayependa kusifiwa na kwa hivyo, uamuzi wake wa kutangaza kugombea urais dhidi ya Museveni, ni kwa ajili ya kutafuta umaarufu katika taifa, anasema Kabalega Isheruhemba aliyefanya kazi pamoja na Kapteni Ruhinda wakiwa PAYM.
Mwaka 2005, Kapteni Ruhinda na mkewe, mwanasheria Mary Mutesi, waligombea uongozi katika chama. Ruhinda aliyegombea nafasi mweka hazina, alishindwa na Ndaula Kawesa na mkewe alishindwa na Abbas Agaba nafasi ya mwenyekiti wa umoja wa vijana wa NRM.
Ruhinda aliwania uteuzi wa kugombea ubunge jimbo la Rubaga Kaskazini na kushindwa na Tom Kayongo ambaye katika uchaguzi alishindwa na Betty Namisango Kamya wa chama cha FDC.
Wagombea wengine walioshindana na Museveni ni Augustine Ruzindana wa FDC ambaye alipata kusema kwamba Museveni si mtu anayechukulia kirahisi ushindani.
Katika miaka ya 1990, inasemekana Museveni alishindana na Akena P’jok kuwania urais kupitia Chama cha UPM. Tangu aliposhika madaraka mwaka 1986, Museveni inaelezwa kuwa hajawahi kumtaka P’jok washirikiane kikazi.
Mwaka 2005, Dk. Elizabeth Nabatanzi aliazimia kugombea uenyekiti wa NRM dhidi ya Museveni, lakini alisitisha mpango wake na badala yake akaja kuteuliwa mmoja wa wasaidizi binafsi wa Museveni.
Wapo wanaoamini kuwa hatua ya Kapteni Ruhinda ni ya makusudi ya kumlaghai au kumtisha rais ili badala yake ampatie kazi ya kufanya katika kipindi hichi ambacho anaonekana hana kazi maalum.
Kulingana na Assimwe Steven wa Tume ya Uchaguzi ya NRM, Rais Museveni anajulikana kwa kushirikiana na washindani wake katika chama. Hatua yake ya kumteua Paul Ssemogerere na Joash Mayanja Nkanji – ambao walipambana katika uchaguzi mkuu wa 1980 – kuwa mawaziri miaka ya 1980 ni uthibitisho.
Vyama vinne vilishiriki uchaguzi huo mwaka 1980 ambavyo ni Uganda People’s Congress (UPC) cha Dk. Milton Obote, Democratic Party (DP) cha Ssemogerere, Congress Party (CP) cha Nkanji na UPM cha Museveni.