Msimpe Shibuda umuhimu wa bure


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
John Shibuda

SHIBUDA ananogesha mjadala barazani. Umepata kuona wapi, eti yeye awe mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), lakini meneja wake wa kampeni awe Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete?

Ukimsikia mtu anazungumza hivi, unajua huyu si mtoa hoja makini, bali mtu wa mzaha. CHADEMA ni jahazi la kuwavusha Watanzania toka tulipokwama hadi ng'ambo ya ahueni. Inabidi maneno ya utani ya Shibuda yapuuzwe.

Akipuuzwa, hata kama ametumwa, basi hata hicho alichotumwa hakitofanikiwa. Kimsingi yeye yuko kwenye chama cha demokrasia pana kuliko CCM na ni haki yake kutangaza kuwa anautaka urais…Hakuna mgogoro hapa. CHADEMA jadili mambo ya maana…

Uchumi unakwenda na maji. Elimu inadorora. Kilimo hakuna. Muungano umekwamishwa. Baraza la mawaziri kubwa mno. Hatuhitaji wakuu wa wilaya wasiochanguliwa na wananchi. Thamani ya sarafu yetu imeshuka. Hayo ni miongoni mwa masuala makubwa ya kujadili.

Shibuda yuko hivyohivyo hata alipokuwa CCM na hapaswi kupewa umuhimu asiokuwa nao; eti kumfukuza chama. Afukuzwe kwa kosa lipi…?

Tuwe wajanja kuliko wajanja uchwara ndani ya CCM. Wanaandika vichwa vya habari vya gazeti la UHURU: ‘CHADEMA kwafukuta moto’; eti shauri Shibuda kachekesha wana-CCM kwa kujitangaza mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA!

Hivi CHADEMA ni chama chepesi kiasi cha kupeperushwa na upepo wa Shibuda kujinadi urais 2015? Hapana ndugu zangu.

Mimi ni CCM-mfu; lakini sidhani Shibuda katumwa kazi maalumu ya kubomoa CHADEMA…Mwache Shibuda aendeleee na ndoto zake za alinacha; lakini bora yuko kwenye kambi ya wana-mabadiliko.

Dk. Lwaitama ni mwalimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Makala hii imechotwa kwenye mtandao wa “Mabadiliko.” Anapatikana kwa imeili: kerezesia_mukalugaisa@hotmail.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: