WANAHARAKATI nchini Swaziland wamemjia juu mmoja wa washauri wa Mfalme Mswati kwa maneno yake kwamba haogopi ugonjwa wa ukimwi akidai kiwango cha maambukizi kinakuzwa tu na watu wanaotaka misaada.
Mshauri huyo wa Mfalme, Prince Mangaliso, alizungumza na vyombo vya habari wiki iliyopita na kudai kwamba ukimwi ni ugonjwa wa kawaida unaokuzwa mno na wanaharakati wanaotengeneza fedha kwa njia hiyo.
“Ni kweli kwamba, kama ilivyo kwa nchi nyingine, kuna wagonjwa wa ukimwi hapa nchini kwetu. Hata hivyo, kiwango cha maambukizi kinachotangazwa si cha kweli na wanaotoa takwimu hizo wanazidisha kwa faida yao,” Mangaliso aliwaambia waandishi wa habari.
Mshauri huyo, ambaye anatoka katika ukoo wa kifalme wa Swaziland, alisema wengine wanaofaidika na ukuzaji huo wa takwimu zaidi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) ni makampuni ya kutengeneza na kuuza madawa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha maambukizi nchini hapa ni asilimia 26, ikiwa na maana katika kila watu wazima 100 unaokutana nao, watu 26 wanaishi na virusi vya ukimwi.
Prince Mangaliso aliwaambia waandishi wa habari kwamba kinachoendelea nchini humo kwa sasa ni kuwatisha badala ya kuwaelimisha wananchi juu ya ugonjwa huo, ingawa akasema yeye hana woga wowote dhidi ya ukimwi.
Hata hivyo, wanaharakati wa masuala ya ukimwi chini ya mwamvuli wa mtandao wa Swaziland For Positive Living, wamekemea matamshi hayo ya mshauri huyo kwa kuyaita “ya kipuuzi.”
Hlophe aliliambia Shirika la Utangazaji wa Uingereza (BBC) kwamba kufananisha mtu kwenda kuoga baada ya kufanya ngono na kutahiriwa ni kitu kisichoingia akilini.
“Kama kuna kitu ambacho kimedhihiri katika maelezo ya Mangaliso basi ni upuuzi wa kiwango cha juu. Tunadhani anatakiwa kuomba radhi raia wa Swaziland ambao wameathirika na ugonjwa huu kwa muda mrefu,” alisema mratibu wa mtandao huo Tengetile Hlophe.
Katika maelezo yake, Mangaliso alikejeli pia wale wanaodai kutahiri wanaume hupunguza maambukizi ya ukimwi, akisema madai hayo hayana tofauti na mtu anayekwenda kuoga mara baada ya kumaliza kufanya mapenzi ili ajiepushe na maambukizi.
Mama Hlophe alisema kejeli hiyo ya mwanaukoo huyo wa kifalme dhidi ya kutahiri wanaume ni kinyume kabisa na tafiti za kisayansi ambazo zimebaini pasipo shaka ya kuwa kitendo hicho kinapunguza maambukizi.
“Tafiti katika nchi kama Kenya, Uganda na Afrika Kusini zimeonyesha kwamba mtu aliyetahiriwa anapunguza uwezekano wa kuambukizwa virusi vya HIV vinavyoambukiza ukimwi kwa asilimia 60.
“Huyu mshauri ameonyesha wazi kwamba hajui ukimwi umeleta matatizo gani kwa nchi yetu. Asilimia 42.5 ya akina mama wajawazito wanaokwenda hospitalini nchini hapa huwa wanakutwa na HIV.
Hili ni tatizo na si mzaha,” alisema Hlophe. Prince Mangaliso ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri wa Rais, alifanya mazungumzo yake hayo na gazeti maarufu la nchini hapa liitwalo Times.
Ni katika mazungumzo yake hayo na gazeti hilo ndipo alipotamka kwamba yeye “haogopi ukimwi kwa namna yoyote ile.”
Mtawala wa nchi hiyo pekee inayoendeshwa kifalme barani Afrika, Mfalme Mswati, ana wake 13 na ni miongoni mwa watu wanaoandamwa sana na wanaharakati kwa vile tabia yake ya kuoa wanawake wengi inachochea kuenea kwa ukimwi.
