Mtandao wa Kikwete ndiyo gamba CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete

SEKTARIETI mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Wilson Mukama inaendelea kujiapiza kuwa sharti “…mafisadi waondoke ndani ya chama chetu.”

Naye mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete anaonekana kukubaliana na hoja kwamba ili kurejesha imani ya wananchi kwa chama chake, sharti mafisadi watoswe.

Waliotanjwa na makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa kwenye kikao cha Kamati Kuu mjini Dodoma, kuwa wamekuwa wakitajwa kuwa mafisadi, baada ya Kikwete kuonya kuwa hataki kumung’unya maneno, ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge.

Lowassa alikuwa waziri mkuu wa kwanza katika serikali ya Kikwete. Rostam amekuwa swahiba wake wa miaka mingi. Chenge alikuwa  miongoni mwa wanachama wa kundi la wanamtandao waliofanikisha ushindi wa Kikwete mwaka 2005.

Bali kuna fikra ya nyongeza, kwamba kutuhumu Rostam, Lowassa na Chenge kuidhoofisha CCM, hakuwezi kupata uzito bila maelezo kuwa Kikwete mwenyewe ni sehemu ya kundi hilo na sehemu ya matatizo yaliyopo ndani ya chama chake.

Kwanza, Kikwete aliyeingia madarakani kwa mbwembwe za kurejesha matumaini kwa wananchi, mpaka sasa hajaweza kutekeleza hata robo ya yale aliyoahidi. Hata kile alichoita “Maisha bora kwa kila Mtanzania,” ameshindwa kukitekeleza au hata kuonyesha njia ya kukifikia.

Baadhi ya wananchi waliamini, bila chembe ya shaka, kwamba baada ya mtangulizi wake Benjamin Mkapa kutanua wigo kati ya maskini na tajiri, Kikwete angeweza kuleta afueni kwa wananchi wa tabaka la kati na la chini. Siyo ilivyotokea kuwa.

Baadhi ya wenzake ndani ya chama wanasema, “…kushindwa kwa serikali kutekeleza matarajio ya wananchi kumetokana na Kikwete kutafuta ikulu kwa udi na uvumba, lakini huku akiwa hajui anakwenda ikulu kufanya nini.”
 
Matokeo yake, katika uchaguzi mkuu uliopita, katika namna ya kutafuta jinsi ya kujiokoa, Kikwete alilazimika kumwaga lundo la ahadi mpya, huku akijua fika kwamba mamia ya ahadi za mwaka 2005 hayajatekelezwa.

Katika baadhi ya maeneo, Kikwete aliahidi hata yale ambayo hayawezi kutekelezeka.

Kwa mfano, serikali haiwezi kujenga uwanja mpya wa ndege mjini Bukoba na ikaweza kufanya hivyo wilayani Misenyi, wakati kwa zaidi ya miaka saba imeshindwa kumalizia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mbeya.

Aidha, serikali haiwezi kuboresha usafiri majini kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kununua meli mpya ya abiria, wakati haijaweza kununua meli kama hiyo, tangu mwaka 1996, kwa matumizi katika Ziwa Viktoria.

Haya yana maana gani? Ni kwamba aliyepigania kuingia ikulu kwa muda wa miaka kumi; akifanya maandalizi na kampeni kamambe, hakuwa amefanya utafiti wa nini taifa linahitaji.

Ndiyo maana pamoja na kukaa madarakani kwa miaka mitano mfululizo sasa, bado anasema hafahamu kwa nini wananchi wake ni masikini.

Pili, kudhhofika kwa CCM kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na makundi ya wanamtandao yaliyotumika kumuingiza yeye madarakani.

Makundi haya yanayodaiwa kuratibiwa na Rostam Aziz, yanatuhumiwa kuvuruga chama kwa kufanya kazi ya kuchafua washindani wa Kikwete ndani chama chake.

Miongoni mwa waliochafuliwa na wanamtandao, ni Dk. Salim Ahmed Salim, John Malecela, Profesa Mark Mwandosya na Fredrick Sumaye.

Hakuna mahali popote panapoonyesha kuwa Kikwete alichukizwa na hatua hii ya kuchafua washindani wake wa kisiasa. Kinachofahamika machoni mwa wengi, ni hatua ya Kikwete ya kuwapa kazi wale wanaotuhumiwa kushiriki kuchafua wenzake.

Hata kumuondoa Philip Mangula katika nafasi ya katibu mkuu, mara baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha CCM hapa ilipo.

Nafasi ya Mangula ilirithiwa na Yusuph Makamba ambaye haikuchukua muda akaanza kutuhumiwa kwa kukigawa chama kwa msingi wa “huyo hakuwa mwenzetu;” kupandikiza mbegu ya chuki miongoni mwa wanachama na viongozi; kushindwa kusimamia maadili ya chama na kujenga makundi miongoni mwa viongozi na wanachama.

Yote haya yalifanyika kwa kuwa Kikwete alijiandaa kushika madaraka ya dola na chama, lakini hakuwa amejiandaa katika kutafuta tiba ya mipasuko aliyoitengeneza.

Uamuzi wake wa kujitenga na wanamtandao miaka mitatu baada ya kuingia madarakani, haukusaidia kuvunja makundi yaliyooteshwa. Tathimini ya haraka inaonyesha kuwa mkakati huo, haukumsaidia kujenga chama na kupata utulivu ndani ya serikali.

Hii ni kwa sababu, kusambaratika kwa mtandao kulikwenda sambasamba na kujiimarisha kwa kundi jipya linalojulikana kama “Vision 2015.”

Miongoni mwa wanachama wapya wa kundi hili, ni waliokuwa wafuasi wake katika uchaguzi wa mwaka 2005 ambao sasa wameungana na  waliokuwa washindani wake katika vita vya kuwania urais katika uchaguzi ujao.

Tatu, uamuzi wa Kikwete wa kutaka kuwaondoa watuhumiwa wakuu wa ufisadi ndani ya chama chake sasa, badala ya kushindwa kufanya hivyo miaka miwili iliyopita, kutazidi kukidhoofisha chama na Kikwete mwenyewe.

Hii ni kwa sababu, hatua ya kuwaondoa akina Rostam, Lowassa na Chenge katika vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), hakuwezi kutajwa kuwa mafanikio ya kukitakasa chama.

Kama kweli Kikwete amedhamiria kusafisha chama, sharti awafukuze watuhumiwa wote wa ufisadi kutoka chama hicho na wote wanaotuhumiwa kukivuruga.

Vilevile, ni lazima wote wanaotuhumiwa ufisadi wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma dhidi yao. Hii ni kwa kuwa, tuhuma za ufisadi ni juu ya hujuma kwa serikali na umma wa taifa hili; na siyo CCM peke yake.

Kuwaondoa watuhumiwa katika vikao vya maamuzi vya chama, lakini wakabaki na nafasi zao za ubunge, hakuwezi kutakasa chama.

Kwa mujibu wa katiba ya CCM, wabunge wa chama hicho, ni wajumbe wa mkutano mkuu wa chama chao. Mkutano mkuu wa chama ndiyo unaofanya kazi ya kuchagua wajumbe wa NEC; ndiko sera za chama, katiba ya chama, mwelekeo wa chama na uhai wa chama, hujadiliwa na kuamuliwa.

Je, Kikwete yuko tayari hatma ya chama chake, na huenda hata yake, iamuliwe na watuhumiwa wa ufisadi?

Mkutano mkuu wa chama ndiyo unaochagua mgombea urais wa Muungano na unaoidhinisha mgombea urais wa Zanzibar.

Wananchi wanajua kuwa kuondoa “mafisadi” katika vikao vya NEC na CC, bado kutawawezesha kushiriki katika uchaguzi wa mgombea urais wa Muungano na yule wa Zanzibar. Je, Kikwete ameliona hilo?

Lakini kuna hili pia. Watuhumiwa wote watatu ni wabunge wa Bunge la Muungano; Bunge ndilo lenye mamlaka ya kusimamia fedha za umma; ndiko sheria za nchi zinatungwa na ndiko, kwa mujibu wa katiba, wananchi wanasimamia serikali yao.

Ndani ya Bunge, miswada ya serikali na mipango ya bajeti ya serikali ndiko hupitishwa. Katika kipindi hiki cha kwanza cha miaka miwili cha Bunge la kumi, Kamati ya uongozi ya Bunge ambayo inaongozwa na spika Anne Makinda, mmoja wa watuhumiwa – Lowassa – ni mjumbe wa kamati hiyo.

Lowassa ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, mambo ya nje, ulinzi na usalama.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kanuni ya 115, sehemu ya 3 (a), kazi ya kamati ya uongozi, ni kumshauri spika kuhusu mambo yote yanayohusu shughuli za Bunge; na kuweka utaratibu utakaorahisisha maendeleo ya shughuli za Bunge au za kamati ya Bunge.

Si hivyo tu, Kifungu cha 3 (b) kinaeleza kazi za kamati ya uongozi, kuwa ni pamoja na “kupokea hoja zenye maslahi kwa taifa zinazojitokeza kwenye kamati za Bunge na kisekta wakati wa kupitia bajeti za wizara na kuishauri serikali kuhusu hatua mwafaka za kuchukua kabla ya hotuba ya bajeti kusomwa bungeni.”

Hapa Kikwete anataka kusema kuwa Chenge, Rostam na Lowassa, wameharibu taswira ya chama mbele ya wananchi, lakini wamekuwa watakatifu bungeni?

Kwamba watuhumiwa wa ufisadi wanaweza kushauri spika katika kuendesha shughuli za Bunge, bila kuathiri hadhi ya Bunge, serikali na chama chake. Anaweza kutuhumiwa kuliibia taifa, lakini akapewa kazi ya kusimamia hoja zenye maslahi ya taifa. Huu ni uabunwasi.

Nani anaweza kuamini Kikwete, kwamba Chenge anaweza kusimamia maslahi ya taifa pale Bunge linapotaka kujadili suala la ununuzi wa rada, mikataba ya madini au wizi wa kampuni ya Meremeta?

Kila mbunge wa Bunge la Muungano, ni diwani katika halmashauri ya wilaya, miji na manispaa anakotoka. Ndani ya halmashauri hizo, ndiko serikali inakopeleka miradi ya mabilioni ya shilingi.

Je, Kikwete anaweza kusema ni sahihi kufukuza mafisadi katika chama, lakini wakaendelea kusimamia fedha za umma katika halmashauri za wilaya?

Vyovyote itakavyokuwa, kuwaondoa watuhumiwa wa ufisadi katika chama, lakini wakabakishwa kwenye Bunge, hakuwezi kukisaidia chama cha Kikwete wala Kikwete mwenyewe.

Badala yake, hatua hiyo itasaidia wananchi kufahamu kuwa ndani ya CCM hakuna mwenye dhamira ya kupambana na ufisadi; hiki kinachofanyika sasa, inawezekana kuwa vita vya madaraka.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: