Mtei: Kazi shambani zimeniepushia kitambi


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 02 December 2009

Printer-friendly version
Edwin Mtei

NINAELEKEA kwenye makazi ya mwanasiasa mkongwe, Edwin Mtei. Ninatokea mjini Arusha. Ameniarifu kuwa anaishi Tengeru, eneo linaloitwa Chama. Kwamba, kielelezo kikubwa unapoingia kwake ni bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), inayopepea kwenye lango kuu.

Ninashuka eneo la Chama na kutembea meta karibu 100 hivi. Mbele ninakutana na kibanda cha mlinzi ambaye ameketi nje. Hapa ndipo pana lango kuu linaloingia kwenye makazi yake, yaliyozungukwa na shamba la mibuni.

Kutokana na kimya kingi na kuwapo miti mingi, naweza kuwaona nguchiro wengi wakiruka kwenye mibuni na miti mingine. Ni ishara kuwa mazingira ya hapa yametunzwa.

Ndani ya shamba kuna tanki kubwa na kisima kirefu cha maji. Baada ya hatua chache ndipo ninazikuta nyumba zake ambazo zimezungukwa na shamba hilo, mabanda ya mifugo, wakiwamo ng’ombe, kuku na nguruwe.

Nje ya nyumba ya upande ninaotokea, ninamkuta Mtei akiwa ameketi. Ni saa 5.15 asubuhi ya Jumapili, 9 Agosti, 2009. Ameshika kalamu mbili za wino, daftari na hotuba zake mbili; moja ikiwa ni ile aliyoitoa wakati Benki Kuu (BoT), ilipotimiza miaka 43 na nyingine ni aliyoitoa wakati wa maonyesho ya Nane Nane Kanda ya Kaskazini, mwaka huu, mjini Arusha.

Baada ya mazungumzo mafupi,ananitembeza shambani kwake. Hapa ndipo nayaona mabanda yenye mifugo hiyo, mashine za kuchambua na kusafisha kahawa, na kahawa iliyoanikwa kwenye vichanja.

Kuna bomba kubwa la maji ambayo yanatumika kusafishia kahawa na mengine kuingia kwenye bwawa la samaki, lililopo kwenye shamba hili.

Shamba lina mibuni ya kawaida na chotara. Mtei ananiambia kuwa aina hii ya chotara ni bora na huzaa sana. “Aina hii mpya ya mibuni nilianza kuipanda hapa shambani miaka sita iliyopita. Mti mmoja unaweza kuzaa kahawa hadi kilo nne.”

Kuna zao la vanila alilolinunua kutoka Bukoba, Kagera na pia kuna pilipili manga ambazo hustawi shambani humu.

“Pamoja na mazao yote yaliyopo hivi sasa, bado ninafuga hapa shambani. Kuna ng’ombe ambao ni mradi wa mama (mkewe), kuna kuku ambao ni mradi wa mtoto wangu na mkewe na mimi ninasimamia mradi wa nguruwe,” anasema Mtei.

Kwa hakika, katika eneo hili kila mmoja anafanya kazi zake na mahali pake. Wapo wanaolisha nguruwe, wapo wanaonywesha ng’ombe maji na wapo wanaofanya kazi zao kwenye mabanda ya kuku.

Kwenye mradi wake wa nguruwe, Mtei ananieleza kuwa mabanda yamegawanyika katika sehemu tatu: Sehemu yenye nguruwe wenye watoto wanaonyonya, sehemu ya nguruwe wanaopandishwa na ile ya wale wanaokua.

Mtei anajivunia uwezo wake wa kufanya kazi za shamba kwa muda mrefu bila kuchoka na kwamba kufanya hivyo kunamfanya asiwe maumbile ya hatari kwa afya yake. “Sioti kitambi kwa kuwa ninafanya kazi na kutembea sana shambani mwangu.”

Shamba hili lina ukubwa wa eka 50, ambalo alilinunua mwaka 1980. Aliamua kuendesha shughuli zake katika shamba hilo baada ya kujiuzulu wadhifa wa waziri wa fedha wakati huo Rais akiwa ni Mwalimu Julius Nyerere.

Aliamua kujiuzulu mara baada ya kupendekeza kwa serikali ya Mwalimu kwamba Tanzania ifuate masharti ya Shirila la Fedha duniani (IMF) na Benki ya Dunia, kutokana na uchumi kudorora.

Kutokana na mapendekezo yake kupingwa na Mwalimu Nyerere, ndipo Mtei alipoamua kuachia ngazi na kwenda kuishi Tengeru.

“Nilikuja hapa shambani baada ya kubadilishana na bwana mmoja shamba hili na nyumba yangu ya Dar es Salaam. Yeye aliipenda nyumba yangu na mimi nikaamua kuja hapa kuanza maisha mapya.

“Kwa hiyo, kufanya kazi na kutembea humu shambani hakuwezi kuniotesha kitambi. Mimi bado ninashughulika na kilimo cha kahawa, lakini majirani zangu wameng’oa mibuni na kujihusisha na kilimo cha mazao mengine.

“Mimi ninaitwa a farmer in action (mkulima kwa vitendo). Kwa miaka mitatu sasa tumekuwa tuking’oa mibuni ya zamani na kuipanda ile ya kisasa.

“Lazima nikiri kuwa uzee ndio kikwazo kwangu ili kupanua kilimo changu. Ningekuwa bado kijana ningekwenda mkoani Rukwa, Kigoma au kusini kutafuta mashamba makubwa ya kahawa,” anasema Mtei.

Mwanasiasa huyo mkongwe amekuwa akiwatumia majirani ili kuchuma kahawa. Kwa siku wanaweza kuhudhuria wachumaji hadi 100.

Mzee Mtei, akiwa Katibu Mkuu wa wizara ya fedha mwaka 1965, aliagizwa na Mwalimu Nyerere aanze mchakato wa maandalizi ya kuwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Maandalizi hayo yalikuwa ni kutafuta wataalam, kusanifu sarafu mpya na kutafuta mchapishaji.

“Sheria ya BoT ilipitishwa na Bunge Desemba 1965 na kuanza kutekelezwa rasmi 6 Januari, 1966, tulipoanza kupangisha ofisi za kufanyia kazi na nyumba za waajiriwa wetu kama taasisi inayojitegemea.

“Kutoa sarafu ya kitaifa na BoT kuwa ni benki ya mabenki na serikali, kulizinduliwa tarehe 14 Juni, 1966 wakati Rais Julius Nyerere alipokabidhiwa noti za kwanza…Umma, mawaziri na wabunge wote walihudhuria sherehe hizo kwani kesho yake ilikuwa ni Bunge la Bajeti linaanza kikao,” anasema Mtei.

Mtei alikabidhi kiti cha Gavana kwa Charles Nyirabu 23 Aprili, 1974, alipoondoka kwenda Arusha kuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Uhusiano wangu na BoT ulikuwa wa karibu zaidi mwaka 1977 nilipoteuliwa kuwa waziri wa fedha…Hata baada ya kuacha uwaziri, nilikuwa na mawasiliano ya karibu na BoT nilipoteuliwa kwenda IMF, wadhifa niliokuwa nao kati ya Novemba 1982 na Novemba 1986,” anasema Mtei.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: