Mtihani kwa TFF, Wambura


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

KELELE zinazopigwa na aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Michael Richard Wambura zimenikumbusha kitendawili cha utotoni kisemacho, “linapokuja kwetu linatanguliza kelele”.

Majibu ni mengi. Zamani jibu lilikuwa radi, kwamba mara nyingi kabla ya mvua kuanza kunyesha radi hupiga sana na wakati mwingine inaweza isinyeshe. Siku hizi, jibu linaweza kuwa gari au chombo chochote cha moto kama pikipiki, treni au ndege.

Ngurumo za vyombo hivyo vya usafiri huwa ni taarifa kwamba ama basi, au lori au ndege au pikipiki inakuja au inapita.

Kila radi ikipiga au gari au ndege ikipita huacha gumzo kubwa. Hawa watalaani, wale watasifu na kule watalia imeacha vifo.

Lakini jambo moja muhimu ni kwamba ngurumo za radi zikianza au yakisikika makelele ya basi watu huanza kujiandaa. Kama ni radi, watu huanza kuondoa nguo na wao wenyewe kuingia ndani ili wasinyeshewe au baadhi huchukua miavuli.

Maelezo haya yote yanakusudia kueleza jambo moja kuhusu Wambura, kwamba kwa makeke yake, kampeni za wazi na shutuma na dhidi ya vyombo vya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambavyo kimsingi ndivyo vyenye maamuzi ya mwisho agombee nafasi ya uongozi au la.

Wambura ni kama anacheza mchezo wa kitoto “…mkinipiga mtakuwa mnanionea, na mkiniacha basi mtakuwa mnaniogopa.”

Upande unaoambiwa “mtakuwa mmenigopa” ukiona hiyo ni dhihaka mbaya huamua kumvaa wanayemwona ni mchokozi na hapo ugomvi huanza. Ole wake kama ameanzisha ugomvi hakuna wakubwa wa kukusaidia!

Wambura anapompa siku saba, mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratius Lyatto kuomba radhi na asipofanya hivyo atamfikisha kortini ni mtindo uleule “…mkinipiga mmenionea, mkiniacha mnaniogopa.”

Anapotema ndimi za moto, Wambura anategemea nini au anasaidiwa na nini ili ashinde vita aliyoianzisha? Kwa sheria za nchi Wambura ana haki ya kugombea TFF.

Lakini ajue wakati anajitangazia usafi katika vyombo vya habari na kwamba katiba ya nchi inampa haki kuwania nafasi yoyote anayotaka, hao anaowaona kuwa ni wabaya wake wanatumia kanuni za soka kumdhibiti.

Hapo ndipo Wambura hajatofautisha na hajapatafutia dawa ya kudumu. Mahakama za nchi zinaweza kusema Wambura hana kosa kisheria na zinaweza kumpa haki ya kupinga jina lake likiondolewa. Mwisho wake ni nini?

Kamati ya uchaguzi ikiondoa jina lake kwa sababu yoyote ile, atakuwa amesukumwa kutumia vyombo vya kisheria ndani ya mfumo wa soka anaouponda na si nje ya hapo.

Mahakama za kisheria haziwezi kuingilia masuala ya chaguzi za vyama vya soka. Huu ndio ukiritimba ambao Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeweka.

Mfano, hivi karibuni serikali ya Misri iliwaadhibu kwa kuwafuta kazi viongozi wote wa soka kwa kuzembea kuweka ulinzi wa kutosha hadi watu wapatao 74 walikufa katika vurugu kati ya mashabiki wa klabu ya Al Masry na Al Ahly. Fifa ikaonya kwamba Misri itafungiwa ikitekeleza adhabu hiyo.

Yako wapi makeke ya Mohammed bin Hammam wa Qatar aliyetaka kumng’oa Sepp Blatter? Nani anamsikia tena Lennart Johansson wa UEFA?

Viongozi wa TFF nao ni binadamu wana udhaifu wao, lakini kama walivyo binadamu wote duniani hawawezi kuona wanadhalilishwa wakabaki kimya. Mdau yeyote wa soka atake asitake, aheshimu kanuni asiheshimu, akubali taratibu asikubali; TFF ama kwa utashi au kwa sheria ndio wenye funguo fulani ni msafi agombee na fulani hana udhu asigombee.

Awali mbaya wa Wambura alikuwa Katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah lakini sasa mgomvi wake ni Lyatto.

Hapa Wambura ni kama anasema, “…mkikata jina langu mmenionea, mkiniacha mmeniogopa.” Katika hali hii, Wambura anataka TFF wafanyeje?

Bila shaka watapanua mvutano huu, watafunua mambo mengine ambayo kimsingi hatupaswi kujua kumhusu, lakini dakika za mwisho kamati ya uchaguzi ndiyo itasema imejiridhisha Wambura ana sifa au hana sifa.

TFF ikisema Wambura hana sifa kutokana na mlolongo wa tuhuma, atakimbilia mahakamani kudai haki yake. Hapo TFF watakuwa wamemsukumiza tena afanye kosa kama lile alilofanya alipowania uongozi katika klabu ya Simba. Nina uhakika itakuwa hivyo.

Nyoka hapigwi mkiani ila kichwani. Wambura ataruka, atashutumu lakini asiporudi chini akakaa akatumia vyombo halali vya soka – TFF na Mahakama ya Usuluhishi katika Michezo (CAS) – atakuwa amefika mwisho wa barabara ya soka.

Mdau yeyote anaweza kuandika makala kupinga makala hii ili kuonyesha Wambura ana nafasi nje ya taratibu zilizopo. Ukweli bila kusafishwa na vyombo halali vya soka au hata baadhi ya watendaji kuondoka, sioni mtu wa kuogopa kukata jina la Wambura Desemba 2012 kutokana na mitego aliyojitegea.

0
No votes yet