Mtihani kwa wanaofukuzia urais 2015


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KATIKATI ya mauzauza ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bungeni Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha alipopolewa kwa mawe eneo la Tunduma, mkoani Mbeya.

Polisi Namba Moja huyo alionja ‘joto ya jiwe’ kutokana na kile wananchi wa Tunduma walichodai alifanya matumizi mabaya ya mali za umma kwa kutumia magari ya serikali kwa shughuli za kichama.

Vijana waliojaa jazba kwa kitendo hicho cha waziri, walijipanga barabarani wakimzomea na kupiga miluzi huku wengine wakirusha mawe kabla ya kudhibitiwa na polisi waliokuwa wanasaidiana na walinzi wa CCM, maarufu kwa jina la Green Guard.

Mmoja wa waliokamatwa na aliyejitambulisha kwa jina la Yusuf Haonga alihoji,  “Hawa wanatuchanganya. Inakuwaje wanatumia raslimali za nchi kwa kazi za chama? Pesa hizo si zingetumika kuhudumia wagonjwa waliolala hospitalini badala yake wanazitumia wao?”

Aliongeza kuwa kitendo cha waziri akiwa mtumishi wa umma kufanya ziara ya kichama huku akitumia magari ya serikali kiliwakera na waliamua kumtupia mawe ili kutoa onyo kwa viongozi wengine wa serikali.

Maelezo haya yatufikirishe tupate kujua uelewa wa wananchi sasa kwa mambo mbalimbali yanayowagusa. Baadhi ya viongozi wetu bado wamegandamana na mawazo yaleyale ya kizamani.

Wananchi wa sasa wanajua kuwa mali ya serikali ni mali ya nchi na ni mali ya wananchi wote.

Wanajua pia kuwa mali ya chama ni mali binafsi ya chama na wanachama pekee. Inapotokea kiongozi halielewi hili kwa wakati huu wa sasa inasikitisha sana!

Wamekataa viongozi wa umma kutumia mali za wote kwa maslahi ya kundi fulani. Wamesema hili liwe fundisho kwa viongozi wengine (wazito kusoma alama za nyakati). Kuwakamata na kuwatia ndani siyo suluhisho. Huko ni kuanzisha mapambano dhidi ya wananchi.

Pamoja na kwamba jambo walilofanya vijana hao ni ovu na halifai kwa viwango vyovyote vile, ni ujumbe kwa watawala kwamba watenganishe shughuli za serikali na za chama.

Tatizo hili ni sugu na hata wakati wa uchaguzi mkuu, CCM ilitumia magari ya serikali kwa kubadili namba zisomeke kuwa magari ya watu binafsi. Kama CCM bado haitaki kufunguka, watawakamata na kuwafunga, lakini watawafunga wangapi?

Kutoka Nyamongo, kijana Daniel Masimbe wa kijiji cha Nyarwana kata ya Kibasuka alipigwa risasi na polisi katika koromeo zilizotokea mgongoni na kumuua palepale.

Inadaiwa kwamba alikuwa mmoja wa watu zaidi ya 100 waliovamia mgodi wa dhahabu wa North Mara eneo ambalo kwa miaka mingi walikuwa wanachimba dhahabu kabla ya kuondolewa na kupewa wawekezaji.

Mgogoro huu ni wa muda mrefu, lakini serikali ya CCM haitaki kulitafutia ufumbuzi wa kudumu badala yake inafurahia vijana wakiuawa kila mara.

Hatuwezi kukubali viongozi wetu waendelee kupigwa mawe wala hatuwezi kukubali kuona watu fulani wanataka kuendesha nchi kwa kutumia vurugu. Lakini pia hatuwezi kuwavumilia viongozi wanaowalazimisha wananchi kuwapopoa kwa mawe kwa vitendo vyao vya kifisadi.

Wote tunataka amani. Palipo na dhuluma amani haipatikani. Hatuwezi kukubali watu wachukue sheria mkononi na vivyo hivyo hatuwezi kukubali viongozi wasiotaka mabadiliko wachukue hilo kama kisingizio ili waendelee kuwa kero kwa wananchi.

Tuendako, lazima uwepo utaratibu au mahali ambapo wananchi wanaweza kumshtaki au kumwajibisha kiongozi aliyekiuka maadili. Wangekuwa na mahali pa kumshtaki, Tunduma wangemshtaki Waziri Nahodha, lakini hakuna utaratibu huo.

Japo wanajua vizuri kuwa yule ndiye mwenye mamlaka yote ya mabomu ya machozi na bunduki zote za kuulia watu waliamua, liwalo na liwe! Hii ni nguvu ya umma ambayo ikitumika vizuri ina manufaa kwa maendeleo lakini ikitumiwa vibaya inaweza kuwa na madhara.

Tukishakuielewa hali hii ndipo tunaweza kujiuliza, je, wanaoufukuzia urais sasa  wana ubavu wa kuwavuruga wananchi wa leo?

Kuna viongozi wanaotaka kulazimisha ionekane kama ni dhambi kwa mtu kuusaka urais sasa. Wote wanaotajwa kuufukuzia urais ni wanachama wa CCM. Na wanaopiga kelele ni wanachama wa CCM.

Mashaka yanazidi kuona kwamba viongozi wa CCM ndio wanawaogopa kina Emmanuel Nchimbi, Bernard Membe, Samwel Sitta, Fredrick Sumaye, Edward Lowassa na Asha Rose Migiro wanaotajwatwaja katika kinyang’anyiro cha urais kuliko hata Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA ambaye alikuwa tishio katika uchaguzi mkuu uliopita.

Tukirejea hotuba ya Spika wa Bunge Anne Makinda aliyelitangazia Taifa pale Karimjee wakati wa kuuaga mwili wa hayati Regia Mtemi kuwa ‘ndiye alishinda kiti cha ubunge katika jimbo la Kilombero’, CCM hawaoni kwamba kauli hiyo inaimarisha habari zilizozagaa kuwa Dk. Slaa ndiye aliyeibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu uliopita, lakini hakutangazwa?

Regia pia hakutangazwa. Ushindi wake umetangazwa baada ya kifo chake! Mnadhani wananchi watakaa na fundo mioyoni mwao mpaka lini? Katika hili anayechochea vurugu nchini ni nani?

Rais ajaye lazima awe chaguo la wananchi. Anayedhani anaweza kuwa rais wetu ajitokeze hadharani sasa watu wapate muda wa kutosha kumpima. Ajulikane mapema watu wamjue wasirudie makosa. Hakuna mwenye mamlaka ya kukataza hili.

Watu wanataka kumchonga mtu wao wanayemtaka halafu waje wawaletee wananchi dakika za mwisho kwa kuwashtukiza. Kama wanaotajwa wanafaa au hawafai wa kuamua ni wananchi hapana mwingine!

Nijuavyo CCM kama chama waliisha upoteza utaratibu wa kumpata mgombea urais kwa njia iliyo wazi. Kundi la wanamtandao lilipoipindua CCM mwaka 2005 liliharibu utaratibu mzima uliokuwapo. Ndiyo maana kila mtu sasa anajaribu kutumia njia anayoiona.

Kama havunji sheria mwacheni, kuna ubaya gani? Kinachotumika hapa ni nguvu binafsi za anayeutaka urais. Hii ndiyo imezalisha makundi mengi ndani ya chama. Kukosekana kwa uongozi imara wa mwenyekiti wa chama kumewafanya wananchi wa leo kuiona CCM kiutawala kama mufilisi. Waliomo ndani chini ya uongozi huu ni sawa na watu waishio ndani ya jumba bovu, kuangukiwa si ajabu!

Baada ya sekretarieti chini ya mtendaji Wilson Mukama kuja na dhana mufulisi ya gamba katikati ya kero lukuki zinazowakabili wananchi, wamepoteza mvuto na kukifanya chama kupoteza mwelekeo. Sasa wanatokeza watu kutaka kuweka mambo sawa.

Lakini nao badala ya kutumbua usaha kwa kurekebisha uongozi ulioshindwa kudhibiti wanachama wake, wao wanawageukia wanachama ambao tayari wamegawanyika. Ulizaneni ndani ya chama busara iliyotumika kufanya sherehe za mabilioni ya shilingi eti kutimiza miaka 35 katikati ya vifo vingi vya wananchi mahospitalini kutokana na mgomo wa madaktari!

Kumbe hela za tafrija zipo. Hotuba ndefu lakini hakuna hata neno moja linaloonyesha mtu anaumia kwa vifo vinavyotokana na mgomo!

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alituambia, “Ubaya wenu nyinyi mambo ya msingi mnayaacha, mnachukua mambo ya kijinga.” CCM wamevurugana, sasa wasituvurugie nchi!

0713334239, ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: