Mufti epusha jangwa BAKWATA


Yusuph Katimba's picture

Na Yusuph Katimba - Imechapwa 12 August 2008

Printer-friendly version

YAPATA mwaka mmoja sasa tangu mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Issa Simba aanze kulalamikiwa kwa kutumia vibaya madaraka na kusababisha hasara kubwa kwa mali za Waislam pamoja na kukomaa kwa makundi miongoni mwa waumini.

Kamati ya Waislam inayofahamika kwa jina la Kamati ya Kuokoa Mali za Waislam, ikiongozwa na katibu wake, Khalifa Khamis, imekuwa ikimlalamikia mufti kwamba uongozi wake unagubikwa na usiri mkubwa na kwamba mali za Waislam hazisimamiwi vizuri.

Kamati hiyo inadai kuwa kutokana na uzembe wa muda mrefu wa Baraza Kuu la Waislam Tanzanzia (BAKWATA), mali za waislam zimekuwa zikipotea.

Panapofuka moshi kuna moto. Lakini mufti amekuwa kimya; bila kujibu hoja wala madai. Jambo hili linaendelea kuleta wasiswasi katika baraza hilo na kuendelea kuibua maswali mengi.

Mambo yanayolalamikiwa na kamati ya kuokoa mali za waislam yana mantiki na manufaa makubwa, si kwa waislam pekee yao bali kwa taifa zima. Kuwepo kwa matumizi sahihi ya mali kungewezesha BAKWATA kusimama na kuendesha miradi yake huku ikitoa ajira kwa jamii.

BAKWATA ni chombo cha kuwaunganisha waislam. Mfarakano katika taasisi hiyo na kuota kwa makundi nchini kunaashiria mgawanyiko; jambo ambalo litapunguza ushirikiano na kuchochea chuki miongoni mwa waislam.

Leo hii waislam wanataka kujua matumizi na mapato ya umoja huu. Wanataka kujua kinachotokana na mali za waislam kama majengo na viwanja.

Wengine wanataka kujua zaidi juu ya mgawanyo wa madaraka, vigezo vya wanaoshika madaraka hayo; mipango ya muda mfupi na mrefu na maendeleo ya taasisi hiyo kwa ujumla.

Haya hayapaswi kuwa maswali magumu kwa mufti na wasaidizi wake. Inatarajiwa kuwa majibu yakipatikana hapatakuwa na mivutano zaidi bali kusikilizana na kuleta maendeleo katika taasisi hiyo.

Mufti anapaswa kutoa majibu hayo kwa kuwa ni haki ya waislamu kujua na kutambua namna taasisi hiyo inavyoendeshwa. BAKWATA inapaswa kukata kiu ya waislam wanaolitakia baraza hilo maendeleo yanayoenda sambamba na mabadiliko duniani.

Ilivyo sasa, kinachoelekea kuwa mfarakano kinatokana na usiri ulioghubika shughuli za BAKWATA. Kuendelea kwa mfarakano kunaweza kusababisha kupotea kwa amani miongoni mwa waislam na nchi nzima.

Kwa mfano, kutopatikana kwa taarifa juu ya viwanja vya waislam na misikiti utaendelea kuwa kero kwa wanaotaka kujua asili yake na hatua zinazochukuliwa.

Kutochukuliwa hatua dhidi ya upoteaji endelevu wa mali za waislam kutaendelea kupanda mbegu ya mashaka miongoni mwa waumini. Nalo ni tatizo linalohitaji majibu haraka.

Kuendelea kutilia mashaka watu wanaohoji upotevu wa mali na hata taratibu na kanuni za ajira katika BAKWATA, kutaendelea na hata kukuza mfarakano. Hilo nalo pia linahitaji majibu ya haraka.

Tayari kuna taarifa za kufanyika maandamano kupinga mufti na hatua alizochukua hivi karibuni za kuwavua madaraka baadhi ya masheikh.

Maandamano haya hayataisha hivihivi tu. Yatapanua ufa. Ili kuziba ufa kabla haujapanuka, yanahitajika majibu kwa kile ambacho wengi wanauliza na wanataka kujua. Hii siyo kazi ngumu kwa mufti na wasaidizi wake.

Sasa kumetokea wanaosema mufti ajiuzulu. Yeye hataki kujiuzulu. Kuna wanaomuunga mkono. Kwao, Shinyanga, tayari masheikh wamesema hapaswi kujiuzulu. Haya nayo yanapanua ufa. Majibu yanahitajika.

Madhehebu ya dini ni sehemu nyingine na muhimu ya utawala. Kilichowashinda watawala na mabavu yao hupindwa kwa imani za waumini na viongozi wao.

Kwa msingi huu, BAKWATA na viongozi wake hawapaswi kufarakana na kusubiri kupatanishwa na serikali. Hekima ya waumini ianze kutawala sasa.

Mufti anayo majibu kwa yote yanayoulizwa. Akipewa muda aweza kutoa majibu. Lakini akichelewa kuyatoa aweza kupoteza fursa mwanana ya kuunganisha waumini waliomweka madarakani.

0
No votes yet