Mukama amdanganya Kikwete


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Wilson Mukama

RIPOTI ya “kikosi kazi” kilichoundwa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete kutathmini uchaguzi mkuu uliopita, imejaa udanganyifu.

Kikosi kazi kiliongozwa na Wilson Mukama ambaye hivi sasa ni katibu mkuu wa CCM na Profesa Eginald Mihanjo wa Chuo Kikuu cha St. Jones cha Dodoma.

  MwanaHALISI limegundua kuwa miongoni mwa yaliyodanganywa ni kuhusu umiliki wa mtandao mashuhuri nchini wa Jamii Forum (JF).

Inaelezwa kwamba ripoti ya Mukama inautaja mtandao wa Jamii Forum kuwa unaundwa na vijana kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Lakini uchunguzi wa MwanaHALISI unaonyesha kuwa mtandao huo hauna uhusiano wowote na Chadema.

Kwa mujibu wa nyaraka kutoka Wakala wa Serikali wa Biashara na Leseni (BRELA), JF inamilikiwa na kampuni ya Jamii Media Company Limited iliyosajiliwa 2 Julai 2008 na kupata hati Na. 66333.

Wanahisa wa kampuni hiyo, ni Steven Diallo, mwenye hisa 40, Maxence Melo mwenye hisa 250, Mike Mushi, mwenye hisa 250, Dickson Charles, hisa 40 na Lameck Mussa mwenye hisa 40.

Wanahisa wengine, ni mwandishi wa habari Mbaraka Islam, mwenye hisa 100 na William Malecela, mtoto wa makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela, mwenye hisa 40. 

Steve Diallo mtoto wa mjumbe wa NEC na mbunge wa zamani wa Ilemela (CCM), Anthony Diallo.

Rais Kikwete aliunda kikosi kazi muda mfupi baada ya kutoa hotuba ya kuadhimisha miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma.

Kikosi kilipewa jukumu la kufanya utafiti juu ya mambo ambayo yanaigharimu CCM na ambayo yalisababisha ishindwe kushinda kwa kishindo katika uchaguzi uliopita.

Katika taarifa yake, Mukama anasema kikosi kazi hicho kiligundua kuwa “kunahitajika udhibiti wa vyombo vya habari vya kijamii (social media) kama vile simu za mkononi, twitter au u-tubes.”

Anasema, vyombo hivyo ndivyo vyenye nguvu kubwa katika kuhamasisha watu, akitoa mfano wa Jamii Forum aliyodai inaundwa na vijana wa Chadema.

Mukama alisema vijana hao wanafanya kazi hatarishi “kwa chama chetu na serikali yake kwa kutoa taarifa nyingi za upotoshaji ambazo zinasomwa na watu wengi sana duniani, hasa vijana.”

Gazeti hili lilipomtafuta William Malecela anayeishi New York, Marekani, kujua iwapo ni mwanachama wa Chadema alisema, “Si kweli hata kidogo.”

Alisema yeye ni mwanachama mwaminifu wa CCM, na kwamba hivi sasa yuko mbioni kufungua tawi la chama hicho mjini New York Marekani.

Alisema, “Tatizo la watu wa CCM hawataki kusoma, badala yake wanakuja na ripoti za kuokoteza mitaani. Mimi ni mwanzilishi wa JF, nimekuwa huko tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006.”

Kwa upande wake Maxence Melo, anasema wakati mtandao huo unaanzishwa mwaka 2006 kabla ya kampuni kusajiliwa mwaka 2008, kulikuwa na watu wengi sana, wakiwamo vigogo wa CCM.

Anasema miongoni mwa wanachama wa mtandao huo, ni Nape Nnauye, Hussen Bashe na Khamisi Kigwangala.

Anasema mbali na wanachama hao wanaofahamika kwa majina yao, wapo wanachama na viongozi wengi wa CCM, wanaotumia majina bandia.

Naye Islam, mkurugenzi mwingine wa kampuni hiyo amesema, “Hawa watu wameshindwa hata kwenda BRELA  kutafuta nyaraka. Hayo yote yaliyosemwa na CCM hayana ukweli hata kidogo. Huo ni uchovu wa kufikiri.”

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki mbili baada ya Rais Kikwete kunukuliwa akisema, “…chama hiki hakiwezi kuendelea kubaki na wezi.”

Kikwete alikuwa akinukuu taarifa ya Mukama iliyosema kushindwa kwa CCM, kumetokana na chama kutuhumiwa kukumbatia watuhumiwa wa ufisadi.

Ripoti ya Mukama ndiyo inayotumiwa na Kikwete kutaka kuwafukuza kutoka katika chama hicho wanaowaita “mafisadi” – Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge.

0
Your rating: None Average: 4.3 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: