Mukama anasubiri kusaga meno


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

WAAFRIKA tungali tunasumbuliwa na uchawi. Siyo jambo la kushangaza kusikia ndugu wanakatana mapanga, kisa kushukiana uchawi.

Matukio ya kuuawa kwa vikongwe wanawake kwa hisia za uchawi yametikisa nchi hii kwa miaka mingi sasa hasa mikoa ya Mwanza, Geita na Shinyanga.

Kwa kifupi, Watanzania kama walivyo Waafrika wengi wanasumbuliwa sana na imani za kishirikina. Kwa Waafrika misiba inachukuliwa kwa uzito mkubwa sana.

Kuzika ni suna. Kushiriki kuzika kunafungamanishwa na kutengeneza amani na waliotangulia mbele ya haki. Ni kawaida kusikia mtu akielezwa kuwa anaishi maisha ya ovyo kwa sababu hata hakujali kumzika baba yake.

Kifo, mazishi na kila kinachoambatanishwa na mtu kutangulia mbele ya haki, kwa Waafrika vinachukuliwa kwa hadhari kubwa.

Wiki iliyopita taifa lilipatwa na msiba wa kuondokewa na mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bob Nyanga Makani. Ulikuwa msiba wa kitaifa kwa maana nyingi. Kwanza, Makani ameshika nyadhifa mbalimbali nchini, ikiwamo naibu gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakili wa Serikali, mwenyekiti na katibu mkuu wa CHADEMA.

Uthibitisho ni ushiriki wa viongozi wa kitaifa, akiwamo Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete; Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad; Mawaziri Wakuu wataafu, Dk. Salim Ahmed Salim; Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye.

Pia viongozi wa vyama vya siasa wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa; Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama.

Miongoni mwa viongozi waliozungumza wakati wa kumuaga Makani katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kabla ya safari yake kwenda kulazwa mkoani Shinyanga kuanza, alikuwa Mukama ambaye alichafua hali ya hewa.

Kwa muonekano waliofika pale, walikuwa na majonzi; walikwenda  kwa kutambua mchango wa kiongozi huyo katika kulitumikia taifa lakini zaidi kuthubutu kuasisi chama cha upinzani cha kupambana na CCM, katika nyakati ambazo upinzani haukuwa na tofauti na uhaini na kila aina ya uasi.

Kwa mshangao, Mukama alipofungua kinywa chake tu alikumbusha kitu kimoja kinachofananishwa na imani za kishirikina; kwamba Waafrika wanaamini wachawi pia hushiriki misiba lakini ndani ya nafsi zao wakishangilia kuona watu wakiwa na majonzi. Wachawi wanafanya hivyo kwa sababu msiba kwao ni kazi ya mikono yao.

Mukama katika hafla ya Karimjee, ingawa alikuwa miongoni mwa waombolezaji, ndani ya nafasi yake alikuwa anasikitika Makani ameondoka na kuiacha CHADEMA nyuma. Alitamani angelikufa nayo, ndiyo maana hakutafakari wala kutambua hatari ya kutumia msiba ule kupanda mbegu za kizandiki na uchochezi usiokuwa na tija.

Mukama, kwa kauli aliyotoa ni kama hakuwa katika hafla ya kumuaga Makani ila kuendeleza malumbano ya kisiasa kwamba CHADEMA ni chama cha kikanda na siyo chama cha kitaifa.

Mukama aliibua hoja kwamba Makani alikuwa katibu mkuu na mwasisi wa CHADEMA pekee ambaye hakutoka Kanda ya Kaskazini, akikusudia kuwasilisha ujumbe kuwa CHADEMA ni chama cha kikanda, kilichoasisiwa katika kanda moja tu ya Tanzania, Kaskazini.

Ni kutokana na kauli hii ya kizandiki Mbowe hakuwa na njia nyingine isipokuwa kumjibu Mukama katika msiba uleule kwa kutaja waasisi wote na walikotoka.

Waasisi hao ni Edwin Mtei (Arusha), Makani (Shinyanga), Marehemu Brown Ngwilupipi (Iringa), Edward Barongo (Kagera), Mary Kabigi (Mbeya), Menrad Mtungi (Kagera), Costa Shinganya (Kigoma), Evarist Maembe (Morogoro) na Steven Wassira (Mara).

Mbowe alisema anawajua waasisi hao siyo kwa kusimuliwa ila alikuwako. Akadokeza: “Mimi wakati huo nilikuwa mdogo na shughuli zangu zilikuwa kuandaa vikao na mikakati ndani ya chama. Nashangaa sana wakati nakumbuka historia ya chama hiki, hivyo watu wasijaribu kuipotosha.”

Maelezo mengi ambayo watu wa bara hili hutoa kusingizia uchawi hayana tofauti na huu ‘uchawi’ mpya wa Mukama, kudhani kuwa njia ya kuua CHADEMA ni kukitangaza kuwa ni chama cha kikanda tena kwenye msiba wa muasisi wake.

Kwangu huu ni uchawi mwingine tena mpya kwa kada wa CCM kushindwa kushughulikia matatizo ya kisiasa ya chama chake kwa majawabu ya sayansi ya siasa na kusaka njia za pori za kukiua chama cha siasa kinachoibua changamoto mpya kila uchao dhidi ya watawala na chama tawala.

Mukama kwa kauli ya kuzungumzia uasisi wa CHADEMA katika shughuli ya maombolezo makubwa na majonzi kama ya Makani ni njia nyingine ya kutafuta pa kupenyeza sumu yake ili kukibomoa chama ambacho ndani ya nafsi yake, anajua kuwa ni chama makini, cha kitaifa tangu kuasisiwa kwake na kimeleta changamoto kubwa kwa chama tawala ili kiondokane na usingizi na mazoea ambayo sasa yameifikisha nchi hii kusikoelezeka.

Mukama anajua fika kwamba kama siyo CHADEMA, leo hii asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM. Anapaswa kuishukuru CHADEMA kwa kusaidia kupunguza kura za Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambao uliipa ujumbe murua CCM kuwa zama za kudanganyana na kupiga propaganda ambazo hazina tija kwa wananchi zimekwisha.

Kura za Rais Kikwete zilipungua kutoka zaidi ya asilimia 80 mwaka 2005 hadi wastani wa asilimia 60 tena za kuchakachua mwaka 2010 ndiko kulimwibua Mukama na utafiti wake wa kujivua gamba.

Kwa kuwa Mukama anajua anatokana na nini hadi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, angeiheshimu CHADEMA kwani ndiyo imemwondolea mtangulizi wake, Yusuf Makamba.

Katika mazingira hayo, Mukama hana sababu ya kutafuta mbinu za kichawi za kuipunguza nguvu CHADEMA; hana sababu ya kutunga mambo juu ya mwanzo wa chama hicho, wala hana sababu ya kulia machozi ya mamba katika msiba wa kiongozi wa CHADEMA.

Anapaswa kutambua kwamba kukwama kwa CCM na kupanda kwa CHADEMA ni kazi ya mikono ya CCM na viongozi wake. Na itakuwa ni kazi ya mikono ya CCM na viongozi wake kubadili hali hiyo, siyo kwa propaganda bali kufanya kazi kweli na wananchi waone mabadiliko.

Kama wenzetu wa mikoa ya Shinyanga, Mwanza na sasa Geita wasivyokuwa na sababu ya kuua vikongwe wakidhani ndio chanzo cha vifo vya watoto au balaa na kila aina ya janga ndani ya jamii, wanapaswa kujua kuwa ni kwa kufanya kazi kwa bidii tu, kupata tiba sahihi ya magonjwa kwa kwenda hospitalini watafanikiwa kupambana na changamoto za maisha.

Mukama ajue kuwa bila kujituma kwa CCM, bila ya juhudi za kweli za kusaka majawabu ya wananchi katika shida zao, visingizio kwamba CHADEMA ni chama cha kikanda havitaondosha shida. Anapaswa kujitazama na kutambua kuwa pamoja na uchawi huu mpya anaoibua sasa bado CHADEMA inachanja mbuga; kama anabisha asubiri 2015. Hatalia kwa staili hii ya juzi kwenye msiba wa Makani bali atasaga meno.

0
No votes yet