Muungano wetu unamnufaisha nani?


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

NAANZA makala hii kwa kuwakumbusha yaliyotokea mwaka 1964. Mwaka huo mimi nilikuwa darasa la kwanza katika shule iliyoitwa Nyangoto Lower Primary School ambayo iliishia darasa la nne na waliofaulu walipelekwa Nyamongo Extended Primary School kuendelea darasa la tano.

Siku moja tulifika shuleni, kama kawaida, mapema asubuhi na kuanza shughuli za usafi wa madarasa, viwanja na barabara. Kabla ya saa 2.00 ikapigwa kengele tukakimbilia mistarini kuwasikia walimu wetu walikuwa na lipi la kutueleza.

Mwalimu mkuu, ninayemkumbuka kwa jina moja tu la Sayi alitokea akifuatiwa na walimu na viranja wakiwa wamebeba maboksi kadhaa makubwa. Maboksi yale yalipofunguliwa ndipo tukagundua kwamba yalikuwa yamejaa vikombe vya plastiki vya kijani vilivyoandikwa maneno “muungano” kwa chini na pembeni.

Sayi akaamrisha vikombe vile vigawanywe kwa kila mwanafunzi kikombe kimoja halafu akatutangazia kwamba turudi nyumbani kwa sababu Tanganyika ilikuwa imeungana na jirani yake Zanzibar na hivyo siku ile ilikuwa sikukuu.

Kutoka pale tilishindana kukimbia kurudi nyumbani na vikombe vyetu. Nakuhakikishia sikupumzika popote kutoka Nyangoto hadi Nyamerama kupitia Keminisi, kote huko ni mbio tupu. Furaha na hamasa ya kukimbia ilitokana na kupewa kikombe cha plastiki na siyo muungano.

Ikumbukwe kwamba wakati ule vyombo vya nyumbani kwa Mkurya wa kawaida vilikuwa vya vigae, miti na vibuyu yaani ebitupa, ebisencho na ebinyongo kwa hiyo chombo cha plastiki kilionekana kama lulu. Tangu siku ile wanafunzi tulitamani sana miungano iwepo mingi ili tupate vikombe vingine vya plastiki.

Hiyo ni kwa upande wetu wanafunzi wa vijijini ambao hatukuwa na habari kilichokuwa kinatokea mijini, maana kijijini kwetu, wakati huo, kulikuwa na watu wawili tu wenye redio: Mwita Kicheere aliyekuwa na NEC na Ngocho Kenani aliyekuwa na Philips.

Swali likaja, walioungana hasa ni akina nani? Uchunguzi wangu umegundua kuwa mwaka 1964, Waunguja waliupindua utawala wa Kisultani na kuuweka wa kwao chini ya Baraza la Mapinduzi. Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Wapemba waliyapinga mapinduzi hayo ya Januari 12. Wapemba waliamini, na nasikia hadi leo, wanaamini kuwa wao ni Warabu hata kama wangekuwa weusi kama mkaa na hivyo waliyaona mapinduzi yale kama ya kupindua utawala wao wa Kiarabu na Kisultani.

Kwa hiyo, walioungana na Tanganyika si Wazanzibari bali ni Waunguja. Katika siku za awali, vyeo karibu vyote vilishikwa na Waunguja, na wakati huo kule Pemba mashamba ya karafuu yakaanza kudorora kwa vile wenye mashamba Waarabu walioishi Unguja, walikuwa wamekimbia nchi au wameuawa katika mapinduzi.

Hali hii ilisababisha maisha kuwa magumu kisiwani Pemba. Wapemba wakatafuta njia ya kuondokana na maisha magumu kwa kuhamia Unguja ambako kwa sababu za kijadi hawakutakiwa.

Waunguja nao (samahani kusema hili lakini ndio ukweli, wanawadharau sana Wapemba kwa kujifanya Waarabu ingawaje na Wapemba nao wanawadharau sana Waunguja kwa uvivu) walitafuta mbinu za kuzuia mtiririko wa Wapemba kwenda Unguja. Hapo ndipo akateuliwa mtawala wa Pemba aitwaye Ramadhani Abdalla maarufu Bwana Mamba.

Huyu anajulikana pia kama kiboko ya Wapemba. Aliweka watu pale forodhani Unguja, ambao kila mtu aliyetelemka kutoka melini kutokea Pemba walimpa mtihani, akishindwa anarudishwa melini na akipasi anaruhusiwa kutelemka Unguja.

Mtihani ulikuwa kutamka neno MKATE. Wapemba wengi husema NKATE.

Uhasama, kutokuelewana, kutetana, kudharauliana na hata kubaguana kati ya Wapemba na Waunguja kuliendelea hadi 1982 alipoingia madarakani Bwana Ali Hasan Mwinyi ambaye alijaribu kusawazisha mambo na kama unakumbuka vizuri enzi hizo ndipo ilipotungwa katiba ya Zanzibar iliyotambua haki za binadamu.

Halafu akateuliwa Waziri Kiongozi mmoja aitwaye Seif Shariff Hamad ambaye kwa makusudi au kwa bahati tu, kipindi hicho kilishuhudia Wapemba wengi wakijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine duniani siyo Tanzania pekee.

Matokeo ya hali hiyo ya Wapemba kusoma kwa wingi wasomi wengi visiwani wakawa Wapemba, lakini kutokana na kuhasimiana, kudharauliana, kutoaminiana na kubaguana, huko nyuma kila ilipoundwa tume kushughulikia mambo ya muungano, waliteuliwa watu kutoka CCM Zanzibar tena wote Waunguja ambao si wasomi au waelewa wa mambo wazuri.

Kwa hiyo, kila kilichoamliwa kuhusu muungano kilipitishwa kwa matakwa ya CCM Zanzibar na Waunguja, ndiyo maana kila mara maslahi ya Zanzibar ni kama hayazingatiwi kutokana na aina ya wajumbe wanaoiwakilisha kwenye masuala ya muungano. Sijui kama hali hii imebadilika leo.

Ili Wapemba wanufaike na muungano waliamua kuingia kwenye biashara, tena biashara yenyewe wanaifanyia huku Bara. Pia wakaanzisha kilimo huku Bara. Halafu wakachanganyika na Wabara kujenga majumba Dar es Salaam, Bagamoyo na Tanga.

Matokeo yake ukienda Kahama (1996)  mwenyekiti wa wachimba dhahabu ni Maalim Kadau, Mpemba; ukienda Shinyanga utawakuta Wapemba wanalima mpunga, Lindi Wapemba wanakata mikoko; Pwani Wapemba wanachoma mkaa na kuuza Yemen na Arabuni.

Sasa Rais wa Zanzibar ni Mpemba, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ni Mpemba, wauza simu maarufu na wafanyabiashara Dar es Salaam ni Wapemba; waagizaji bidhaa wakubwa kutoka Arabuni na Uajemi ni Wapemba; wasomi wazuri vyuo vikuu Bara na Zanzibar ni Wapemba.

Kwa ufupi, wanaonufaika na muungano ni Wapemba japokuwa hawakushiriki kuungana na Tanganyika. Ndiyo maana, kwa sasa Waunguja wamekinai na kuja juu wakidai kwamba wao ndio walimpindua Sultani kwa nini wasinufaike na mapinduzi hayo.

Waunguja wanadai sasa kuwa wao ndio walioungana na Tanganyika na siyo Wapemba kwa nini wasinufaike na muungano huu?

Watanganyika nao hawanufaiki na muungano, wakienda Zanzibar wanaitwa machogo, baa zao na wafanyabiashara wachache Wazanzibari zinapigwa mabomu na kuchomwa moto, makanisa yanachomwa moto kuwa ni ya Bara hata kama wanaosali pale ni Wzanzibari. Kwa sababu hii Watanganyika nao siku hizi hawautaki muungano.

Haya sasa mashushushu, watawala na raia mmeupata ukweli kafanyeni hima kurekebisha mambo kama mnautaka muungano udumu. Lakini mhakikishe kwanza Wazanzibari na Watanganyika wanapata haki ya kutoa maoni yao na kupiga kura ya maamuzi kama wawe na muungano au la, wasiburuzwe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: