MwanaHALISI lakabwa tena


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Ndani ya Jamii
Waziri ofisi ya Rais, Utawala Bora, Sofia Simba

GAZETI la MwanaHALISI linalochapishwa kila Jumatano, limeingia matatani tena.

Safari hii, wahusika wakuu wanaolikaba koo ni Msajili wa Magazeti wa Serikali na Waziri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete anayeshughulikia masuala ya Utawala Bora, Sofia Simba.

Wote wawili – Msajili wa Magazeti na Waziri Simba – wanahoji gazeti kuhusiana na makala iliyochapishwa katika toleo Na. 195 la Juni 30 – Julai 6, 2010 kwenye ukurasa wa 10.

Makala hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Akili ya Sofia haiwezi kuwaza zaidi ya ngono!” iliandikwa na mchangiaji wa kila wiki kutoka nje ya safu ya wafanyakazi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), mmiliki na mchapishaji wa gazeti hili pamoja na la Mseto.

Wakati Msajili wa Magazeti wa Serikali anataka gazeti litoe maelezo kwa maandishi na kufikisha ofisini kwake leo Jumatano tarehe 14 Julai kabla ya saa 6:00 mchana, Waziri Sofia amelalamika kuwa amedhalilishwa katika makala hiyo.

Katika barua yake kwa mhariri wa MwanaHALISI ya juzi tarehe 12 Julai, Msajili wa Magazeti wa Serikali ameeleza kuwa makala hiyo imemdhalilisha, kumfedhehesha na kumkashifu Rais Jakaya Kikwete pamoja na Waziri Simba.

Ameeleza kwamba maelezo yanayotakiwa ni ya kujieleza kwanini gazeti lilichapisha makala hiyo na kwanini lisichukuliwe “hatua za kisheria.”

Kupitia kampuni ya uwakili ya Apex Attorneys Advocates ya jijini Dar es Salaam, Waziri Simba amewasilisha malalamiko yake dhidi ya mchapishaji, mhariri katika nafasi yake ya kikazi na kama mtu binafsi, mwandishi wa makala, Mbasha Asenga na mchapaji wa gazeti aliyetajwa Printech Company Limited.

Kupitia barua ya 5 Julai 2010, Wakili na Mkurugenzi Mshirika wa kampuni hiyo, Frank Mwalongo ameorodhesha madai manne anayotaka yatekelezwe na walalamikiwa katika kipindi cha siku 14 tangu siku ambayo barua hiyo ilipokelewa. Vinginevyo, ni uwezekano wa kufungua madai mahakamani.

Madai hayo yanayotakiwa kutekelezwa na walalamikiwa ni kwanza, kukanusha madai ya udhalilishaji na kumuomba radhi waziri katika maelezo yatakayochapishwa kwa nafasi ya robo ukurasa wa mbele wa gazeti kwa matoleo yasiyopungua matatu yanayofuatana.

Pili, maelezo ya kurekebisha na kuomba radhi lazima kwanza yaidhinishwe na mlalamikaji kabla ya kuchapishwa;

Tatu, malipo ya fidia ya jumla ya Sh. bilioni moja; na nne, malipo ya adhabu ya Sh. 300 milioni.

Makala hiyo iliandikwa na kuchapishwa kufuatia kauli aliyotoa Waziri Simba akiwaambia wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma kwamba kama waume zao wanasaidia vyama vya upinzani, basi njia ya kuwakomesha ni kuwanyima tendo la ndoa.

Hatua hiyo ya Msajili wa Magazeti wa Serikali kulibana gazeti hili kutokana na makala linazochapisha ni mwendelezo wa matukio mbalimbali kama hayo tangu Rais Kikwete alipoingia madarakani Desemba 2005.

Lakini kwa mwaka huu wa 2010, hii ni mara ya kwanza gazeti hili kupokea malalamiko kutoka kwa waziri wa serikali.

Serikali ya Rais Kikwete kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, ililifungia gazeti hili Oktoba 18 mwaka 2008 kwa siku 90 kwa madai ya kuchapisha makala ya uchochezi.

Makala hiyo iliongoza gazeti la tarehe hiyo ilielezea taarifa zilizotafitiwa kwa kina kwa kutumia vyanzo madhubuti kwamba kuna mpango unaomshirikisha mtoto wa rais, Ridhiwani Kikwete ambao unapanga njama za kutaka kumzuia Rais Kikwete asigombee nafasi hiyo kwa awamu ya pili ya miaka mitano.

Waziri Simba anakuwa waziri wa pili tangu gazeti hili lilipoanzishwa Mei 2006, kutishia kulishitaki gazeti.

Wa kwanza alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ambaye alitishia kulishitaki gazeti iwapo walalamikiwa, wakiwemo mhariri na mmiliki wasingetimiza masharti aliyoyatoa.

Hata hivyo, hakufungua kesi mahakamani licha ya kwamba walalamikiwa hawakutekeleza masharti hayo.

Baada ya gazeti hili kuchapisha habari ukurasa wa mbele Septemba 2007 zilizonukuu wabunge wa kambi ya upinzani walipotaja “watafuna nchi 11” chini ya jina maarufu la “Orodha ya Mafisadi” lilitishiwa kushitakiwa mahakamani na baadhi yao, lakini hakuna hata mmoja aliyefanya hivyo.

Kwa sasa miongoni mwa kesi zinazosubiri kusikilizwa mahakamani ni iliyofunguliwa na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ambaye amekuwa akitajwa kama kinara wa mpango wa uchotaji mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mpango huo ulifanikisha wizi wa Sh. 133 bilioni kwa kutumia nyaraka bandia.
Kwa muda mrefu sasa Msajili wa Magazeti wa Serikali amekuwa akimtaka mhariri wa MwanaHALISI kutoa maelezo ya maandishi kuhusiana na makala zake. Mara kadhaa mhariri amekuwa akiitwa ofisini kwa msajili kujieleza.

Mara ya mwisho ilikuwa Aprili gazeti lilipochapisha makala kuhusu hadhi ya ma-First Lady wa Afrika. Mama Salma Kikwete alitajwa pia katika makala ile.

0
0
Your rating: None
Soma zaidi kuhusu: