Mwema epusha polisi na mambo ya ovyo


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
IGP Said Mwema

JAMAA yangu mmoja alinisimlia habari za Nigeria kwamba ni taifa kubwa barani Afrika hata duniani, lakini kwa hakika mambo yake mengi ni ya ovyo kabisa.

Alieleza kuwa Nigeria, mtu anaweza kujibinafsishia kila kitu, kuanzia huduma za kipolisi, barabara, elimu, maji, umeme na kila unaloweza kutumia fedha kujimilikisha kwa sheria na kanuni zako. Fedha.

Juzi nilijikuta nikiakisi hili la Nigeria kila nilipotafakari na kutazama polisi wa Tanzania wanavyofanya kazi. Kwanza nikiri tu kwamba, awali alipoingia kwenye kiti cha mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP) Said Mwema, wengi tuliona mabadiliko ya kiutendaji na uwajibikaji wa vijana wake.

Tofauti hii ilionekana kwa sababu moja kubwa, kwamba alilinganishwa na mtangulizi wake, IJP Omari Mahita. Kwa kiasi fulani Mwema alionekana kuwa na ubavu wa kuthubutu kufanyakazi, alipambana na ujambazi uliokuwa umeota mizizi, aliendesha kampeni ya Polisi Jamii, na kila wakati alionekana kuzidi kujenga taswira njema kuhusu polisi.

Pamoja na mafanikio hayo, katika siku za hivi karibuni Polisi wameanza kurudi miaka ya enzi za Mahita. Mfano yapo matukio ya viongozi wa juu wa polisi kuhusika katika kuwabambikizia watu kesi mbaya za madawa ya kulevya; kuna matukio yanayojirudia ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi katika kuwakabili raia.

Matukio haya, kwa bahati mbaya sana, yanatokea baada ya uchaguzi wa mwaka jana. Inaonekana kama polisi wameagizwa kuwatia adabu raia. Ni matukio kama ya Arusha ambako watu watatu waliuawa bila sababu yoyote kwa kuwa tu polisi walikuwa na silaha na raia hawakuwa na kitu.

Kuna tukio la hivi karibuni zaidi la Tarime. Polisi wameua raia watano kwa risasi na kujeruhi kadhaa kwa kile kinachodaiwa kuwafukuza wavamizi kutoka mgodi wa North Mara eneo la Nyamongo.

Matukio mengine ni kama ya Urambo, Mbeya, Dar es Salaam, Moshi na maeneo mengine, ambayo kwa ujumla wake yanaacha maswali magumu juu ya weledi wa polisi. Je, wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia weledi au kuna nguvu fulani kutoka juu?

Haya hayasemwi kuwabeua polisi, hapana. Yanasemwa kwa sababu, mara mbili, kumekuwa na mambo ya kugeuzageuza maneno kwa upande wa polisi kuhusu mazungumzo yao hasa na wanasiasa.

Nitafafanua. Mwanzoni mwa mwaka huu viongozi wa CHADEMA walikubaliana na uongozi wa polisi mkoa wa Arusha juu ya kufanywa kwa maandamano Januari 5. Walikubaliana hata njia ya kupita, lakini baada ya makubaliano yote hayo, uongozi huo ulipiga marufuku maandamano hayo saa za majeruhi, kwa madai kulikuwa na taarifa za kiintelejiensia kuwa watu wangefanya fujo.

Matokeo ya kuyumba kwa polisi katika kusimamia majukumu yao kwa kusema hivi leo na kesho vile, ndiyo yaliyosababisha mauaji kule Arusha Januari 5, mwaka huu na hata kesi inayowakabili viongozi wa CHADEMA leo.

Kadhalika, huko Tarime CHADEMA walikubaliana na polisi jinsi ya kuendesha ibada ya kuwazika vijana wanne waliokuwa wameuawa na polisi wakidaiwa kuwa ni ‘wezi’ kwamba ibada kubwa ya pamoja ingefanyika kwenye uwanja wa Sabasaba mjini Tarime. Lakini jioni ya siku hiyo, licha ya polisi kuwa wamekaa na kukubaliana vizuri kabisa na viongozi hao wa kisiasa, waligeuza maneno na kueleza kuwa kungelikuwa na fujo.

Cha kushangaza ni kwamba kila polisi wanaposema kutakuwa na fujo, wanatumia nguvu kubwa  kupambana na raia ambao kwa kweli hawajajihami kwa silaha yoyote.

Swali linakuja, kama polisi wanakuwa na taarifa muhimu za namna hiyo kinachozuia kuwakamata kimya kimya wapanga mipango ya kuvunja amani ni nini hadi wawatumbukize raia wengine katika usumbufu mkubwa kama ambao tumeshuhudia Tarime, Arusha na Urambo? Nani hasa anaendesha polisi, IJP Mwema au mwanasiasa fulani mahala fulani? Na ni kwa nini iwe hivyo?

Wiki iliyopita imemalizika kwa taharuki kubwa ya kisiasa ikisababishwa na Polisi. Huko Singida Polisi walimkamata Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA),  Zitto Kabwe, kwa madai kwamba alizidisha muda wa dakika 20 kuhutubia mkutano wa hadhara. Dakika 20!

Jijini Dar es Salaam Polisi wakamkamata Mwenyekiti wa CHADEMA na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kwa madai ya kutekeleza amri ya mahakama.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alikamatwa Jumamosi akalala ndani siku mbili ili afikishwe mahakamani Arusha ambako yeye na viongozi wengine wa chama hicho wanakabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko isivyo halali Janauri 5, mwaka huu na kufanya uchochezi.

Mbowe hakufika mahakamani siku kesi yao ilipotajwa kwa kuwa tayari alikuwa na udhuru kuwa angelikuwa na vikao vya kamati za Bunge. Taarifa hizo zilikuwa mahakamani, hakimu alijua hivyo na alitaarifiwa hivyo wakati kesi hiyo ilipotajwa mara ya mwisho.

Kumekuwa na maswali mengi kutoka kwa wananchi kwamba mbona polisi hawakamati wahalifu sugu wanaohujumu uchumi lakini wamekuwa wepesi sana kufukuzana na raia na wanasiasa katika vitu vidogo vigodo?

Kwa mfano wakati malalamiko ya kukamatwa Mbowe na Zitto yakitolewa na watu mbalimbali, kuna hoja zilijengwa kuwa ni kwa nini polisi wameshindwa kukabili watu wakubwa wenye tuhuma za ufisadi, waliokwapua fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited?

Pia watu wanakumbusha kwamba kuna kesi nyingi za taifa kuhujumiwa katika mbuga za wanyama, kusafirishwa nyara nje ya nchi; wizi kwenye madini; wizi katika uingizaji wa bidhaa feki nchini na maovu mengine makubwa yanayokwamisha uchumi wa taifa hili, lakini husikii  polisi wakijisumbua nayo. Wao ni kuzuia maandamano ya amani ya raia na kufukuzana na wafuasi wa vyama vya upinzani kana kwamba upinzani nchini ni uhaini!

Mambo yanavyokwenda siku baada ya siku ni kana kwamba sasa polisi ni taasisi muhimu ya kushughulika na wanasiasa tena wa upinzani. Polisi wanapofikishwa katika mazingira kama haya, mtu anaanza kupata mawazo yale ya Kinigeria kwamba hivi kweli sasa polisi wamepoteza weledi wao ulioanza kurejewa chini ya Mwema na sasa wanarudi kule kule kufanya mambo ya ovyo?

Je, wanatekeleza wajibu wao kwa kujituma kulingana na taratibu na kanuni za kazi zao au sasa ni kuelekezwa cha kifanya? Ni mwendo wa kukomoana? Je, polisi hawaelewi kwamba hawafungamani na siasa kwa mujibu wa ajira zao? Kama wanaelewa, ni kitu gani sasa kinawatuma kujitumbukiza katika utendaji unaoakisi siasa tena siasa za ovyo kabisa? Hili ni swali analoweza kulijibu IJP Said Mwema.

0
No votes yet