Mwenyekiti wa Mtaa ashitaki MwanaHALISI


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 September 2009

Printer-friendly versionSend to friend

MWENYEKITI wa serikali ya mtaa Msewe, Ubungo, Dar es Salaam, Jaffari Juma Nyaigesha, anataka alipwe Sh. 100 milioni kwa madai ya "kukashifiwa" na gazeti la MwanaHALISI.

Katika kesi Na. 165 ya 2009 aliyofungua katika mahakama ya hakimu mkazi ya Kisutu, Nyaigesha anashitaki mhariri wa gazeti, mshauri, mchapishaji, mtu mmoja aitwaye Stella Kajuna na makampuni mawili ya uchapaji ya jijini Dar es Salaam.

Mashitaka haya yamekuja wakati Nyaigesha akihaha kutafuta kupitishwa kugombea nafasi yake katika uchaguzi wa serikali za mitaa Oktoba mwaka huu.

Baadhi ya wananchi katika kijiji cha Msewe wanapinga mwenyekiti huyo kugombea tena uongozi kwa madai mbalimbali na mtu mmoja, Renatus Paisi, amepeleka pingamizi kwa Kamati ya siasa ya tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tangu mwaka 2003 jina la Nyaigesha limekuwa kwenye mjadala mkubwa katika vyombo mbalimbali vya habari, muhusika akihusishwa na matukio kadha wa kadhaa kijijini kwake, lakini ameamua kushitaaki MwanaHALISI peke yake.

Mwanachama wa CCM ambaye amewekea Nyaigesha pingamizi ili asigombee tena uenyekiti, amejitambulisha kuwa ana kadi Na. DFG 703793.

Katika pingamizi lake la 18 Agosti 2009, Renatus Paisi amesema Nyaigesha amekuwa akituhumiwa kashfa nyingi lakini hajawahi kukanusha, jambo ambalo linachukuliwa kuwa huenda ni sababau ya kufungua kesi dhidi ya gazeti.

Paisi anadai katika pingamizi kuwa Baraza la Kata Ubungo liliishamtia hatiani Nyaigesha kwa "kutumia mihuri ya serikali kwa njia ya udanganyifu. Hukumu hiyo ni halali; hivyo hapaswi kugombea."

Kwa mujibu wa Kesi ya Madai Na. 13 ya 2003 katika baraza ahilo, chini ya mwenyekiti A.G. Mbepera, ambayo uamuzi wake ulitolewa 15 Mei 2004, Nyaigesha alipatikana na kosa la kushuhudia mauzo ya ardhi "huku akijua wazi kuwa aliyeuza kiwanja siyo mwenye mali."

Uamuzi wa Baraza unasema, "Imebainika kwamba ndugu Jaffari ni mtu asiyeeleweka kufuatia kujihusisha kwake kwa karibu sana na kesi hii…Hata hivyo, Baraza linamwona na hatia kwa matendo na kauli zote alizotoa na kusababisha kiwanja husika kiuzwe bila ya idhini ya mwenyewe."

Aidha baraza lilisema kuwa "linapendekekeza kwenye mamlaka iliyo juu ya serikali ya Mtaa, kumchukulia hatua zinazostahili." Nyaigesha hakukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Katika hatua nyingine, pingamizi linahusisha madai kadhaa yakiwemo "kughushi mihuri ya serikali,"

Jambo ambalo inadaiwa lilithibitishwa na mahakama ya mwanzo Manzese, jijini Dar es Salaam. Muhusika hakukata rufaa kupinga.

Mweka pingamizi anasema, "Vyama vya upinzani hati nilizoambatanisha hapa na wao wanazo na wamejiandaa kumwekea pingamizi la kisheria endapo jina lake litashindanishwa na wao ngazi ya kugombea uenyekjiti wa serikali ya mtaa Msewe."

Mwanamke pekee anayeshitakiwa pamoja na waandishi na gazeti, Stella Kajuna, ni mkazi wa Msewe ambaye amekuwa akituhumu baadhi ya viongozi wa serikali ya mtaa kutotenda wajibu wao wa kusimamia haki.

Nyaigesha anadai kuwa waandishi, gazeti na wachapaji wamemkashifu na kwamba anastahili fidia ya Sh. 100 milioni.

Hata hivyo, maelezo ya mashitaka yaliyowasilishwa kwa gazeti la MwanaHALISI tarehe 24 mwezi huu, yakionyesha siku ya kutaja kesi kuwa Jumanne (jana), yanaonyesha kusainiwa na kuwasilishwa mahakamani zaidi ya miezi miwili iliyopita.

Mdai alisaini tarehe 16 Julai 2009 wakati ofisa wa masijala ya mahakama alisaini siku moja baadaye (tarehe 17 Julai 2009).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: