Mzee Mukama amepwelewa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

KUPWA ni kitendo cha maji ya baharini kurudi kwenye kina kirefu. Maji yakijaa hadi ufukweni hubeba samaki, wadudu na takataka na yanapokupwa samaki, wadudu na takataka hupwelewa.

Binadamu anayekosa busara na hekima huyo atakuwa amepwelewa; atazungumza chochote kinachombainisha kwamba hana busara wala hekima.

Mathalani baba akipewa taarifa na majirani kuwa mtoto wake ni mwizi, lakini yeye akajibu kuwa analipiza kisasi eti naye amekuwa akiibiwa, baba huyo amepwelewa.

Baba akiambiwa kwamba mtoto wake anatukana ovyo watu mitaani lakini baba huyo akajibu kuwa eti mtoto wake anajibu mapigo, pia baba huyo amepwelewa; hana busara wala hekima.

Baba mwenye busara na hekima atakaa chini, atatafakari na kisha atamwita mtoto wake na kumkanya. Hawezi kutoa majibu ya kihuni ya eti analipa kisasi au anajibu mapigo.

Mapema wiki iliyopita baba mmoja – mtendaji mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama – aliita waandishi wa habari ili awaambie alivyokasirishwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Baada ya baba yule kutema cheche zote dhidi ya LAAC akidai imejigeuza polisi, mwendesha mashtaka na mahakama, akasema “nchi haiwezi kuendeshwa na wajinga na wahuni”.

Akasisitiza, “Nchi haiwezi kuendeshwa na wajinga na wahuni, na siyo kila mtu ndani ya CCM anahusika na ufisadi wa Richmond, mimi ni Clean Man (mtu safi).”

Nikajiuliza kwani wasafi hawachafuki? Si ndiyo maana tunaoga kila mara? Baba huyu amesahau kwamba hata yule njomba ambaye Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alimwona clean alipoingia ikulu mwaka 1995 alitoka mwaka 2005 akiwa Dirty Man!

Mtu anaweza kujiita msafi, na ndiyo silka ya binadamu, lakini matendo yake yakamuumbua. Nyaraka si ndizo zinasema baba hana udhu?

Kisa cha baba huyu – ambaye ofisi yake iko Dodoma lakini yuko Dar es Salaam kila siku – kutumia maneno “wajinga” na “wahuni” katika mkutano na waandishi wa habari ni kuonyesha hasira akipinga kuhusishwa na ufisadi katika ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa jijini Dar na kuruhusu ujenzi wa bwawa kwa ajili ya wananchi lakini kwenye “ranch” ya kigogo mwingine wa CCM huko Sumbawanga.

Waandishi wakasubiri. Alipomaliza kutema cheche zake wakamuuliza kwa nini CCM iliacha kunadi sera wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki badala yake ikaruhusu “mitusi”.

Baba yule akajibu kwamba matusi yaliyoporomoshwa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde wakati wa kampeni “alikuwa anajibu mapigo ya wapinzani wao wa kisiasa”.

Baba yule alisema Lusinde hakufanya kosa hata kidogo kwa kuporomosha “mitusi”, hiyo ilikuwa namna ya kujibu makombora ya wapinzani wao Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kama baba huyu ambaye ni taswira ya chama anasema ruksa matusi nani atapinga? Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alisikia matusi hayo, lakini hakukemea; masikio ya msimamizi wa uchaguzi huo, Trasiace Kagenzi hayakusikia na mbaya zaidi Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikanyamaza tuli.

Tendwa, ambaye hata kabla vumbi la uchaguzi mdogo halijaanza kutimka alimwonya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema asikanyage Arumeru Mashariki kwa madai aliwaudhi wazee, alifunga masikio asisikie ‘mitusi’ ya Lusinde.

CCM kweli wamepwelewa. Wanafurahia kufanyia uhuni  watu wengine lakini wanakimbilia kortini wakifanyiwa uhuni huohuo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: