Naielekeza bunduki kwetu

ALEXANDER Michael ni rafiki yangu kwa muda wa miaka 15 sasa. Tumefahamiana tangu tukiwa wanafunzi wa shule ya sekondari hapa Dar es Salaam.
Majuzi hapa kapata kazi katika taasisi moja inayojihusisha na mambo ya utafiti. Kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kufanya utafiti kuhusu sababu zilizoifanya mikoa ya Kusini kuwa masikini kuliko mingine hapa nchini.
Alitakiwa kwenda walau katika mikoa miwili na wilaya nne. Alex hakwenda hata katika mkoa mmoja na maana yake ni kwamba hakwenda hata katika wilaya moja.
Lakini alifanikiwa kuandaa ripoti kuhusu “utafiti wake.” Alichokifanya Alex ilikuwa ni kuandaa hojaji (questionnaire) yake na kuchapa karatasi za kutosha. Baada ya kumaliza kazi hiyo, alichukua makaratasi yake na kwenda kulala katika hoteli moja iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani kwa siku tatu.
Alitumia siku hizo tatu kujaza hojaji hiyo iliyokuwa na maswali kuhusu wananchi wa mikoa ya Kusini. Yeye ndiye akajifanya kuwa “wananchi” wa mikoa ya Kusini !
Alipomaliza ‘utafiti’ wake huo, akawasilisha ripoti yake ofisini kwake na kwa sasa ofisi hiyo inatumia utafiti huo wa Alex kueleza sababu za umasikini katika mikoa ya Kusini.
Matokeo ya tafiti za namna hiyo ni kwamba mikoa ya Kusini inaendelea kuwa masikini. Tanzania inaendelea kuwa masikini kwa vile nyingi ya tafiti zilizofanyika ni za dizaini ya ile ya Alex.
Yupo pia jirani yangu Dorca ambaye ni ofisa manunuzi katika hospitali pekee ya rufaa mkoani hapa. Kwa kutumia nafasi yake hiyo, ananunua dawa zilizopitwa na wakati kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wanaofika hospitalini kwake.
Badala ya kununua dawa zilizoombwa, yeye ameamua kununua dawa za kiwango cha chini. Lengo lake ni kutengeneza fedha tu ili aonekane ‘mjanja’ mbele za watu. Na ndugu na jamaa zake wanasema ana akili kuliko akina sisi ambao hatuna pesa kama yeye.
Yupo ndugu yangu Salum, mwalimu mkuu wa shule ya msingi, ambaye ameamua kutumia saruji iliyopangwa kujenga madarasa ya shule yake kujengea ‘kibanda’ chake kule Mbagala.
Kwa kufanya hivyo, madarasa wanayosomea wanafunzi wake yamejengwa kwa matofali yenye mchanga mwingi kuliko sementi. Kama siku itatokea siku watoto watagombana na kuangukia kwenye ukuta wa darasa lao, janga litatokea kwenye shule hiyo.
Na hii ni mifano michache ambayo ipo kwenye jamii yetu. Wale wanaofanya hivi tunaishi nao mitaani kwetu na katika vijiji na vitongoji vyetu. Hatusemi kitu kuhusu wao, sisi tunalia na “mafisadi papa.”
Nimeyakumbuka haya yote wiki hii baada ya kupata fursa ya kutembea na mgeni wangu mmoja aliyetembelea Tanzania kwa muda wa wiki moja kuanzia Ijumaa iliyopita.
Raia huyo wa Sweden alipata mshangao wa mwaka wakati tukiwa njiani kuelekea hoteli ya White Sands jijini hapa. Majumba na magari ya kifahari tuliyopishana nayo njiani yalikuwa kinyume na kile alichotaraji kukiona hapa nchini.
Yeye ni miongoni mwa watu wanaopigania misaada kwa ajili ya nchi masikini kama Tanzania. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutembelea hapa. Alichokiona ameniambia wazi ya kuwa atajifikiria mara mbilimbili kabla ya kuomba msaada kwa Tanzania.
Baadhi ya majumba ya kifahari aliyoyaona aliniambia nchini kwao yanamilikiwa na nyota maarufu wa muziki, filamu na familia za kitajiri. Si nyumba zinazoweza kumilikiwa na watumishi wa umma.
Kwa wale watumishi wa umma wenye nyadhifa za juu, alisema wengi wao hujenga kwa kutumia mikopo ya benki na taasisi nyingine za fedha.
Nikamwambia wale wenye nyumba alizoziona, wengine ni watumishi waajiriwa wa serikali ambao mshahara wao unafahamika. Nilichomwambia sina uhakika nacho ni kwa vipi walipata fedha za kuwawezesha kujenga majumba hayo.
Tanzania kwa sasa ina watu wenye magari yenye thamani kubwa ya fedha. Kuna waajiriwa wa serikali wanaokwenda maofisini na magari yao binafsi yenye thamani ya mpaka Sh. milioni 200.
Cha ajabu ni kwamba hakuna anayeshtuka. Mambo yanakwenda kama kawaida na inaonekana hakuna anayejali ni kwa vipi mtu mwenye mshahara wa Sh. 500,000 kwa mwezi anaweza kumiliki gari la aina ya Vogue lenye thamani ya Sh. milioni 200.
Sikatai kwamba kuna rushwa ya kutisha ndani ya serikali yetu wahusika wakuu wakiwa viongozi wa juu wa serikali yetu. Na ninajua ni vema tukaendelea kupigia kelele ufisadi uliopo kwa wanasiasa wetu.
Lakini nafikiri jamii yetu ina wajibu wa kufanya kwa watu kama Alex na Salum. Tuna kazi kubwa ya kufanya kwa watu ambao tunaona kabisa wana utajiri ambao hauna maelezo mazuri.
Hivi, tunapata uthubutu gani wa kuwasema viongozi wetu kama tunashindwa kuwaeleza ukweli rafiki zetu, majirani zetu, watoto na kaka zetu ambao tunaona wanaharibu maendeleo ya nchi yetu sasa na vizazi vijavyo mbele ya macho yetu.
Watanzania sasa tunafahamika kwa udokozi kwenye mahoteli. Watanzania sote sasa tunafahamika kwa wizi unaofanyika kwenye bandari zetu wakati magari kutoka nje ya nchi yanapowasili.
Lakini yote haya tunafanya kama hatuyaoni. Hatuyakemei kwa sababu yanafanywa na kaka zetu, watu tuliosoma nao na majirani zetu. Hii si sahihi.
Kama ambavyo taifa linaathirika kwa rushwa wakati wa kutia saini mikataba, taifa pia linaathirika wakati wagonjwa wanapolishwa dawa zilizopitwa na muda.
Taifa linaathirika sana wakati wanafunzi wanapokufa shuleni kwa kuangukiwa na matofali. Taifa linaumia wakati watumishi wake wanapoendesha magari ya kifahari na kujenga mahekalu kwa sababu ya kulipa mishahara hewa, kudhulumu pensheni wazee na kuiba mafuta ya magari.
Ufisadi ni ufisadi tu. Hauna rangi, hauna kabila, hauna itikadi, hauna dini. Tutashinda vita dhidi ya ufisadi pale tutakapoanza kuwakemea wale walio mbele ya macho yetu.
Ukianza na yule aliye mbele yako kwa sasa. Mimi nimeanza kumshughulikia Alexander Michael tangu juzi.