Naitamani ndoa ya Yanga, Papic

NIANZE kwa kuwatakia Kheri ya Mwaka Mpya kwa wote waliobahatika kupita katika chujio la Mwenyezi Mungu na kuuona mwaka 2010.
Mwenyezi Mungu awape faraja na kuwapa nafuu walioingia katika mwaka mpya wakiwa katika misukosuko ya aina mbalimbali na hali kadhalika, awaangalie nuru ya milele wote walioshindwa kuuvuka mwaka 2009 na kutangulia mbele ya Haki.
Naam. Baada ya salaam zangu, niende moja kwa moja katika hoja iliyonisukuma kuandika makala haya, nayo inahusiana na ubashiri wa rafiki yangu mmoja wa hivi karibuni kwamba, haoni dalili za Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic za kuendelea kubaki katika klabu hiyo.
Ametoa vigezo kadhaa vya ubashiri wake, ikiwa pamoja na kukosa msaidizi licha ya kuusisitizia uongozi mara kwa mara, amekuwa pia na manung’uniko ya hapa na pale, juu ya mazingira yake ya kazi, ikiwa pamoja na kulazimika kuangalia akiwa baa baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya England na nyingine kimataifa.
Kisa? Klabu haijamuunganishia baadhi ya vifaa muhimu kwa kumwezesha kuangalia moja kwa moja mechi akiwa ametulia katika maskani yake.
Kimsingi, nashawishika na kukubaliana na ubashiri na rafiki yangu huyo ambaye kwa leo ningependa abaki kapuni.
Nashawishika kutokana na kuelewa kwamba, mazingira mazuri ya kazi ni moja ya motisha ya kocha yeyote mwenye kuijua kazi yake.
Tuna mifano mingi ya ndani na nje ya nchi ambako makocha hutumiziwa kila kitu. Na kweli, matokeo ya uwanjani huwa bora.
Tuchukulie mfano wa Jose Mourinho alivyoifanyia makubwa Chelsea kabla ya kuondolewa kimizengwe. Mafanikio yake yalitokana na jeuri ya noti ya bilionea Roman Abramovich.
Mark Hughes ameweza kuliweka juu jina la Manchester City kutokana na kutimiziwa mambo mengi, lakini kwa bahati mbaya, amekosa bahati ya kuendelea kufanya kazi na timu hiyo ya Ligi Kuu ya England.
Kwa hapa nchini, Patrick Phiri wa Simba ni miongoni mwa makocha bora msimu huu.
Angalia, hajainua mdomo wake kuutangazia umma juu ya kero au vikwazo anavyovipata katika kazi yake.
Si kwamba hana, bali kwa kiasi kikubwa anatimiziwa na anaridhika. Nani asiyejua ‘balaa’ ya Simba linapokuja suala la soka ya uwanjani? Ni kwa sababu uongozi unathamini taaluma ya kocha wake na kumpa kila aina ya sapoti.
Nimelazimika kuanzia mbali ili kujenga uhalali wa kuheshimu kilio, ingawa ndio kwanza kinaanza cha Papic, kocha aliyekaa na Yanga kwa muda mfupi, lakini matunda ya kazi yake yakionekana mapema mno.
Kombe la Tusker haliwezi kuwa kipimo kikubwa, lakini angalia Yanga sasa inaonekana kucheza kitimu, inaonekana ikitafuta mabao na inaonekana ikipachika mabao tofauti na kabla ya ujio wake.
Yanga chini ya Papic aliyerithi mikoba ya Profesa Dusan Kondic inacheza soka ya kuvutia, tena ikiwa na wachezaji wale wale ambao ilifikia hatua ya wanazi wa soka kuaminishwa kuwa hawafundishiki.
Na majuzi, baada ya kutwaa Kombe la Tusker, Papic alionekana kuielewa zaidi kazi yake baada ya kuonyesha mshangao wa wazi wa wachezaji wake wanaoendelea kutambia ushindi dhidi ya Simba katika mchezo wa nusu fainali.
Amewaambia dhahiri kwamba, “Mnashangalia nini? Shughuli Bado!”. Kwamba, kamwe hawapaswi kuvimba vichwa kwa kitu kidogo kama hicho, bali akili yao ilenge kuifanyia makubwa Yanga si katika ligi au kumfunga mtani pekee, bali katika michuano ya kimataifa.
Kwa mwenye uelewa wa mambo, atafahamu fika kwamba, Papic ni aina ya makocha bora, ‘asiyecheza na jukwaa’, bali mwenye kusaka historia kutokana na matokeo bora ya uwanjani.
Nashawishika kuamini kwamba, kwa Yanga, Papic ni zawadi kubwa. Imebahatika kupata mmoja wa makocha wenye kuijua vyema taaluma yao.
Kama ni bahati, kwa nini Yanga isijijengee mazingira ya kutompeperusha kocha huyu, angalau kwa kumpa ushirikiano wa karibu ili kurahisisha kazi yake?
Haya ya kocha msaidizi na dekoda yanaweza kuonekana kuwa ni madogo, lakini mambo haya haya yanaweza kuzaa madudu mengi yanayoweza kugeuka kero na hatimaye kumfanya Papic atalikiane na Yanga, licha ya kutua nchini kwa lengo la dhati la kujaribu kuirudisha katika chati ndani na nje ya nchi.
Ndiyo maana najaribu kuuzindua uongozi wa Yanga kwa kusema kwamba, binafsi, kama walivyo wanamichezo wengi kamwe wasingefurahia kuona makocha bora kama Papic wakiondoka kwa sababu ndogo, tena zilizo ndani ya uwezo wa klabu.
Aina ya makocha kama Papic wanapaswa kuenziwa si kwa ustawi wa Yanga pekee, bali hata taifa kwa ujumla kama tulivyoshuhudia hivi karibuni akina Mrisho Ngassa wakirejesha makali ya soka na hata kuwa tishio kiufungaji wa mabao jambo ambalo lilianza kusahaulika kutokana na nyota huyo kuanza kuonekana amepoteza mwelekeo.