Nani anasema safari ya Yanga itaishia kwa FC Lupopo DRC?

NI ukweli usiofichika kwamba, nyoyo za mashabiki wa soka nchini, hasa wale wa Yanga zimetumbukia nyongo baada ya kipigo cha mabao 3-2 mwishoni mwa wiki mbele ya FC Saint Eloi Lupopo ya Lumbumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ilikuwa katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, michuano yenye msisimko wa kipekee, utajiri wa vipaji na juu ya yote, fedha chekwachekwa wanayomwagia washindi wa michuano hiyo kila mwaka.
Na baada ya kichapo hicho kilichowaduwaza wengi, hasa kutokana na kuamini kocha Kostadin Papic angeifanyia miujiza, Yanga sasa ina kibarua kigumu ugenini, ambako salama yao ni ushindi tu wiki mbili zijazo.
Ushindi wa bao 1-0 utawavusha hadi raundi ya pili, ingawa 2-0 utakuwa ushindi bora zaidi mbele ya Wakongo hao.
Naamini kuna wanaoyaona hayo kuwa sawa na maajabu, lakini amini usiamini, katika soka lolote linaweza kutokea.
Yanga, licha ya kufungwa si timu mbaya hata chembe, bado imekamilika katika kila idara, pengine mchecheto tu ndio uliowaangusha hasa baada ya kuduwazwa na bao la mapema (dakika ya 5) la Carrington Gomba katika mchezo wa mwishoni mwa wiki.
Pengine kitu pekee kilichowakandamiza Yanga ni kukosa maandalizi ya kutosha, kama ilivyokuwa wenzao waliokwenda Zimbabwe na Zambia kwa mechi kadhaa za kirafiki.
Aidha, wanafahamu mbinu za kisasa za mchezo, ndiyo maana kocha wao msaidizi, Eric Katenda aliwasili nchini mapema kuisoma Yanga, ikiwa pamoja na kushuhudia wakali hao wa Jangwani wakiizamisha Mtibwa Sugar kwa 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa kuwa wao wanatumia mbinu kama hizo, walijihami kwa kutengeneza mbili, moja ya kuendelea na ligi na nyingine kwa ajili ya michuano ya kimataifa, ndiyo maana hata kocha Papic alipokwenda DRC aliambulia kushuhudia kikosi cha pili kikitesa katika ligi ya huko.
Lakini hapa kwetu, ingawa timu ilifahamu kuwa ina jukumu la Ligi ya Mabingwa tangu katikati ya mwaka jana, haikuwa na mikakati thabiti, hadi ilipozinduka hivi karibuni na kutaka ipumzishwe mechi za ligi ili kujiandaa kwa mchezo na Lupopo!
Ebo, miezi tisa ya kujiandaa kuikufaa ndiyo ifae wiki moja? Kama si kuendekeza tabia za uzimamoto ni nini?
Yameshatokea, bila shaka sasa Yanga wakijipanga vizuri, bado wanaweza kufanya kile walichokuwa wamekikusudia, yaani kuitupa nje ya michuano ya mwaka huu FC Lupopo.
Yote yanawezekana, lakini kamwe haitakuwa kazi rahisi, kwani hata Lupopo wenyewe walitamba mapema kwamba wana kiu ya kuyafikia mafanikio ya watani wao wa jadi TP Mazembe pia ya Lubumbashi ambao ni mabingwa wa sasa wa Afrika.
Lakini hiyo isiikatishe tamaa Yanga, kwani yaweza kwenda na moyo kama waliokuwa nao watani wao Simba SC mwaka 1979.
Kwa wasiokumbuka, mwaka huo, katika michuano kama hii Simba ilikandikwa 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Lakini Simba, baada ya kujeruhiwa nyumbani, mbele ya mashabiki wake walioondoka uwanjani na kilio, walijifunga kibwebwe na kwenda katika mchezo wa marudiano wakiwa na kiu ya kuwafuta machozi Wanamsimbazi.
Kila mmoja aliamini Simba inakwenda Zambia kukamilisha ratiba, baada ya kukatishwa tamaa na kipigo cha aibu cha 4-0!
Katika hali iliyowastaajabisha wengi, kwenye mchezo wa marudiano Wekundu wa Msimbazi, waliibuka na ushindi wa mabao 5-0 mjini Lusaka, matatu yakifungwa na Thuwein Ally Waziri, mawili na George 'Best' Kulagwa.
Wanamsimbazi wakaandika historia mpya, kwamba soka ni popote, cha msingi na kuweka nia.
Kwa bahati mbaya, baada ya kuing’oa Mufulira, nyota yao ilizimwa katika hatua iliyofuata baada ya kutolewa na Raccah Rovers ya Nigeria.
Mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam na timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana 0-0 na ziliporudiana mjini Lagos, Rovers walishinda 2-0, hivyo Simba kutolewa.
Ndiyo maana naamini kwamba, licha ya kichapo cha Dar es Salaam, Yanga ikijipanga vizuri, makocha na wachezaji wakawekwa sawa kisaikolojia ikiwa pamoja na kupewa maandalizi ya uhakika, hakuna kitakachoshindikana.
Kama FC Lupopo wameweza ugenini, kwanini Yanga isiweze kuwaziba midomo Wakongo huko Lubumbashi, hasa katika wakati huu ambao Yanga haina ukame wa mabao?
Cha msingi ni kujipanga. Yanga inapaswa kujihesabu kuwa bado iko mashindanoni, kwani soka ni mchezo wa dakika 90 na lolote linawezekana.
Kila la kheri Yanga katika maandalizi ya mchezo wa marudiano.