Nani kawaloga TFF?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly versionSend to friend

NDANI ya miezi miwili tangu Aprili mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefanywa vioja vikubwa vitatu.

Kwa TFF hii, kamwe hatukuwa tumezoea kuwaona wakivurunda mambo. Angalau walianza kuachana na madudu yaliyofanywa mara kwa mara enzi za FAT (Chama cha Soka Tanzania ambacho kimezaa TFF).

Ndipo tunapojiuliza, nani kawaloga TFF na hata kuanza kupoteza heshima waliyokuwa wamejiwekea?

Labda tukumbushane tu baadhi ya madudu yaliyotokea katika kipindi hicho na yanayoonekana kupoteza heshima ya chombo hiki chenye mamlaka ya kusimamia ustawi wa soka nchini.

Ilianza kwa kuwaadhibu Mussa Hassan Mgosi wa Simba na Shaaban Kado wa Mtibwa Sugar kwa madai ya kupigana uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Bara.

Waliwekwa pembeni na kukosa mechi kadhaa wakisubiri suala lao lizungumzwe katika vikao. Mwisho wa siku wakaonekana walihukumiwa kimakosa.

Tayari hapo wachezaji hao walishakosa mechi kadhaa, hivyo kuwaathiri wachezaji wenyewe na hata klabu zao zilizowasajili kwa fedha nyingi.

Kutoka ya akina Mgosi, kikaja kioja kingine. Hiki ni cha kuwafungia Mwenyekiti wa Moro United, Abdul Sauko na makocha wa klabu hiyo, Fred Felix Kataraia `Minziro’ na Msaidizi wake, Abeid Mziba `Tekelo’.

Kisa? Walimshambulia kwa matusi na kumtishia maisha msimamizi wa mchezo wa Ligi Kuu baina ya Prisons ya Mbeya na Moro United uliofanyika siku ya mwisho ya msimu wa ligi uliomalizika Aprili 26 mwaka huu huko Mbeya.

Kama si msimamo wa Sauko na wenzake, isingeweza kubainika kwamba kilichoelezwa na uongozi wa TFF katika kuwafungia viongozi hao hakikuwa na chembe ya ukweli.

Tungebaki kuandika kwenye kumbukumbu zetu kwamba, watu kama Sauko na wenzake ni wababe kwa viongozi wa soka nchini.

Ilibainika aliyetajwa hakuwa na mamlaka yoyote, bali `alitumiwa’ na wakubwa fulani ndani ya shirikisho kwenda kuwaharibia Moro United waliokuwa wanapigania uhai, kwani walikuwa wanachungulia shimo la kushuka daraja.

Kama si kupigana kiume na kushinda, hadithi ingekuwa nyingine kwani hata sare isingekuwa na maana kwao.

Pamoja na ushindi na furaha ya kubaki katika ligi, bado wakaadhibiwa kwa utovu wa nidhamu, lakini wao wakali na mtu anayeitwa Sunday Burton Kayuni (Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF), kuwa ndiye aliyetengeneza mambo yote haya.

Kayuni ninayemjua mimi, si huyu wa sasa anayeangushiwa kila aina ya lawama TFF. Sina hakika amebadilika lini, kwani tangu kijijini kwake Msia, barabara kuu itokayo Mpembe, Mbozi kwenda Ileje, Sunday ni mtu timamu.

Ni utimamu wake ndio uliomjengea heshima kubwa katika ukocha, akizipa mafanikio timu kadhaa tangu enzi za Sigara, Yanga, Mtibwa na hata AFC Leopards ya Kenya na Taifa Stars.

Kabla ya Sauko ya wenzake hayajasahaulika, Kayuni ametajwa tena (na Ismail Aden Rage) kutaka kuiharibia Tabora katika michuano ya Kombe la Taifa iliyoanza tena baada ya kusimamishwa kwa amri ya mahakama kutokana na pingamizi la Tabora iliyokataa kutolewa kafara kwa uzembe wa TFF.

Itakumbukwa kwamba, Tabora ilikata tiketi ya robo fainali kituo cha Dodoma , lakini ikapingwa kwa kumchezesha Haruna Moshi `Boban’ aliyepigwa kadi nyekundu katika mchezo wa kwanza katika kituo hicho.

Ingawa alikosa mechi moja kama kanuni zinavyoeleza, alizuiwa kucheza mechi nyingine hadi TFF itakapoamua, lakini Tabora waliingilia kati na kupata kibali cha Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Frederick Mwakalebela, ikiuruhusu mkoa huo kumchezesha Boban.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni bahati mbaya, mawasiliano ya msimamizi wa kituo na Mwakalebela `hayakuwa mzuri’, ikaonekana Tabora imedharau amri ya TFF na hivyo kung’olewa mashindanoni, nafasi ikaenda kwa Morogoro.

Wanyamwezi wakaja juu kudai haki yao . Na kweli, wamefanikiwa na kurudi tena mashindanoni.

Ya Kombe la Taifa nayo yamekwisha, lakini kwa kiasi kikubwa yameivunjia heshima TFF, kwa kuonekana ni watu wasio na umakini katika utendaji wao.

Tunaweza kuhoji mambo mengi, lakini itoshe tu kusema kwamba, ama TFF wamelewa madaraka kiasi cha kusahau majukumu yao na kujikita katika majungu na fitna, au wamelogwa ili wasijue wanachokifanya na hivyo kuharibi sifa nzuri ya utendaji waliyokuwa wamejijengea tena uongozi wa Rais wake, Leodegar Chilla Tenga uingie madarakani Desemba 31 mwaka 2004.

Tayari tumeshashuhudia madudu haya yakiongozana, lakini kama TFF hawatawekana chini kuyajadili haya, si ajabu tukashuhudia uozo mwingine, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: