Nape haifahamu katiba ya CCM?
KATIKA mdahalo wa wiki jana kwenye kituo cha ITV uliowakutanisha viongozi vijana watatu kutoka vyama vitatu vikuu vya siasa, tumejifunza mengi; na tumeweza kulinganisha uwezo wa vijana hao – John Mnyika (CHADEMA), Mtatiro Julius (CUF) na Nape Nnauye (CCM).
Hata hivyo, kwa tathmini ya haraka, Mnyika aliwazidi wenzake kwa hoja. Yeye na Mtatiro walimbana Nape hadi akatoa kauli inayozidi kukiangamiza chama chake.
Kwanza, alikiri kwamba vita ya ufisadi nchini illibuliwa na CHADEMA. Kwa mantiki hiyo, CCM haiwezi kujidai kwa kupiga vita ufisadi, kwa sababu jukumu kubwa ililo nalo ni kujitetea dhidi ya tuhuma za ufisadi ndani yake.
Maana yake ni kwamba, chochote kinachoitwa mapambano dhidi ya ufisadi ndani ya CCM, ni maigizo tu. Chochote kinachofanywa na chama hiki katika mapambano haya, ni mkakati wa makusudi wa kuwanusuru mafisadi ambao wananchi wanataka washughulikiwe.
Pili, Nape alikiri kuwa CCM kimejaa mafisadi. Alisisitiza kwamba orodha ya mafisadi wale 11 waliotajwa na Dk. Willibrord Slaa, 15 Septemba 2007 pale Mwembeyanga, Dar es Salaam, ni fupi sana.
Kwa maelezo ya Nape, ufisadi wa CCM unaanzia chini kwenye mizizi ya chama. Hawa waliotajwa ni vigogo tu, ambao hata hivyo ndio walioohusika na ufisdi mkubwa ulioliingiza taifa katika maafa.
Hoja ya Nape inapingana kabisa na kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, ambaye Mei 2010 alidai ndani ya chama chake hakuna mafisadi.
Ingawa wote ni viongozi waandamizi wa CCM, na kauli zao ni za chama chao; na kwa kuwa wametoa kauli zinazojikanganya na kupingana kuhusu suala lile lile; hii ya Nape ndiyo inachukuliwa kwa uzito zaidi kwa sababu inaendana na ukweli wa mambo; na imetolewa na mtu mwenye dhamana ya kueneza itikadi, mipango, kauli na matamko ya chama.
Mantiki ya kauli ya Nape, ndiyo inafafanua kwa sehemu kubwa, kwanini chama hicho kimeshindwa kuchukua hatua dhidi ya mafisadi wakubwa ambao kimekuwa kinawatuhumu.
Tunajua wazi kuwa jitihada za CCM zilikuwa za kujikosha, ili kupoza makali, kurejesha heshima yake iliyopotea na kuwanusuru watuhumiwa kwa mbwembwe.
Na kama si mmoja wa watuhumiwa hao, Edward Lowassa kusimama kidete, kumkumbusha Rais Jakaya Kikwete asili ya hoja hii – na kwamba naye (Kikwete) yu miongoni mwa mafisadi; na kama si ujadiri wa Lowassa kusisitiza naye alishiriki kuingiza nchi kwenye mkataba tata wa Richmond, huku akihoji tataribu za kichama zilizokiukwa katika kushughulikia suala hilo, CCM ingekuwa imefanya maigizo ya kufukuza watu kama mradi wa kujisafisha.
Hali hii ndiyo ilimfanya Nape ashindwe kueleza kwa kina msimamo wa chama chake kuhusu vita dhidi ya ufisadi; na ndiyo ilimsukuma katika kukianika chama chake kuhusu ufisadi uliokithiri kuanzia mashina hadi taifa.
Tukichunguza vema maana ya ndani ya kauli ya Nape, tutagundua kuwa CCM kimesimikwa katika nguzo za kifisadi – kama kweli kina ufisadi kuanzia mashina hadi taifa.
Maana yake ni kwamba hakuna wa kumfunga pakae kengele! Wote wameoza. Swali ambalo wengi wanajiuliza, ni kwa nini Nape anakitumbukiza chama chake kwenye mkenge?
Kushindwa kwa CCM kuchukua hatua kali, ndicho chanzo cha Nape kutapatapa hadi akatamka kuwa moja ya uamuzi mzito uliochukuliwa dhidi ya mafisadi ni kuivunja Kamati Kuu (CC) ya chama chake!
Lakini inajulikana wazi kuwa CC ilijiuzulu ili kumpisha mwenyekiti aiunde upya, baada ya lawama kwamba haikuwajibika vema kuleta ushindi wa kishindo mwaka 2010. Ilitokana pia na lawama za wanachama na baadhi ya viongozi dhidi ya katibu mkuu aliyekuwapo, Yusuph Makamba na sekretarieti yake.
Hivyo, kujiuzulu kwa CC ilikuwa njia ya rais kuitikia kishindo cha upinzani wa ndani kwa ndani dhidi ya uteuzi wake kwa Makamba, ambaye alikuwa analalamikiwa tangu alipoteuliwa na Kikwete mwaka 2006.
Kimsingi, kitendo hicho hakikuwa ushindi kwa Kikwete bali ushindi kwa wapinzani wake, ambao wamekuwa wakilalamikia uteuzi wake usioridhika wa viongozi katika nafasi nyeti ndani ya chama na serikali.
Hivyo, haikuwa sahihi kwa Nape kujisifu, kwamba hatua hiyo ilikuwa moja ya utekelezaji wa mkakati wa kupambana na ufisadi ndani ya chama.
Na kama hilo alilosema ni kweli, basi maana yake ni kwamba kamati kuu ilikuwa ya mafisadi; kama kamati kuu ilikuwa ya mafisadi, CCM kimekuwa kinaongozwa kifisadi, na yote yaliyosimamiwa na kamati kuu hiyo ni ufisadi mtupu.
Je, hii maana yake nini? Nape ametoa shitaka kubwa sana dhidi ya chama chake. Amethibitisha kile ambacho wazee wa chama chake, kina Kingunge Ngombale-Mwiru na Mukama wamewahi kukana huko nyuma.
Lakini yote hiyo imetokana na kuelemewa kwa hoja kutoka kwa vijana wenzake. Alitumia asilimia karibu 60 za muda wote kujitetea, na nyingine 40 kushambulia wenzake, badala ya kujenga hoja.
Na wakati akifanya hivyo, wenzake walikuwa wakijenga hoja kwa kutumia matukio ya kweli yanayofahamika. Alishindwa hata kukubaliana na wenzake juu ya ubovu wa katiba iliyopo katika vipengele kadhaa, ili apate pa kuanzia kujenga hoja yake.
Badala yake, aliishia kushambulia vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo vinajitapa kwa kuwafukuza uanachama na ubunge Hamad Rashid Mohammed na David Kafulila.
Katiba ya Tanzania, kutokana na ubovu wake, haizungumzii hatima ya mwanachama kufukuzwa, hasa akiwa pia ni mbunge. Badala yake inaongelea mwanachama kuacha kuwa mwanachama (si kuachishwa au kufukuzwa), kujiuzulu mwenyewe, pamoja na sababu nyingine.
Hii ingewapeleka kina Mnyika, Dk. Sengodo Mvungi, Mtatiro kwenye mjadala wa katiba ya nchi zaidi; na hivyo Nape kupata ahueni hadi kipindi kiishe.
Nape akitulia ni mzuri. Tatizo lake anajichanganya na kupoteza muda katika propaganda badala ya hoja.
Kwa mfano, alisahau kwamba katiba ya CCM katika ukurasa wa wa 125, ibara ya 110 inazungumzia juu ya kazi za kamati kuu ya CCM, ambayo ameisifia sana kwamba ilijiuzulu; na kusababisha kuundwa kwa kamati kuu nyingine.
Katika ibara ya 110, sehemu ndogo ya 7 Katiba ya CCM inasema hivi kuhusu kazi za kamati kuu:
"Kumsimasisha uongozi kiongozi yeyote isipokuwa mwenyekiti wa CCM na Makamu wa mwenyekiti endapo itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za uongozi."
Hoja zake kuhusu vikao na kufuata taratibu, ingeeleweka kama kamati kuu ingechukua uamuzi wake, mfano iwapo wahusika wanakata rufaa, vinginevyo kamati kuu ya CCM ilitakiwa baada ya kujiridhisha, kukamilisha jukumu hilo la kuwavua magamba wanachama iliyodhamiria kuwashughulikia April 2011, kwa azimio kwamba hawana sifa za uongozi, kwa mujibu wa katiba.
Vinginevyo aelezee umma kwamba, wanachama hao wana nguvu kuliko wale ambao katiba inasema hawawezi kuvuliwa madaraka – mwenyekiti na makamu wake.
- Login or register to post comments