Nape: Sauti ya upweke nyikani


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version

PROPAGANDA ni njia ya kuuza chako, kukieneza, kukithaminisha. Hapa tunajadili itikadi katika siasa. Uhai wa vyama vya siasa, pamoja na mipango thabiti na mikakati, hutegemea pia idara, ama ya propaganda au ya uenezi wa itikadi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa miongo mitatu ya uhai wake pamoja na miongo miwili ya vyama vya awali, kilikuwa makini sana kuteua watu wa kuongoza idara hii.

Kwanza, viongozi wakuu wa chama hiki, tukianza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mpaka wakati wa Benjamin Mkapa, walikuwa wao wenyewe mahiri katika kufanya propaganda dhidi ya maadui wa chama ndani ya chama, ndani na nje ya nchi.

Ukiangalia kauli mbiu za wakati wa Nyerere - hasa wakati vita baridi na vita dhidi ya maadui watatu wa taifa letu, utagundua kuwa yeye mwenyewe alikuwa mwana propaganda aliyebobea.

Aliweka msingi kwa makada waandamizi katika kuandaa majarida na machapisho mbalimbali kwa ajili ya kuelimisha umma juu ya siasa na itikadi ya chama tawala.

Ni wakati huo, makada kama Kingunge Ngombale Mwiru, Daudi Mwakawago, Joseph Mbwiliza, Wilson Mukama na Moses Nnauye walikomazwa kwa kudaka upesi fikra za Mwalimu na kuzitumia kuelimisha umma.

Kupitia propoganda zao maadui wa ndani walitishwa na uhamasishaji; lakini pia maadui wetu wa kweli na wa kufikirika walipata ujumbe kamili bila kubuni.

Nakumbuka wakati ule Kamuzu Banda wa Malawi, Idd Amin wa Uganda, Makaburu wa Afrika Kusini na Wareno waliokalia baadhi ya nchi za kusini na Magharibi wa Afrika, walivyoimbwa na kuchafuliwa mbele ya mataifa mengine.

Wakuu waliopita wa Idara ya Propoganda au Itikadi na Uenezi na Siasa za CCM, waliacha sifa ambayo wanaoteuliwa siku hizi wanapata taabu sana kuvaa viatu vyao na kuonekana wanafanya kazi.

Akina Kingunge Ngombale-Mwiru, David Mwakawago na Moses Nnauye watakumbukwa daima ndani ya CCM iliyokuwa inatukuka wakati huo.

Hivi sasa tunaye kijana Nape Nnauye anayeiongoza idara hiyo. Kuna wanaolalamika juu ya utendaji kazi wake.

Ni vigumu kujua kijana huyu anafanya kazi za mezani saa ngapi, anasoma majarida na vitabu saa ngapi, na anajiandaaje kuongea na umma saa ngapi.

Ni rahisi kumlalamikia Nape kuliko kumsaidia. Kwani kijana huyu yuko katika mazingira tofauti. Ni nyakati nyingine kabisa.

Wazee waliotajwa hapo juu ama wamekufa au wamekwisha nguvu. Wengine ni wastaafu au wapowapo. Kizazi kipya cha kuzalisha hoja motomoto hakionekani.

Lakini hata hili lina sababau zake. Miaka 50 ya utawala wa chama kimoja haumomonyoi miili tu; unamomonyoa akili na uwezo wa kufikiri.

Kama hakukuwepo na mrithishano wa fikra na hasa fikra zinazokua na kunyumbulika; zile fikra endelevu zinazozaa matunda mema wakati wote, basi itafika wakati kutatokea mkwamo.

Nilipoongea na Nape alidai, mwenyekiti amelalamika kuwa wapinzani wanaachwa wanapotosha ukweli, kwa hiyo inabidi wajibiwe.

Akasema hata ndani ya CCM kuna wapinzani wanaostahili kushughulikiwa. Huyu hakika hafanani na baba yake, Moses Nnauye, lakini ni katika mazingira tofauti kabisa.

Leo hii kuna fursa kubwa ya kutoa kauli. Kuna vyama vingi vya siasa. Tena leo hii kuna vyama ambavyo vimejidhihirisha kuwa makini zaidi.

Tuseme hivi, kuna vyama vyenye uwezo wa kufikiri na kupanga na ambavyo vina mikakati ya kukamatana na chama kikubwa, cha zamani, chenye mizizi na kuweza kukitikisa.

Tangu huko nyuma, CCM na hata Tanu, vilikuwa vyama pekee. Aidha, vilikuwa vyama dola. Kumomonyoka kwa nguvu zake, hata kama siyo sana, kutokana na kuwepo uhuru wa kuwa na vyama vingine, kumejenga mazingira tofauti.

Wizi, ufisadi, rushwa, kutojali, kuchukulia kila kitu kwa mazoea tu na kuona kila mmoja hana akili isipokuwa wenye chama kizee; vyote hivi vimeiweka CCM mahali pabaya.

Kimeshiba sana kwa ulafi na kuvimbiwa. Hakiwezi hata kujiamsha; mpaka kiamshwe kwa bakora – na wanachama wake na wale wa upinzani.

Katika mazingira haya, ambamo upinzani unachukua nafasi yake, lazima CCM nayo ichukue nafasi yake mpya: ile ya upinzani.

Kwani hoja za kujenga wanazo wapinzani. Hoja za kuleta nafuu wanazo wapinzani. Hoja za kuondoa wizi, ufisadi, rushwa na kutojali ziko upinzani.

Si hayo tu. Wananchi, hata wanachama wa CCM wamechoka kusubiri mabadiliko. Katika miaka 50, wengi wamekufa wakitamani kuona mafanikio lakini hayaji. Leo waliobakia wanasema, “…potelea mbali; tushiriki huku ili tuone kama tutaona mabadiliko tukiwa hai.”

Hapa lazima CCM iwe kwenye upande wa upinzani. Ujogoo wake umepwaya na unaisha polepole kadri upinzani unavyokata mbuga kueleza kuasi mfumo uliowatelekeza.

Kwa hiyo badala ya CCM kuongoza na kuonyesha njia, sasa chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaongoza na CCM inafuata.

Hapa ndipo katibu mwenezi wa CCM, Nape Nnauye anapata shida. Kwanza, anaonekana kuwa peke yake. Wengine wamebakia kucheka na kuandaa utaratibu wa “kugawana mbao” baada ya kuona banda linabomoka.

Ni hapa pia Nape anakuja na nadharia nyingi. Laini na ngumu. Anakuja na misemo na hata kaulimbiu nyingi, hata zinazokinzana. Ni sauti iliayo nyikani!

Atakamata kujivua gamba. Akisikia CHADEMA wamekuja na “vua gamba, vaa gwanda,” naye anatafuta kingine.

Hapo anakuja na “vua gamba, vaa uzalendo.” Katika haraka ya kujibu wapinzani anajikuta ameharibu alichokusudia.

Kwani ukivua gamba, ambalo kwa sasa ni maarufu kama vazi la kijani na njano na ambalo ni CCM – ukavaa uzalendo, maana yake ni kwamba wanachama wake siyo wazalendo.

Kuna walioanza kumkebehi kuwa Nape  amesema CCM yote, inayovaa kijani na njano, haina uzalendo. Hii siyo maana aliyokusudia Nape, bali ni maana inayosikika masikioni mwa wasikilizaji wa Nape.

Kijana huyu haonekani kuchoka lakini pia kuwa na msaada wa karibu wa vichwa vyenye kufikiri haraka na kuweka kila kitu sawa. Ni kama amesuswa. Na anaweza kuwa amesuswa.

Sasa amekuja na hili la wanaohama CCM kwenda upinzani ni “oili chafu.” Oili huwekwa ndani ya injini ya mitambo na huwa na matumizi ya muda fulani, kisha humwagwa na kuwekwa nyingine. Hivyo hakuna oili ya kudumu ndani ya mashine.

Kijana Nape anafukuzia wapinzani. Wakisema hili anawajibu kwa lile. Wakienda Jangwani mkutanoni, naye anawafuata.

Wazee wa chama wako kimya. Vijana wanaota kugawana mbao. Walafi wanaendelea kumung’unya nchi na utajiri wake.

Hawezi kusimamisha upya nguzo za CCM zilizodhoofika na paa lake linalodondoka. Afadhali kubomoa. Tutajenga upya.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: