Nassari: Hoja ya ardhi ilinipa ubunge


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

TAREHE 2 Aprili 2012 kulikuwa na kila aina ya hoi hoi na shangwe katika viunga mbalimbali vya jimbo la Arumeru Mashariki baada ya msimamizi wa uchaguzi mdogo, Trasias Kagenzi kumtangaza Joshua Nassari wa CHADEMA kuwa mbunge mpya.

Wanachama na wafuasi wa chama hicho waliimba “People’s Power (Nguvu ya Umma)”

Shangwe kama hizo zilisikika pia kwenye viwanja vya Barafu mjini Dodoma wiki iliyopita baada ya Nassari pamoja na mbunge mwingine wa Viti Maalumu, Cecilia Daniel Paresso aliyechukua nafasi ya Regia Mtema aliyefariki kwa ajali ya gari maeneo ya Ruvu, Pwani.

Huko wafuasi waliimba “Freedom is Coming” yaani ukombozi unakuja) na “CCM bye bye” wakimaanisha kuwa Chama Cha Mapinduzi kwaheri.

Japo nguvu hiyo ya umma ndiyo ilimsaidia mtoto huyo wa tano kati ya watoto wanane wa mchungaji, Samuel Nassari kushinda kiti hicho cha ubunge kilichoachwa wazi na hayati Jeremiah Sumari, Nassari anasema hoja ya ardhi ilikuwa turufu yake.

“Nilijenga vizuri hoja ya ardhi na CCM waliona hatari ya hoja hiyo ndipo wakaanza kutoa ahadi mbalimbali za kumaliza kero ya ardhi Arumeru Mashariki,” anasema Nassari.

Kijana huyo anasema, “…hilo halikuwezekana kwa sababu CCM hawaaminiki, wananchi wamewakataa kwa sababu wameongoza kwa muda mrefu…”

Alisema sababu za CCM kutoaminika ni kutokana na ukweli kwamba wamekaa miaka 50 – miaka 35 ya CCM na miaka 15 ya TANU – bila kutatua tatizo hilo la ardhi.

“Wanaarumeru waliona CCM inawadanganya tu, hivyo hawakutaka kudanganyika, hawakuichagua CCM,” alisisitiza.

Mbunge huyo anayetajwa kuwa ni jembe jipya ndani ya CHADEMA alisema kwa kadri alivyojenga hoja kuhusiana na tatizo la ardhi na alivyopata mwitikio mkubwa katika jimbo zima wananchi wa Meru wangeshangaa kama yeye asingetangazwa mshindi wa ubunge wa jimbo hilo.

Anasema kwamba watu wa Meru hawakuangalia nguvu ya rasilimali watu na fedha ambayo CCM waliiweka ikilinganishwa na vyama vingine hususan CHADEMA.

Kuhusu ushindi huo Nassari anasema, “Ushindi wangu Arumeru Mashariki ni ushindi wa CHADEMA na hii ni ishara kwamba siku za CCM kuongoza taifa zinazidi kupungua.”

Katika uchaguzi huo uliokuwa na msisismo mkubwa Nassari alipambana na wagombea wengine maarufu hasa Sioi Sumari wa CCM aliyekuwa anawania kurithi kiti hicho kilichoachwa wazi na baba yake Jeremiah Sumari aliyefariki dunia 19 Januari 2012 kutokana na saratani ya ubongo.

Katika uchaguzi huo, Nassari alivuna kura 32,972, Sioi alipata kura 26,752 huku Abdallah Mazengo wa AFP akiambulia kura 139.

Wengine ni Mohamed Mohamed wa DP kura 77, Hamis Kiemi wa NRA kura 35, Shabani Kirita wa SAU kura 22, Chipaka Moova wa TLP kura 18 na Charles Msuya wa UPDP kura 18. Kura 661 zilizoharibika.

Ingawa waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ni wapigakura 127, 455 waliopiga kura walikuwa 60,699, nusu ya waliojiandikisha.

Katika mahojiano hayo Nassari anasema kuwa ushindi wa Arumeru Mashariki ni kipimo cha namna wananchi wasivyoridhika na watawala, mgawo wa ardhi na shida ya maji.

Anasema walichotaka wananchi wa Arumeru kwa sasa ni kusikia jinsi mgombea Nassari anavyonadi sera zinazolenga kutatua matatizo yanayowakabili ambayo CCM imeshindwa kutetea kwa miaka yote iliyotawala.

“Tatizo la CCM na viongozi wake wastaafu wanajadili watu. Na mbaya zaidi husema uongo kitu ambacho si uadilifu na si suluhisho la  matatizo ya Wanaarumeru na Watanzania kwa ujumla,” anasema.

Nassari amesema kushinda ni jambo moja na kutimiza matakwa ya Wanaarumeru ni jambo jingine, kwamba sasa anatakiwa kufanyia kazi changamoto mbalimbali.

Changamoto zinazomkabili ni pamoja na kupatia ufumbuzi matatizo ya ardhi, maji na elimu na kuanzisha mfuko wa maendeleo wa vijana na wajane.

Tayari Nassari ambaye aliapishwa wiki iliyopita mjini Dodoma, ameanza kazi rasmi kwa kuchimba visima viwili vya maji katika Kata ya Mororoni.

Kuhusu ardhi anasema kazi kubwa ni kuhakikisha kuwa anasimamia mgawo wa ardhi unaozingatia haki na hilo anatambua ya kuwa ni changamoto kwake.

“Mimi sasa ni sauti ya wananchi waliofukarishwa na mfumo mbovu wa kugawa ardhi ulioanzishwa wakati wa ukoloni na kuendelezwa chini ya uongozi wa TANU na CCM,” anasisitiza.

Alipoulizwa kama ataweza majukumu ya ubunge, Nassari alijibu, “Ndiyo nitaweza. Nilianza na Mungu, nakwenda na Mungu na nitamaliza na Mungu.”

Majukumu yake mengine yatakuwa kuwakilisha vema wananchi wa Arumeru Mashariki katika bunge ambalo lina majukumu ya kutunga sheria na kuisimamia shughuli mbalimbali za serikali.

Akaongeza, “Ushindi wa Arumeru Mashariki ni ujumbe kwa watawala kwamba wamechokwa. Na usisahau kuona kwamba CHADEMA inakubalika kwa akina mama na vijana ambao wengi wamejiandikisha na kwamba kutakuwa na mabadiliko makubwa uchaguzi ujao wa 2015.”

“Tutawaondoa madarakani kwa sababu wananchi wamekasirishwa, hasira ambayo fedha haiwezi kununua wala kuzuia,” alieleza.

Anasema kutokana na hasira yao wananchi sasa hawana hofu ya matusi wala vitisho  bali wamedhamiria kwa dhati kubadili upepo wa sasa kwa sababu CCM wameshindwa kutoa huduma bora kwani Watanzania wengi ni maskini na wamefukarishwa na ufisadi ambao umelelewa.

Alisema tathmini inaonyesha CHADEMA inafanya vema ndani ya bunge na nje ya bunge hivyo watu wana imani na chama hiki na kinategemewa kufuta machozi ya wananchi kutokana na matatizo ya muda mrefu hasa suala la ardhi.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: