NEC na uparaganyaji siasa KigomaUjiji


Anthony Kayanda's picture

Na Anthony Kayanda - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version

JIMBO la Uchaguzi la Kigoma Mjini limekuwa na upinzani mkubwa kisiasa unaohusisha vyama vya CCM na CHADEMA kwa kipindi chote tangu mfumo wa vyama vingi uliporudishwa mwaka 1992.

Ushindani ulianza kwa CCM kushikwa koo na Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) kilichokuwa kikiongozwa na Chifu Abdallah Fundikira.

Lakini ghafla, mwaka 1993, CHADEMA kilichukua nafasi na kuanza kusumbua CCM. Hadi leo hii, CCM inaendelea kukabiliwa na ushindani wa nguvu kwa CHADEMA.

Vyama hivi vinapokezana uongozi kwenye ubunge na udiwani, pamoja na Meya wa Manispaa.

Ushindani wao umeibua sura ya kushangaza pale wachambuzi wanapotafakari maamuzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kugawa nafasi za viti maalum vya udiwani kwa vyama hivi.

Lipo swali muhimu linaloulizwa: Ni maamuzi yepi ya Tume yalikuwa sahihi – yale iliyoyafanya baada ya uchaguzi mkuu wa 2005 au 2010 – katika kupitisha madiwani wa viti maalum wa Manispaa ya Kigoma Ujiji?

Mwaka 2005, Manispaa ya Kigoma Ujiji ilikuwa na kata 13 kimuundo wakati mwaka 2010 ziliongezeka na kufikia kata 19.

Katika uchaguzi wa 2005, CHADEMA ilishinda udiwani kata saba dhidi ya sita za CCM, chama ambacho pia kilishinda mbunge jimbo la Kigoma Mjini, kikiwakilishwa na Peter Serukamba. Kisheria, mbunge pia huwa mjumbe Baraza la Madiwani.

Kwa hivyo, CCM iliingiza wajumbe saba katika Baraza la Madiwani bila ya kujumlisha wa viti maalum ambao idadi yao miaka yote kuanzia 1995 ulipoanza uchaguzi wa vyama vingi, wamekuwa ni watano tu.

Katika uchaguzi mkuu wa 2000, CHADEMA ilishinda kata nane na ikapata pia mbunge Kigoma mjini, Dk. Aman Walid Kabourou. CCM ilishinda kata tano.

Katika mgawanyo wa viti maalum vya udiwani, CCM ilipata wajumbe wawili wakati CHADEMA ilipata watatu.

Kwa kupima yanayotokea na kuamuliwa na Tume, ndipo inapokuja hoja: Maamuzi ya Tume yamefuata kanuni za mgawanyo au yamepindisha kanuni?

Laban Tanda, aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, alitangaza kuwa kila chama kimepata nafasi tatu za viti maalum. Tangazo hilo lilizua tafrani kubwa na kuleta kitu kipya katika historia ya kisiasa ya eneo hili.

Kwa kuwa CCM na CHADEMA walikuwa na idadi sawa ya madiwani – kumi – kuliamuliwa utaratibu mgeni wa vyama kuongoza manispaa kwa kupokezana. Meya aliyetoka chama A ataongoza kwa miezi 30 (miaka miwili na nusu) na kumpisha Meya wa chama B kumaliza kipindi kama hicho kabla ya kuingia uchaguzi mpya.

Tukio la kwanza lilikuwa ni kitendo cha Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kigoma mjini, Nashon Bidyanguze kutuhumiwa kujaribu kumtorosha aliyekuwa diwani wa Viti Maalum wa CHADEMA, Bahati Rehani, na kumpeleka jijini Dar es Salaam wakati upigaji kura ya kuchagua meya ukiwa tayari.

Jaribio hilo lilikwama baada ya taarifa kuvuja; viongozi wa CHADEMA waliweka mtego kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam ambako walifanikiwa kumshika Bidyanguze akiwa pamoja na diwani Bahati.

Diwani huyo alirudishwa Kigoma ili apige kura kuchagua Meya. Upigaji kura wenyewe ulijaa matatizo. Kila kura zilipopigwa, washindani walifungana kwa kura 10.

Hali ilivyokuwa ngumu, Mizengo Pinda, wakati huo 2006 akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), alilazimika kwenda Kigoma kusaidia ufumbuzi wa mvutano wa kumpata meya.

Muafaka ukafikiwa kuwa vyama hivyo vigawane vipindi vya uongozi na ndipo ndoa rasmi ya kisiasa ikihusisha vyama hasimu, ilipofungwa.

Ukaja uchaguzi wa 2010 safari hii kata zikiwa ni 19. CHADEMA ilishinda kata kumi huku CCM ikishinda tisa na mbunge wake, Serukamba, akatetea kiti.

Cha kushangaza Msimamizi wa Uchaguzi Kigoma Mjini, Lewis Kalinjuna, alitangaza mgawanyo wa madiwani wanne wa viti maalum kwa CHADEMA na CCM watatu.

Mgawanyo huo ulikuwa tofauti na ilivyokuwa 2005 japokuwa mazingira ya ushindi yalifanana. Sasa iweje, katika mazingira yaleyale Tume iamue tofauti?

Mwaka 2005, CHADEMA walikwenda mahakamani kupinga maamuzi ya Tume kuongeza diwani mmoja wa viti maalum kwa CCM, ingawa pingamizi lao lilitupwa na Mahakama ya Wilaya.

Mambo yaligeuka 2010. Tume iliwapa CHADEMA nafasi nne za madiwani wa viti maalum na CCM nafasi tatu, jambo lililowafanya waende mahakamani kupinga maamuzi hayo.

Mahakama ya Wilaya Kigoma ilitupa pingamizi la CCM lililotaka iongezewe nafasi moja kama ilivyokuwa 2005 vyama hivyo vilipozidiana kwa diwani mmoja wa kuchaguliwa.

Wanaochambua mwenendo wa siasa Kigoma Mjini wanajiuliza nini chimbukoa la yanayotokea. Ufundi katika kuchakachua (CHADEMA 2005 na CCM 2010) au ni matokeo ya utawala usiofuata sheria na kanuni?

Siasa zinahitaji utawala mzuri kama ilivyo kwa kitu chochote kile katika maisha ya mwanadamu. Iwapo kila taasisi itatoa huduma kwa kuzingatia sheria na kanuni itaepusha Kigoma kutumbukia katika balaa la machafuko kwa kuwa vyama vinavutana sana.?

0785 788727
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: