Ngeleja anapiga porojo tatizo la umeme


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja ameshindwa kazi. Tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo, Februari 2008, Ngeleja ameshindwa kushughulikia ipasavyo suala la uhaba wa umeme linalolikabili taifa.

Tayari baadhi ya wabunge wanasema, “Ngeleja ni chanzo cha matatizo ya umeme kwa sababu sera na mipango yake havitekeleziki. Wanamtaka aachie ngazi.

Ushahidi ni huu. Juni 2008 Ngeleja aliutangazia umma “tatizo la uhaba wa umeme litakwisha ndani ya miaka miwili ijayo.” Halikwisha.

Desemba 2010 alitembelea mradi wa kuzalisha gesi wa Songo Songo, Kilwa Kisiwani unaotekelezwa na kampuni ya Pan African Energy. Alisema tatizo la umeme litakuwa historia ifikapo mwaka 2013 kwa vile serikali itakuwa na uhakika wa kuzalisha megawati 900 kutoka vyanzo mbalimbali.

Lakini mpaka sasa, mgawo uko palepale.Zipo sababu nyingi zinaleta mgawo wa umeme. Lakini kubwa inatajwa kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa yanayozalisha umeme.

Kisa: Ngeleja hajalieleza ukweli. Hajasema kiini cha mgawo ni serikali kufanya maamuzi ya hovyo katika mambo ya msingi. Hajaeleza kwa mfano, suala la upungufu wa gesi asilia inayozalishwa kutoka Songo Songo, wilayani Kilwa mkoani Lindi, litakuwa endelevu ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kukarabati visima hivyo vya gesi.

Gesi hiyo ni mali ya serikali. Iligunduliwa na Shirika la Maendeleo ya Mafuta la taifa (TPDC) miaka ya 1980. Lakini uendeshaji wake ambao unahusisha uchimbaji pamoja na usafirishaji kutoka Kilwa hadi jijini Dar es Salaam unafanywa na kampuni ya Songas ya Canada kupitia kampuni ya Pan African Energy Tanzania.

Habari kutoka ndani ya TANESCO zinasema kuna visima kadhaa vya gesi vinaelekea kufa kwa vile havijafanyiwa ukarabati wa nguvu.

Tatizo ni uzembe wa mkandarasi - kampuni ya Pan African Tanzania Energy ambayo inabebwa na Songas. Tayari visima vitano kati ya 10 vinavyozalisha gesi vimechakaa na kuota kutu, huku mabomba ya gesi yaliyopo ardhini nayo yakiwa hatarini kupasuka. Kiasi cha dola za Kimarekani 450,000 zinahitajika kwa ajili ya kukarabati kisima kimoja cha gesi.

Visima hivyo ambavyo vimepewa majina ya “SS” awali vilikadiriwa kutumika kwa miaka 50 mpaka kwisha kwa gesi yake.

Lakini sasa kutokana na kutu hiyo kisima “SS 3” kinaweza kuzalisha kwa miaka 13 tu; kisima “SS 4” hadi miaka sita tu; kisima “SS 5” kimeharibika kabisa, kwa maana hiyo hakitoi gesi tena.

Kisima “SS 7” kina uwezo wa kuzalisha kwa miaka 16 tu, na kisima “SS 9” mwaka mmoja tu.

Kwa miaka kadhaa kampuni hii imekuwa ikiahirisha zoezi la kuviokoa visima hivyo. Hata juzi ilipotoa matangazo ya kuvifanyia ukarabati, hakuna lolote lililofanyika. Ndiyo msingi wa TANESCO ilitangaza mgawo kwa siku saba lakini ukageuka kuwa wa mwaka!

Aidha, kuna madai ya kuibuka mgogoro kati ya TPDC na Songas. TPDC inadaiwa haimtaki mkandarasi Pan African anayeshirikiana na Songas kuendesha shughuli za uchimbaji gesi.

Ngeleja amekiri kuharibika kwa baadhi ya visima hivyo lakini amejigamba kuwa serikali inalifanyia kazi. Ni majigambo yaleyale.

TANESCO inakabiliwa pia na kibarua cha kukarabati mitambo yake ya kuzalisha umeme wa maji. Mbali ya uchakavu wa mitambo ya maji, kumepungua kwa mvua katika mikoa yaliko mabwawa ya kuzalisha umeme, na tatizo la kujaa tope baadhi ya mabwawa kama Mtera, kumepunguza uwezo wa TANESCO kuzalisha umeme.

Mabwawa ya maji yana uwezo wa kuzalisha megawati 773, lakini kutokana na matatizo hayo sasa yanazalisha umeme usiozidi megawati 400.

Nayo mitambo inayotumia gesi ina uwezo wa kuzalisha megawati 225. Lakini kutokana na uchakavu wa mitambo ya kusafirisha na kuzalisha gesi kutoka Songosongo, mitambo ya Songas yenye uwezo wa kuzalisha megawati 180, sasa inazalisha kati ya megawati 80-100.

Mtambo wa Tegeta wenye uwezo wa kuzalisha megawati 45, sasa unazalisha megawati 25. Mtambo wa Dowans/Symbion wenye uwezo wa kuazalisha megawati 100, hivi sasa unazalisha megawati 60.

Mitambo inayozalisha umeme wa IPTL inayomilikiwa na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ina uwezo wa kuzalisha 100. Sasa unazalisha megawati 10 tu. Ngeleja alijigamba serikali imetoa fedha za kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL.

Lakini fedha zilizotolewa haziwezi hata kuendesha mitambo hiyo kwa nusu mwezi.

Tatizo ni Ngeleja. Hasimamii jambo moja kabla ya kuanza jingine. Anataka kubeba yote kwa wakati mmoja.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: