Ngeleja, Jairo hawahitajiki wizarani


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MWANZONI mwa miaka ya 1980 wakati huo nikiwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mvuha, wilayani Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro kilitokea kituko cha mwaka kama siyo cha karne.

Kilikuwa kipindi cha sikukuu ya Kiislamu. Vijana wawili walikunywa pombe nyingi mapema asubuhi kabla ya saa 5.00 kusherehekea sikukuu ile.

Baada ya kuuchapa mtindi, vijana wale waliingia ndani kulala asubuhi ile huku wakiwaacha wake na wapenzi wao nje wakiendelea na maandalizi ya mapishi kwa ajili ya sikukuu.

Muda wa kati ya saa 9.00 na 10.00 alasiri mmoja wa vijana wale aliamka na kwa kudhani ni usiku, akawasha kibatari na kutoka nje uchi wa mnyama akienda chooni huku akikinga kibatari kwa mkono wa kushoto kuzuia upepo kisizimike!

Akidhani ni usiku wa manane, jua alilokuta nje likiwaka alidhani ni mbalamwezi, alielekea chooni huku akina mama waliokuwa wanapika ukumbini wakikimbia na kutawanyika kulia na kushoto.

Pale ukumbini alibaki mke wake akiwa mdomo wazi, akishangaa kilichomsibu mumewe hadi kuamua kutoka nje ya nyumba yake uchi, tena mchana akiwa ameshika kibatari.

Hayo ndiyo matatizo ya ulevi. Ulevi wa namna hii hadi kutoka nje uchi mchana na kibatari, ndio unaoweza kulinganishwa na kitendo cha Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na katibu mkuu wake David Jairo “kushangilia ushindi baada ya Jairo kurejeshwa kazini na Katibu Mkuu kiongozi, Philemon Luhanjo.”

Kukumbatiana na kushangilia wakapigwa picha, Ngeleja na Jairo walikuwa wametoka nje uchi mchana wa jua kali. Ngeleja alijishushia hadhi hadi akaacha shughuli za Bunge mjini Dodoma akatimka mbio kwa spidi kwenda Dar es Salaam kumpokea na kumshangilia Katibu Mkuu wake.

Jairo alikuwa anakabiliwa na tuhuma za kuchangisha fedha kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini kwa lengo la kuzitumia fedha zilizochangwa kushawishi wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo kwa urahisi.

Tunasema lengo la kuchangisha fedha hizo lilikuwa baya na hatusubiri Kamati ya Bunge itoe matokeo ya uchunguzi wake kwa sababu tunafahamu fedha za serikali hutolewa na kutumiwa baada ya kuombwa na kutolewa kwenye bajeti.

Sasa kama fedha zilitolewa kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge kuwa zitumike kwenye taasisi fulani kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, madarasa, mafunzo, safari za wakuu wake au hata manunuzi ya vifaa zikichangwa na kutumika kushawishi wabunge maana yake ni kwamba zimeibwa.

Hakuna sababu yoyote ya Waziri mzima kupaparika na kukimbilia kumpokea ofisa wa chini yake na kumpongeza kwa maua na vitambaa vyeupe na wakapiga picha kushangilia huku wafanyakazi wao wakiimba kuwa wameshinda. Je, ulikuwa ushindi dhidi ya nani?

Wafanyakazi wa wizara ya nishati na madini hawakuona ubaya wowote kwa fedha kuchangwa wakapelekewa wabunge kwa sababu yoyote ile kwa kuwa hakuna fedha iliyotoka wizarani kwao.

Na kwa sababu wafanyakazi wa Nishati na madini wamezoea kuambulia makombo yanayotolewa na wezi wanaoitwa wawekezaji katika sekta ya madini, wanyama pori na gesi basi kwao wao wazuri ni wakubwa wao wanaowashirikisha ubadhirifu wa mali ya umma.

Wafanyakazi wa Nishati na Madini hupata posho katika hizo semina elekezi za kuweka mikakati ya kuondoa kero ya umeme, kukamilisha mipango ya muda mrefu na ya muda wa kati ya kukabiliana na tatizo sugu la nishati na hata mpango mkakati wa sekta ya nishati nchini! Upuuzi mtupu usioleta umeme.

Wafanyakazi hawa wanajua jinsi mikataba ya kifisadi inavyotiwa saini kwenye hoteli za Ulaya huku Waziri Mkuu akiwa amelala hotelini humo kama ule wa Buzwagi. Kwa nini wao wawe na uchungu wakati wakubwa nchini hawana uchungu?

Kitendo cha Ngeleja kujisahau hadi akaenda kumfungulia mlango Jairo wakati Jairo ndiye anayepaswa kumfungulia mlango yeye kinajieleza kwa nini hakuna umeme Tanzania na hautakuwepo hadi Ngeleja na Jairo watakapoondoka Nishati na Madini.

Kitendo hiki kinanikumbusha zamani wakati nikichunga mbuzi kule Ukuryani katika vijiji vya Nyamongo, Tarime. Tukiwa watoto tulikuwa na mtindo wa kuimba wimbo wa kushangilia kama mbuzi wa mtu fulani wakivamia shamba la jirani yake na kuharibu mazao.

Badala ya kuwaondoa mbuzi shambani wasiharibu mazao ya jirani, sisi tuliimba kwa sauti ya juu: “koleleee kolikolikooo, tiga chitoleee nawe alatolaaa. Koleleee kolikolikooo, tiga chitoleee nawe alatolaaa.”

Maana ya wimbo huu kwa lugha rahisi ni kwamba shambani kwa mtu anayeitwa Lele kulikuwa kunafanyika shughuli tuliyoiita kolikolikooo ambapo mbuzi wanaharibu mazao yaani kutola, nawe alatola maana yake naye mchungaji anashiriki kutola yaani kuharibu mazao.

Huu ulikuwa wimbo wa watoto watukutu kushangilia uharibifu wa mazao kwenye shamba la Kolele na uzembe wa mwenzetu asiyekuwa makini katika uchungaji wa mbuzi ambaye naye alishiriki kutola.

Hapa Jairo ndiye anachukua nafasi ya mbuzi wanaotola mazao ya Watanzania na mchungaji wa mbuzi ambaye badala ya kuwaondoa mbuzi shambani yeye anashiriki kutola mazao yetu ni Ngeleja!

Nasema haya kwa sababu badala ya Ngeleja kubaki Dodoma akasubiri matokeo ya uchunguzi upelekwe bungeni yeye alitumia shangingi lake la kiwaziri, dereva akalipwa posho naye akajilipa posho wakatimka hadi Dar es Salaam kushangilia mtuhumiwa kurejeshwa kazini aendelee kuwaandikia posho zingine!

Na mwisho, ‘kila mfuga kuku vioja huviona.’ Msemo huu wa Waswahili unamaanisha kuwa yeyote anayefuga kuku ataona matukio mengi yakihusisha wezi (binadamu), mburukenge, vicheche, fungo, nunda na hata nyoka walao kuku wake.

Msemo huu ndio unaofaa kutumika Tanzania ya leo ambapo wafuga kuku ni wananchi ambao nchi yao ina madini ya kila aina, gesi asilia, misitu, ardhi, mbuga za wanyama, mito, milima na kila aina ya vivutio lakini wanakabiliwa na kila aina ya viroja.

Vioja hivi vinawahusu wanyang’anyi wanaokuja katika hali mbalimbali kama vile wawekezaji, wabia, wawezeshaji, washiriki katika maendeleo na wafadhili wenye kila aina ya masharti kabla ya kufadhili au kutoa misaada yao.

Wanyang’anyi wa kutoka ng’ambo wana ahueni kidogo, wabaya ni wanyang’anyi wa ndani akina Jairo, Ngeleja na wafanyakazi walio chini yao ambao wanahakikisha au wameweza kuhakikisha mipango mkakati, mipango ya muda mrefu na muda mfupi ya kumaliza tatizo la umeme haliishi bali linaendelea daima dumu huku wao wakinufaika kwa posho na teni pasenti.

0
Your rating: None Average: 2.5 (2 votes)