Ngeleja sasa amwacha Zitto ulingoni

- SAKATA LA DOWANS
HITIMISHO la mjadala wa ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Dowans Holding (Tanzania) Limited, bado halijafikiwa.
Ni wiki mbili sasa tangu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja atangazie taifa kwamba “mjadala wa Dowans umefungwa.”
Ngeleja alisema serikali imejiondoa katika ununuzi wa mitambo ya Dowans na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na tatizo lolote la uhaba wa umeme litakalojitokeza.
Kabla ya hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Dk. Idris Rashid alikuwa ametangaza kwa jazba na ghadhabu, kwamba kampuni yake inajiondoa katika mjadala wa ununuzi wa mitambo ya Dowans na kwamba “asilaumiwe iwapo nchi itaingia gizani.”
Haitarajiwi, kwa sababu zozote zile, kuona serikali ikibadili kauli yake. Hii ni kwa kuwa imetolewa baada ya kujiridhisha kuwa kauli iliyotolewa na Dk. Rashid, kwamba “asilaumiwe kwa litakalotokea,” ililenga kutisha serikali, wananchi, wawekezaji na nchi wahisani.
Ilikuwa kauli iliyojaa ubabe na iliyotoa wito kwa serikali kumfuta kazi. Kwa kauli zake, Dk. Rashid alikuwa anakiri kuishiwa maarifa, ujuzi na mbinu za kuongoza shirika muhimu la nishati nchini.
Pamoja na kwamba Ngeleja (serikali) ameshindwa kumfukuza kazi Dk. Rashid kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wake, lakini kauli yake angalau imerudisha hadhi na heshima ya serikali.
Akiongea kwa kujiamini baada ya kupima nyakati za kisiasa, Ngeleja alisema “mjadala wa Dowans umefungwa.”
Aliahidi serikali kuimarisha vyanzo vyake vya umeme na kutafuta vyanzo vipya ikiwa pamoja na kununua “mtambo mpya wa kuzalisha megawati 200 za umeme.”
Hata hivyo, katika hali ambayo mpaka sasa imeacha wengi midomo wazi, Ijumaa iliyopita, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliibuka na kutoa kauli inayoonekana kutetea Dowans.
Katika kile kilichoitwa “kumuunga mkono Zitto (Zitto Kabwe, mbunge CHADEMA),” Profesa Lipumba alisema Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPA) ya mwaka 2004 inayozuia ununuzi wa mitambo iliyotumika, “si nzuri kwa maendeleo ya nchi kama Tanzania.”
Aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, “Kama tunazungumzia shughuli za kibiashara, inabidi tuangalie mahitaji yetu ni nini, faida na hasara yake.”
Pamoja na kwamba hakusema wazi juu ya kununua au kutonunua mitambo ya Dowans, lakini msimamo wake wa kupinga Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004, umetafsiriwa kuwa Profesa Lipumba, kwa kutojua au makusudi, “ametumika” kutetea Dowans.
Hata kama sheria ya manunuzi kweli ina matatizo, lakini ni muhimu kutambua kuwa imetungwa kuzuia watawala na watendaji serikalini kutumbukiza nchi katika matumizi mabaya ya fedha na mali za umma.
Profesa Lipumba anajua kuwa tayari watawala wameingiza nchi hii kwenye mkenge kutokana na uamuzi wao wa kununua mitambo michakavu.
Mfano ni ununuzi wa kivuko cha Kigamboni katika miaka ya 1990. Kivuko kilinunuliwa kwa mabilioni ya shilingi, lakini kilikufa siku mbili baada ya kuanza kazi. Hakuna hatua iliyochukuliwa kutokana na sheria kuruhusu ununuzi wa mitambo iliyochoka.
Hivyo basi, Profesa Lipumba amejilinganisha na mtetezi mkuu wa Dowans, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe.
Katika hili, Zitto yuko tayari hata kupindisha kanuni za Bunge ili kutimiza malengo yake. Kwa mfano, Kamati ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma, haihusiki na usimamizi wa sera katika mashirika hayo. Inahusika na kuangalia matumizi ya shirika husika.
Lakini ni Zitto ambaye ameamua kubebea bango Dowans, kama vile kamati yake ni Kamati ya Nishati na Madini. Ni uvunjaji huo wa Kanuni za Bunge uliomlazimu Spika wa Bunge, Samwel Sitta kutoa mwongozo kwa wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.
Mwongozo huo unasema, endapo kamati moja imeona jambo ambalo kisera linasimamiwa na kamati nyingine katika kupitia kazi za sehemu husika, basi kamati hiyo inapaswa kulipeleka suala hilo kwa Kamati husika.
Msimamo wa Zitto umefanya baadhi ya wabunge na wananchi kujiuliza iwapo ana ubia Dowans, amepewa au ameahidiwa chochote, au ni “kazi ya kujitolea” tu ya kuwabeba Dowans na watetezi wake.
Ni Zitto anajua kuwa tayari imethibitika kuwa madai yaliyotolewa na Dk. Rashid kuwa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu, Hale na Mtera yako hatarini kukauka, hayakuwa na ukweli.
Baadhi ya wataalamu wanaoitakia mema Tanesco wanasema bila kutafuna maneno, kwamba kuna kila dalili kuwa mvua zinazonyesha katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini, zitajaza mabwawa ya kuzalisha umeme kabla ya mwezi Machi na Aprili mwaka huu.
Inatarajiwa mvua hizo zitajaza mabwawa hayo hadi kulazimisha kufungulia maji ili kuzuia kubomoka kwa kuta za mabwawa. Hili, Zitto hataki kuliona.
Tatizo kubwa ni kwamba, hakuna hata mtetezi mmoja wa Dowans anayejihangaisha kutaka kujua angalau uhalali wa mkataba, hadhi na heshima ya kampuni ya Dowans mbele ya jamii.
Hakuna anayetaka kujikumbusha historia ya kampuni hii kabla ya kutaka kuitumbukiza serikali katika mkenge. Hawataki kusema Dowans imesajiliwa lini, wapi na akina nani? Wanahisa wa Dowans ni akina nani na wako wapi?
Je, mbali ya kuwa wakurugenzi wa Dowans, wanafanya shughuli gani nyingine? Wanaaminika ndani na nje ya nchi? Kwa kiwago gani?
Majibu ya maswali haya ni muhimu sana kabla ya kushawishi serikali kununua mitambo ya Dowans. Serikali makini na inayojiheshimu haiwezi kufanya biashara na watu au makampuni ambayo uhalali wake haujathibitika.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi alishindwa kulieleza Bunge na taifa, nani mmiliki wa Dowans.
Alishindwa kuliambia Bunge na dunia kuwa wakati anakubali pendekezo la kampuni ya Richmond Development Company (LLC) kuhamishia mkataba wake kwenda Dowans alikuwa anajadiliana na nani. Hadhi na heshima ya Dowans kitaifa na kimataifa ikoje. Haya hakuyasema.
Badala yake, Karamagi alisema alipokuwa chini Canada alipigiwa simu na wamiliki wa Richmond kueleza mpango wa kuhamisha mkataba wao kwenda Dowans. Akasema, “Nami nikakubali.”
Ni hatua ya hiyo ya kukubali kuhamisha mkataba bila kuchunguza uhalali wa kampuni; uwezo wake kifedha na kitaaluma; kuongeza muda wa mkataba kinyemela kutoka mwaka mmoja hadi miwili, ambayo yalimgharimu Karamagi hadi kulazimika kujiuzulu.
Kuna taarifa za uhakika kwamba hata Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), hakuwa anaifahamu Dowans. Hata mbunge wa Igunga, Rostam Aziz alipotakiwa kutaja wamiliki wa Dowans, aliishia kusema “nawafahamu kwa kuwa kampuni yangu ya Caspian iliwahi kuwaomba kazi.”
Rostam hakuwataja kwa majina wamiliki wa Dowans. Hakufafanua anawafahamu kwa kiwango gani. Wala hakuweza kukidhi matakwa ya Bunge na umma uliotaka kujua uhusiano wake, Dowans na Richmond.
Taarifa kwamba Dowans ilisajiliwa nchini Costa Rica, zimeanza kusikika sasa baada ya mipango ya kuuza mitambo kukwama. Lakini kuna ushahidi kwamba baada ya Bunge kupata taarifa kuwa Dowans ilisajiliwa nchini Costa Rica, iliamua kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu (AG) wa nchi hiyo ili kupata ukweli wake. Tayari amekana kufahamu Dowans.
Katika mazingira hayo, Zitto alipaswa kupima kama serikali inaweza kujitumbukiza katika uchafu huo. Je, kwa kufanya hivyo serikali haiwezi kuchochea wananchi kuwanyima kura? Labda kama hilo ndilo alilolilenga Zitto.
Vinginevyo, suala la nchi kuingia katika giza, si suala linalomhusu Zitto. Ni suala linalohusu serikali. Ni jukumu la Zitto kuimbia serikali itimize wajibu wake kama ilivyoahidi wakati wa kuomba kura kwa kutafuta vyanzo vingine vya umeme.
Kwamba serikali ilijua kuwa azimio la Bunge lililotolewa Februari 2008 lilitaka kuvunjwa kwa mkataba wa Dowas; basi serikali haipaswi kuingiza nchi gizani kwa kisingizio cha mitambo ya megawati 100 ya Dowans.
Watetezi wa Dowans, badala ya kutaka kuingiza nchi katika mgogoro, wanapaswa kujiuliza na kuuliza serikali: Iko wapi mipango ya kupatikana umeme kutoka miradi mikubwa ya maporomoko ya Mto Rufiji unaotosha kwa nchi nzima na mwingine kuuzwa nje ya nchi?
Je, sera ya serikali ni hii ya umeme wa kuungaunga, kwa huyu kutoa megawati 20, yule 30 na huyu 100 kama vile nchi inatunga shanga?
Taarifa za kitaamu zinasema umeme unaoweza kuzalishwa na maporomoko ya Mto Rufiji ni megawati 3,956 kwa siku. Mahitaji ya umeme kwa sasa nchini hayazidi megawati 1,200 kwa siku. Hii ina maana kwamba serikali ingekuwa na akiba ya megawati 2,700 za umeme kwa siku.
Akiba hiyo ingeweza kuuzwa kwa nchi jirani za Msumbuji, Zimbabwe na Afrika Kusini. Si hivyo tu, kwa mradi huu, nchi ingeweza kufunga mabwawa yote ya sasa yanayozalisha umeme na kuyawasha wakati wa dharula tu.
Hapa taifa lingeweza kusitisha mikataba yote ya kinyonyaji liliyoingia na makampuni ya kuzalisha umeme. Aidha, umeme unaotokana na nguvu za maji hauna gharama za Capacity Charge (gharama za kuweka mtambo).
Utafiti uliofanywa katika Mto Rufiji unaonyesha kwamba kuzalisha umeme katika mto huo ni nafuu ikilinganishwa na vyanzo vingine vya umeme.
Umeme unaweza kuongeza tija katika kilimo katika bonde hili lenye hekta zipatazo 300,000. Umeme kutoka bonde hili waweza pia kutumika kwa kilimo na uzalishaji mwingine katika mabonde ya Kilombero, Usangu na Ruaha yaliyoko chini ya Mamlaka ya Maendeleo ya RUBADA.
Kama serikali itawekeza katika kilimo cha kisasa cha umwagiliaji wa mpunga, inaweza kuzalisha tani 7.5 milioni kwa mwaka. Hii ina maana kwamba njaa litakuwa suala la historia tu.
Swali la kujiuliza ni je, haya hayafahamiki kwa watetezi wa Dowans? Je, kwa nini serikali haitaki kuwekeza katika kutafuta umeme kupitia maporomoko ya Mto Rufiji, badala yake inang’ang’ania kununua mitambo ya Dowans?
Kuna taarifa kuwa kila mfanyakazi wa Tanesco anapewa wastani wa uniti 750 kwa mwezi kwa yeye kulipa aslimia 30 tu ya bei ya kawaida. Nchi mzima ina wafanyakazi zaidi ya 5,000.
Kwa utaratibu huu, wafanyakazi wa Tanesco wanatumia karibu Sh. 4.8 bilioni kwa mwaka. Hili si tatizo kama shirika lingekuwa linaendeshwa kwa tija.
Lakini katika mazingira ya sasa ya mikataba ya kinyonyaji na ufujaji wa rasimali za shirika, fedha zinazotumiwa na wafanyakazi hawa kwa muda wa miaka 10 zinatosha kujenga mtambo wa umeme kupitia maporomoko ya Mto Rufiji.
Lakini kuna hili la kufananisha Dowans na IPTL. Mkataba kati ya serikali na IPTL ulifungwa mwaka 1995 baada ya nchi kukumbwa na ukame. Mkataba wa dharura ukafanywa kuwa wa miaka 20!
Wamiliki wa IPTL walidanganya serikali kwamba mitambo yao ina thamani ya dola za Marekani 150 milioni. Kwa thamani hiyo, serikali ilikuwa inalipa Capacity Charge ya dola 3.4 milioni kwa mwezi.
Lakini baada ya serikali kufikisha IPTL katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, ilibainika kwamba mitambo hiyo ina thamani ya dola 90 milioni.
Kwa muda wa miaka 20 serikali italipa kile kinachoitwa, “Capacity Charge” ya dola 800 milioni, wakati mtambo una thamani ya dola 90 milioni.
Hii ina maana kwamba hata kama serikali ingeamua kununua mtambo huo na kuutosa baharini, mara baada ya kuwekeza katika maeneo kama Rufiji, ingeokoa zaidi ya dola 800 zinazoweza kutumika kwa kazi nyingine.
Hapa ndipo Bunge liliposema mitambo ya IPTL inunuliwe ili kuliondolea taifa hasara ya kudumu. Haya ndiyo Zitto na Kamati yake walipaswa kuyasimamia na kuwaeleza Watanzania. Si kuhubiri Dowans.
Haiingii akilini kusikia tena kuwa bado serikali inajadiliana na wenye mitambo ya Dowans ambao hawajiweki wazi ili, kwa vyovyote iwavyo, mitambo hiyo iweze kununuliwa.
Lakini kama serikali itaenda kwa kauli ya Ngeleja, italazimu watetezi wa ununuzi wa mitambo ya Dowans, wakiwemo Zitto na Lipumba, watangaze maslahi yao katika hili, kwani hakuna sababu ya kuliumisha kichwa taifa.