Ni hatari demokrasia ikipuuzwa


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

JUMAPILI wiki hii, wananchi wa Arumeru Mashariki na sehemu kadha nchini watakuwa kwenye uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi za uongozi – ubunge na udiwani.

Hakuna nafasi ambayo inapiganiwa sana kama ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki. Jimbo hili lilikuwa linaongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), na sasa Chama cha Demekorsia na Maendeleo (CHADEMA) na vyama vingine vinapigana kulinyakua.

Kama ilivyokuwa katika chaguzi kadhaa zilizopita lugha ya kejeli, vijembe, mipasho na vituko vimeendelea kutawala huko Arumeru. Matumizi ya nguvu hayajawa mabaya sana lakini siku hizi chache zilizobakia zitaamua.

Wananchi wanaoenda kupiga kura wanastahili kupata matokeo ya kura zao. Wananchi hawa wanataka kutumia sauti pekee ambayo watawala wanaielewa – yaani kura - ili waweze kutuma ujumbe uliokusudiwa.

Jaribio lolote la mtu yeyote kujaribu kuzuia wananchi kupiga kura kwa uhuru na amani ni jaribio la kuwafunga midomo wasizungumze; ni utekaji nyara wa demokrasia. Demokrasia inadaiwa, isipokubaliwa hupiganiwa.

Kuna watu wanaamini kuwa demokrasia italetwa kwa hisani au kwa huruma ya watawala. Kwamba demokrasia yaweza kuletwa kwa kuwapigia watu magoti na kuwabembeleza.

Kweli kabisa wapo watu wanaofikiri - katika mioyo yao - kuwa demokrasia inaweza kujengwa bila msuguano kati ya watawala na watawaliwa, walio nacho na wasio nacho, wenye nguvu na wale wasio na nguvu. Hakuna nchi iliyowahi kujenga demokrasia kwa kuremburiana, kukonyezana na kukumbatiana.

Demokrasia hujengwa kwa migongano.

Yaani utawala ambao wananchi wana nguvu ya mwisho ya kutawala hujengwa kwanza kabisa kwa migongano. Kuna aina tatu kubwa ya migongano.

Mgongano wa kimaslahi, mgongano wa kifikra na mgongano wa damu. Harakati za kupigania demokrasia zinapofikia mgongano wa damu maana yake ni kuwa njia nyingine zote za kupata demokrasia zinakuwa zimeshindwa isipokuwa mapambano na mgongano wa kulazimisha mabadiliko.

Mahali popote panapotokea tofauti kubwa ya kimaisha kati ya wale walionacho na wale ambao wanatamani kuwa nacho; au pale ambapo kuna matabaka ya wenye nguvu na madaraka (mabwana) na wale wasio navyo (watwana au watumwa) kunatokea mgongano wa kimaslahi.

Wale walio kwenye madaraka na wenye kunufaika na madaraka hayo hutaka kuendeleza hali yao hiyo ya kuwa juu ya wengine na hivyo maslahi yao ni kuhakikisha kuwa wao wanadumu katika kufanikiwa kwa milele.

Sasa mgongano wa kimaslahi mara nyingi huweza kutulizwa kwa kutoa maslahi fulani fulani kwa wale walio chini. Yaani, wale wenye maslahi ya juu zaidi huamua kuridhisha maslahi kidogo ya wale walio chini ili kuwaridhisha.

Ni kanuni ile ile ambayo baba au mama ambaye amechoshwa na kelele za mtoto kulia huamua kumpa doli achezee au peremende alambe. Wote wawili maslahi yao yanaridhishwa - baada ya kelele kuisha na mtoto ya kuoneshwa kupendwa na kujaliwa.

Katika taifa, yako maslahi ya madaraka na kutawala na maslahi ya huduma na mahitaji mbalimbali kutimizwa. Walio madarakani wana lengo la kuendelea kutawala ili kutimiza mahitaji yao mbalimbali hasa ya mali na hali ya juu ya maisha.

Wale watu wa chini, maslahi yao ni kupata huduma mbalimbali za kijamii na nafasi za kuweza kuishi katika hali ya unafuu. Hata hivyo, hawa wa chini hawana madaraka au nguvu (wanajiona hawana) ya kujitimizia mahitaji yao.

Hawa wa chini wanategemea maamuzi na utendaji wa wale wenye madaraka. Kwa maneno mengine, wananchi hutegemea maamuzi na utendaji wa wale walio kwenye serikali ili mahitaji yao ya maji, barabara, afya bora, nafasi za ajira na mengineyo yatimizwe.

Hata hivyo, kwa vile mahali popote penye utawala wenye kutawaliwa ni wengi kuliko wale wenye kutawala, basi ni vigumu sana kwa watawala kutimiza mahitaji yote ya watawaliwa kwa kiwango cha juu cha kuridhisha.

Matokeo yake watawala hujaribu kuwaridhisha walio chini kwa kiwango cha chini ili kuwanyamazisha. Kwa mfano, wanaweza kujenga shule zenye viwango vya chini sana au barabara ambazo zikimalizika zinaonekana nzuri, lakini miezi michache baadaye zinahitaji matengenezo makubwa.

Mgongano huu wa maslahi una matokeo ya wazi kabisa katika maisha ya wananchi. Inafika wakati wananchi wanatambua kuwa matatizo yao mbalimbali (maslahi) yanahusiana moja kwa moja na watawala walioko madarakani na hivyo wananchi wanawaasi viongozi wao.

Katika mgongano wa kimaslahi, jamii ambayo ina migongano ya kimaslahi ambayo inagusa maisha ya watu mbalimbali au makundi mengine ya kijamii; maslahi yao husababisha watu waanze kufikiria.

Watu huanza kuuliza maswali na kuhoji kwanini hali fulani ipo na kwanini inaendelea kuwepo. Kwa kutumia njia mbalimbali mijadala hufanyika katika ulimwengu huu wa teknolojia ya kisasa na fikra za watu mbalimbali hupitishwa kutoka upande mmoja wa nchi au dunia kwenda upande mwingine.

Mawazo na fikra hizi huchochoea majibu kutoka kwa watawala. Majibu ya watawala kwa kiasi fulani hutuliza baadhi ya watu. Yaweza kuwa majibu ya kejeli, dharau au kupuuzia lakini kwa vile yanatolewa na wenye madaraka na nguvu basi baadhi ya watu huyapokea, huyakumbatia na kuyabusu kama zawadi ya mkungu wa ndizi.

Pamoja na hayo wachache wataendelea kuuliza na kuhoji. Watahoji juu ya uwezo wa watawala, watahoji juu ya nia na mipango ya watawala, na watahoji dhamira na maamuzi ya watendaji serikalini.

Kwa kadiri watakavyoendelea kuhoji ndivyo majibu mepesi mepesi yatakavyozidi kukataliwa. Hapa ndipo pande mbili zenye fikra tofauti juu ya jambo lile lile huibuka na huanza kugongana.

Kwa nchi yetu hivi sasa, bado ni mgongano wa nafasi za maslahi ya kisiasa. Wapo wale wenye kufurahia nafasi hizo sasa na wale wenye kutamani kushikilia nafasi hizo au zaidi ya hizo.

Kwa watu wasio na madaraka wanajikuta wanawekwa pande mbili za kisiasa – yawezekana  zipo nyingine ndogondogo – ya nani anamuunga mkono nani na nani atanufaika na nini akiingia madarakani.

Katika nchi ambazo zimepiga hatua za kidemokrasia mgongano huu hugeuka na kuwa mgongano wa kiitikadi. Mara nyingi mgongano wa kiitikadi ukiiva sana huweza kusababisha ule mgongano wa mwisho.

Kuhusu mgongano wa damu/mgongano wa kimapinduzi, huu hutokana na kushindwa kupatikana na ufumbuzi wa mgongano wa kimaslahi na mgongano wa kifikra; kushindwa kutatuliwa huko husababisha mgongano wa damu.

Yaani, watu katika jamii fulani wanafikia mahali wanashindwa kutatua tofauti zao au kuridhishana katika matamanio yao, na hivyo hulazimika kutumia siyo nguvu za “hoja” bali hoja za “nguvu.”

Hapa ndipo watawala katika kujaribu kuzima kuenea kwa fikra wasizozitaka huanza kutumia nguvu, mauaji, watu kupotezwa, vifungo na mengineyo hutumika.

Tatizo ni kwamba mbinu hizo zaweza kufanikiwa kwa muda fulani na kwa baadhi ya watu. Lakini roho ya mwanadamu imeumbwa kuwa huru; haiko tayari kukubali kukandamizwa milele, kunyanyaswa daima au kupuuzwa bila kukoma.

Roho ya mwanadamu ikishafikishwa mahali kwenye kona simba anapowindwa na kujikuta kwenye kona ya mlima akiwa amezungukwa na wawindaji, hujitetea. Mwanadamu atajitoa mhanga kupigania nafasi ya kuwa haki, kupigania haki yake na thamani yake, naam mwanadamu atakuwa tayari kupoteza vyote ili kupigania utu wake.

Kama wananchi wanafika mahali na kuona mabadiliko wanayoyataka hayawezi kuja kwa sanduku la kura au kwamba kwenye sanduku la kura sauti yao inapuuzwa na kukejeliwa, watajaribu tena na tena kuleta mabadiliko wa njia hiyo na kwa mazungumzo.

Lakini ole wetu kama wananchi watafikia mahali waone kuwa njia za kidemokrasia za kuleta mabadiliko zimeshindikana. Ole wetu kama wananchi wataamua mgongano wao usiwe tena wa maslahi na fikra, bali mgongano utakaolazimisha maslahi yao yasikilizwe kwa damu yao.

Ole watakaiona siku hiyo!

0
No votes yet