Ni mwaka wa uamuzi siyo uchaguzi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 06 January 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Kisima cha Mjadala

HUU ni mwaka wa uchaguzi. Mwaka ambao utaamua ni mwelekeo upi kama taifa tuuchukue. Mwaka huu ni mwaka wa uamuzi; uamuzi kati ya yale yale au tofauti, vile vile au tofauti, walewale au tofauti. Ni mwaka wa kuamua kuridhika au kutoridhika.

Ndugu zangu, uamuzi hutangulia uchaguzi. Tunaamua kwanza kabla ya kuchagua. Watu wanaofikiria kuchagua bila kuamua kwanza, hujikuta baadaye katika dimbwi la majuto na masikitiko kwani kile walichokichagua sicho ambacho walikuwa wanakitaka hasa.

Ni sawa sawa na mtu ambaye anaamua kwenda kulima lakini hajui atapanda nini. Ni muhimu basi, kwa mtu huyo kuamua kulima mahindi na hivyo kujiandaa kiutalamu, zana, mbolea na kila kinachohitajika kwa ajili ya kilimo hicho.

Atakuwa ni mtu ajabu yule ambaye ataanza kulima pamba kwa sababu anazo mbegu wakati ardhi, hali ya hewa na mahitaji mengine ya kilimo hicho hana uwezo wa kuyatimiza.

Vivyo hivyo katika uchaguzi huu wa mwaka huu. Wengi watatuambia ni mwaka wa “uchaguzi” kwamba tuchague “viongozi wazuri” na wale “wanaotufaa.”

Na kama maneno ya rais yana ukweli basi asilimia 70 ya wananchi wetu watakimbilia kwenda “kuchagua” yule wanayemtaka. Kwa haraka tunaweza kuamini mojawapo ya hadaa kubwa za kisiasa wakati wa uchaguzi.

Nimesema hapo juu kuwa uamuzi hutangulia uchaguzi; maana yake ni kuwa mpigakura ni lazima aamue anataka nini siyo mgombea anasema nini; lazima aamue anahitaji nini na siyo kusubiri mgombea anaahidi nini; aamue kukataa nini siyo kusubiri mgombea ampe nini. Uamuzi basi ni kitu muhimu kwenye uchaguzi kabla saa ya kuingia kwenye chumba cha kura.

Tunataka nini?

Katika hili wapiga kura watatofautiana. Kwa muda mrefu kampeni zetu za kisiasa zimezunguka kwenye ahadi za barabara, shule, kliniki, maji, umeme na mengineyo. Kampeni hazinogi isipokuwa hadi ziwe na ahadi za vitu hivyo. Na kwa muda mrefu wanasiasa wetu wametumia mahitaji ya vitu hivyo kuweza kujiuza kwetu.

Hili utaliona pia kwenye hotuba ya rais Kikwete ya kuuaga mwaka 2009 na kuukaribisha mwaka huu mpya. Katika hotuba hiyo Kikwete kama ilivyotarajiwa na baadhi yetu ameendelea kuzungumzia yale yale “mahitaji” ambayo yeye na chama chake wanajua Watanzania wanataka yatimizwe.

Kwa vile hicho ndicho wanachofikiria basi ametoa ahadi nyingine za nini kitafanyika ndani ya mwaka huu; ameahidi barabara kukamilika, kuongeza bajeti na ahadi kedekede zinazofanana na zile zile za uchaguzi. Lakini bado swali ambalo hawajatuuliza wananchi ni “nini tunataka?”

Kuna vitu tunavyovitaka lakini sivyo vyote tunavyovihitaji. Kuna vitu vinavyoweza kufanywa na sekta binafsi, kikundi na taasisi huru zisizo za kiserikali. Lakini kuna vitu ambavyo tunavihitaji.

Lakini kuna jambo moja kubwa ambalo limenishangaza katika hotuba ya rais Kikwete. Nalo ni matokeo ya darasa la saba. Rais ameshangaa matokeo waliopata watoto wetu. Binafsi sielewi kwanini rais anashangaa!

Tatizo kubwa la mpango wao wa elimu ya msingi kama tulivyoukosoa miaka mitatu iliyopita ni kuwa umejengwa katika kuongeza wingi. Madarasa yaliojengwa hayana mengi hayana viwango, shule hazina walimu, hakuna vitabu vya kiada na ziada. Ili mradi zinazoitwa shule, zimegeuka kuwa vijiwe vya watoto kukulia.

Bahati mbaya hili haliko katika elimu tu. Lipo karibu katika kila eneo. Rais Kikwete anatilia mkazo wingi zaidi. Hicho ndicho wanafikiri tunakitaka. Kwamba vitu vingi vitatutuliza. Ni sawa sawa na kumpatia mtoto mdogo vitu vya kuchezea kwa wingi wake bila kujali kama mtoto yule anasaidiwa katika makuzi yake na vitu hivyo.

Nini tunahitaji?

Hivyo basi utaona swali ambalo tunahitaji kulijibu kabla ya kuamua na hatimaye kuchagua ni kujua nini hasa tunachohitaji?

Je, tunahitaji shule nyingine nyingi za msingi au tunahitaji huduma bora, elimu bora kwenye shule zilizopo? Je, tunahitaji kituo kipya cha afya au kuboresha kilichopo kwa kukifanya kuwa cha kisasa? Je, tunahitaji barabara mpya ya lami au tunahitaji kupanuliwa hizi zilizopo? Tunahitaji serikali kununua magari mengi zaidi ya kifahari wakati watu wanakufa njaa kwa kukosa maji?

Ni katika hili ndipo kashfa mpya ya Benki Kuu ya taifa (BoT) inaeleweka vizuri zaidi. Kwamba kwanini serikali ya rais Kikwete imeridhia matumizi ya Sh. 3 bilioni kwa ujenzi kwa nyumba mbili za wafanayakazi wa benki wakati kina mama wajawazito katika hospitari ya Temeke wanalundikana kwa kukosa chumba cha mapumziko baada ya kujifungua ambacho gharama yake chini ya Sh. 500 milioni.

Siyo kina mama wa Temeke tu, bali hata watoto wetu katika shule kadhaa nchini wanaendelea kukosa vyoo vyenye hadhi ya kibinadamu, madarasa yanayoendana na elimu inayotolewa na wafanyakazi wetu wakiendelea kuhenyeka kila kukicha.

Leo hii wanapanga kutumia mabilioni ya shilingi kuboresha viwanja vya ndege wakati watu wetu wanahangaika na njaa katika mikoa mbalimbali kwa sababu za kizembe –siyo Mungu wala ukame.

Inakuwaje kwenye taifa lenye samaki, matunda na vyakula bwelele watu wake wafe njaa? Hivi, kina Kikwete wanajua kuwa hata Marekani huwa wanapata ukame na mazao yao yanapungua kwa sababu ya ukame huo, lakini hatuwaoni wakilalamikia “njaa” ?

Au wanafikiri ni kwa sababu Wamarekani ni “Wamarekani” na wana akili zaidi ya kukabiliana na majanga na uwezo mkubwa wa kukabiliana na majanga.

Ndugu zangu, tunavyoendelea kutafakari sababu za Kikwete kutokugombea tena mwaka huu mojawapo inazidi kujitokeza taratibu; kushindwa kwake kuliongoza taifa kuelekea kujitegemea.

Endapo tutaamua kumchagua tena na kwa kufanya hivyo kuwachagua wasaidizi wake wale wale, basi tutakuwa tumeamua kuchagua watu wale wale walioshindwa kuongoza; sera zile zile zilizotufikisha hapa, mipango ile ile yenye kuendeleza utawala wa mfumo wa kifisadi.

Tukifanya hivyo basi tutakuwa tumeamua kuchagua matokeo yale yale; halafu tutajiuliza tumefikaje hapa. Uamuzi ni wetu. Tuamue kutaka mabadiliko; na tuchague mabadiliko!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: